Search This Blog

NILIOA JINI NA KUZAA NAE - 4





    Simulizi : Nilioa Jini Na Kuzaa Nae

    Sehemu Ya Nne (4)



    ILIPOISHIA

    “Aliwahi kunieleza”

    “Je ulikubali kwa hiyari yako?”

    “Hapana, sikukubali”

    “Alikuwa anakutisha?”

    Hapo nikanyamaza. Sikutaka kusema ukweli kuwa alikuwa ananitishia maisha.

    Yule mama alitambua mawazo yangu, akaniambia.

    “Sema usifiche”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo alikuwa ananitisha” nikamwambia.

    Banuna akanitazama kwa uso wa tadhaa.

    “Alfred sema ukweli, nimekutisha mimi? Si tumekubaliana tuoane, uliniambia kuwa umenipenda?” Banuna akaniambia lakini sauti yake haikuwa na nguvu kwa vile maneno aliyosema yalikuwa ya uongo.

    SASA ENDELEA

    Sikumjibu chochote. Nilikuwa nimeinamisha kichwa changu chini. Sikutaka kutazamana na macho yake.

    Mama mtu akakasirika.

    “Banuna, wewe muongo. Umekuja kunidanganya hapa!”

    Banuna akamjibu kwa kiarabu. Pengine hakutaka nisikie uongo wake. Lakini mama yake aliendelea kuchachamaa. Wakawa wanajibizana kwa kiarabu.

    Mwisho Banuna alinyanyuka kwa hasira. Sikujua aliambiwa nini. Mama yake naye akanyanyuka. Banuna alitamka neno lililomuudhi yule mama, akampiga kibao Banuna.

    “Ondoka hapa fedhuli mkubwa!” Mwanamke huyo wa kijini alimwambia Banuna kwa ukali kisha akaongeza.

    “Mrudishe kijana wa watu kule ulikomchukua. Mrudishe sasa hivi halafu ukome kumfuatafuata tena!”

    Banuna alipopigwa kibao aliondoka huku maneno yakimtoka mdomoni.

    “Sitamuacha hata ukunipiga. Nimeshampenda. Nitaendelea naye hivyo hivyo!” akamjibu mama yake na kutokomea kwenye pazia.

    Yule mama alikuwa akumfuata nyuma huku akijibishana naye kwa kiarabu. Na yeye aliingia kwenye pazia hilo hilo. Sauti zao za kujibizana zikawa zinasikika kwa ndani. Baadaye kukawa kimya.

    Nikajikuta nimeachwa peke yangu mahali hapo. Kwa mara ya kwanza nilianza kusikia uoga hasa vile ambavyo mwenyeji wangu aliyeambiwa anirudishe, amenikimbia kwa hasira.

    Nilijua kuwa nilikuwa nimemuudhi kwa kumkana mbele ya mama yake ambaye ingawa alikuwa jini, alikuwa muadilifu sana.

    Alipoambiwa na Banuna kuwa anataka kuoana na mimi, alitaka uthibitisho kutoka kwangu. Nilipopinga jambo hilo aliamua kumuonya Banuna asinifuate tena, lakini Banuna alikuwa kisoi.

    Niliendelea kukaa pale kwa muda kidogo kabla ya kumuona jini mwingine mwanaume aliyenifuata na kuniambia.

    “Mama ameniambia nikurudishe kwako kwa usalama, sasa inuka twende”

    Niliponyanyuka akaniambia.

    “ Nifuate”

    Nikamfuata. Tulipita katika njia ileile tuliyopita na Banuna mpaka tukatokea ile sehemu yenye kiza. Jini huyo hakuniambia nimshike bega, hivyo ikanibidi niwe karibu naye sana ili tusipoteane. Tukaenda mpaka tukatokea kule juu ya mnara.

    Yule jini akachutama na kuniambia.

    “Kaa kwenye mabega yangu”

    Nikakaa. Akanibeba na kuniambia nifumbe macho, nikafumba macho. Vile ananyanyuka tu, nikahisi tunaibuka juu ya bahari!

    Nilifumbua macho yangu bila kuambiwa. Ilikuwa miujiza mikubwa ambayo sikupata kuiona maishani mwangu.

    Yule jini alinipeleka hadi ufukweni mwa bahari, akachutama na kuniambia nishuke. Nikashuka.

    Niliposhuka alichora msitari kwenye tope, akaniambia.

    “Fumba macho yako halafu vuka msitari huu. Ukishavuka fumbua macho yako”

    Nikaenda nyuma ya ule msitari, nikafumba macho yangu na kuinua hatua kuvuka ule msitari. Nilipofumba na nilifumbua macho na kujikuta nipo mbele ya mlango wa nyumba ninayoishi Makorora.

    Niliangalia kila upande ili kujiridhisha kuwa kweli nilikuwa nyumbani ninakoishi. Nikaona ni kweli. Macho yangu hayakunidanganya.

    Ilikuwa bado usiku. Na kitu kingine cha ajabu ni kuwa nguo zangu zilikuwa kavu kabisa. Nilisimama kwa muda mbele ya huo mlango nikifikiria kati ya kubisha mlango niingie ndani, au nirudi kwa Juma.

    Kwa vile ilikuwa usiku, kubisha mlango ilikuwa ni vyema zaidi ila nilipata shaka kuwa naweza kuingia chumbani mwangu na kukutana na Banuna mwenye hasira.

    Wazo hilo lilinifanya niamue kwenda kwa Juma. Ilikuwa ni hatari usiku ule kutembea nikiwa peke yangu lakini nilijikaza kiume. Nikatembea haraka haraka kuelekea mtaa wa pili.

    Mwili ulikuwa unanisisimka kila nilipokumbuka nilivyopelekwa ujinini. Sasa niligundua kuwa Banuna alipokuja kunichukua, sikuwa na akili yangu. Nilikuwa kama niko kwenye ndoto. Lakini kwa muda ule niliorudishwa nilijiona niko sawa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niseme ukweli kama ningekuwa na akili yangu timamu wakati Banuna anakuja kunichukua, nisingekubali. Tungebishana sana na ningekimbia. Na yeye kwa kujua hilo ndio maana alinizuga akili.

    Nilipofika nyumbani kwa Juma nilijaribu kufungua mlango, kwa vile nilipoondoka na Banuna hatukuufunga. Lakini nikaukuta umefungwa.

    Nikaenda kwenye dirisha la chumba cha Juma, nikamgongea huku nikimuita.

    “Juma! Juma!”

    Mara moja Juma alizinduka na kuuliza.

    “Wewe nani?”

    “Mimi Alfred”

    “Alfred?” Juma alionekana kushituka, akauliza. “Alfred si yumo humu ndani?”

    “Ni mimi. Nilikuwa nimetoka, wewe ukiwa umelala”

    Mara nikaona taa inawashwa.

    “Alfred ulitoka saa ngapi, mbona mlango umefungwa kwa ndani?” Sauti ya Juma ikauliza kutoka ndani.

    “Nifungulie, nitakueleza”

    Baada ya ukimya wa dakika mbili hivi, Juma akafungua mlango wa nje.

    “Ulitokaje humu ndani?”

    “Tuingie ndani nikueleza”

    Tukaingia ukumbini. Juma akaufunga mlango wa nje kisha tukaingia chumbani. Mimi nilikaa kwenye kiti, Juma akakaa kwenye kitanda.



    “Juma utashangaa nikikueleza kuwa Banuna alikuja kunichukua huu usiku na kunipeleka kwao ujinini chini ya bahari!” nikamwambia Juma.

    “Unasema kweli Alfred?”

    “Huwezi kuamini Juma lakini hivi ninavyokwambia ninatoka ujinini”

    “Alikuja kukuchukua saa ngapi?”

    “Sijui ilikuwa saa ngapi lakini alinipeleka baharini, tukazama chini ya bahari na kukuta mji wao”

    “Acha bwana!. Mji uko chini ya bahari!”

    Hapo nikamueleza Juma jinsi nilivyoondoka na Banuna, tulivyozama chini ya bahari na kutokea katika mji wa majini. Pia nilimuelezea yale yaliyotokea wakati tulipokuwa ndani ya jumba la majini hao lenye mnara mrefu.

    “Mama yake amekataa msioane?” Juma akaniuliza baada ya kumueleza kisa kizima.

    “Amekataa. Nafikiri yule mama alitaka nikubali mwenyewe na sio kulazimishwa kama anavyotaka Banuna”

    “Sasa itakuwaje, kwa maana kesho ndio napata mshahara ambao tumepanga nikupe uende Zanzibar?”

    “Banuna alipokatazwa asinifuate, alisema kwa kiburi kuwa atanifuata. Sasa sijui itakuwaje!”

    “Kama mama yake amemkataza, unadhani anaweza kuendelea kukufuata kweli?”

    “Amesema ataendelea”

    “Labda amesema kwa hasira tu”

    “Siwezi kujua. Na hata alipoambiwa anirudishe huku alikataa. Nimerudishwa na jini mwingine”

    “Sasa unaweza kwenda Zanzibar kesho lakini Banuna akawa hana shughuli na wewe tena. Hapo ni sawa na kuharibu pesa bure. Au unaweza usiende lakini keshokutwa ukaona amekufuata”

    “Hapo ndipo penye utata”

    “Sasa tusubirishe kwanza tuangalie. Kama atakutokea tena utakwenda”

    “Sawa”

    Nikaendelea kuzungumza na Juma hadi asubuhi kwani hatukulala tena.

    Kutoka siku ile ulipita mwezi mzima sikumuona Banuna. Hapo nikapata uhakika kuwa Banuna alishaamua kuachana na mimi kwa sababu haikuwa kawaida yake kupitisha hata wiki moja bila kunitokea.

    Ile hofu niliyokuwa nayo ya kupata vitisho vya Banuna, sasa ikaniondoka. Nikaamua kurudi chumbani kwangu.

    Maisha sasa yakawa ya utulivu na ya amani. Siku moja nilipata barua ya kuitwa katika kampuni moja ya ulinzi ambako nilikuwa nimeomba kazi. Nikaenda. Nilifanyiwa usaili na baadaye niliambiwa niende kesho yake kuanza kazi.

    Siku iliyofuata nilipokwenda niliajiriwa kazi ya ulinzi. Nilipewa sare za kampuni nikavaa a kupelekwa kwenye duka la muasia mmoja kuanza kazi ya ulinzi wa duka hilo.

    Nilikuwa naingia kazini saa mbili asubuhi na kutoka saa kumi jioni. Nikishakunywa chai asubuhi ndiyo nashinda hadi saa kumi jioni ninapotoka na kurudi nyumbani. Kuanzia saa kumi anaingia mlinzi mwingine ambaye anaendelea hadi asubuhi ya siku ya pili.

    Zamu hizo zilikuwa zinabadilika kwa wiki. Anayeingia mchana anabadilishiwa zamu na kuingia usiku.

    Katika juma lile la kwanza nilikuwa nimepangiwa zamu ya mchana. Hii ilikuwa nzuri kwani iliniwezesha kulala nyumbani kuliko zamu ya usiku ambapo unalazimika kukesha macho usiku kucha.

    Siku tatu baada ya kuanza kazi yangu alikuja msichana mmoja wa kiarabu pale dukani. Akanunua vitu vingi. Alipokuwa anatoka nikamsaidia boksi moja na kumpelekea kwenye gari lake. Akanishukuru kisha akanipa shilingi elfu ishirini kama bahashishi yangu.

    Kwanza sikuelewa pesa hizo alizonipa zilikuwa za nini. Nikawa nimeduwaa na kumuangalia ili aniambie pesa hizo zilikuwa za nini.

    “Ni zako. Nimekupa kwa msaada wako” akaniambia huku akifungua mlango wa gari hilo na kujipakia.

    Kwa kweli nilimshangaa msichana huyo kwa kunipa pesa zote hizo kwa msaada mdogo tu. Hata hivyo nilishukuru na kuzitia mfukoni. Msichana huyo akaliwasha gari na kuondoka.

    Nikarudi kwenye kiti changu kilichokuwa kando ya mlango wa duka hilo, nikaendelea na kazi yangu. Kabla ya wiki ile kumalizika yule msichana alikuja tena pale dukani. Kwa bahati mbaya vitu alivyotaka kununua havikuwepo. Alipotoka akanipa tena shilingi elfu ishirini kisha akaenda kwenye gari lake na kuondoka.

    Siku nyingine tena wakati niko katika zamu ya mchana, msichana huyo akaja tena Nakumbuka ilikuwa saa kumi wakati nabadilishana zanu na mlinzi mwenzangu. Msichana huyo hakushuka kwenye gari. Alisubiri mpaka wakati naondoka akanifuata na gari na kusimama karibu yangu. Na mimi nikasimama.

    Msichana huyo alitoa kichwa kwenye dirisha la gari na kuniambia.

    “Kijana hujambo?”

    “Sijambo. Habari yako?”

    “Nzuri. Unarudi nyumbani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo,ninarudi nyumbani”

    “Ingia garini nikupeleke. Nina mazungumzo na wewe!”

    “Una mazungumzo na mimi?” nilimuuliza kama vile sikumsikia vizuri.

    “Mbona umeshituka?”

    “Hapana, sikushituka”

    “Basi ingia garini”

    Nikafungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia. Msichana akalindoa gari.





    “Unaitwa nani?” akaniuliza.

    “Naitwa Alfred”

    “Umeanza hizi kazi za ulinzi lini?”

    “Nina muda mrefu isipokuwa kwenye kampuni hii niliyoko sasa, nimeanza siku chache tu zilizopita”

    “Sawa. Una mke na watoto?”

    “Hapana, sijaoa bado”

    Msichana aliniangalia akatabasamu kabla ya kuniuliza.

    “Una mchumba?”

    Na mimi nikatabasamu na kutikisa kichwa.

    “Sina mchumba” nikamjibu.

    “Unangoja nini?”

    “Najiweka sawa kwanza”

    “Unalipwa mshahara wa kiasi gani kazini kwako?” Msichana akaniuliza baada ya kimya kifupi.

    “Mshahara mdogo tu… haufiki hata laki moja”

    “Nimekuuliza hivyo kwa maana. Ninahitaji mlinzi kwenye nyumba yangu. Nimeona wewe unafaa. Nitakulipa mshahara mzuri”

    Niliukumbuka sana wema wa yule msichana, nikamuuliza.

    “Nyumba yako iko wapi?”

    “Iko Raskazoni”

    Eneo alilolitaja lilikuwa linaishi watu wenye vipato vya juu.

    “Unahitaji kulindiwa nyumba yako wakati wa mchana au usiku?”

    “Kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi asubuhi”

    “Sawa”

    “Uko tayari?”

    “Utakuwa unatoa likizo na siku za mapumziko?”

    “Nitazingatia sheria zote za kikazi. Kwa wiki kutakuwa na siku moja ya mapumziko zikiwemo siku za sikukuu na likizo ya mwaka. Pia ukiwa mgonjwa, nitagharamia mimi matibabu yako”

    “Sawa. Utanilipa mshahara wa kiasi gani?”

    “Nitakulipa mshahara mzuri. Utaniambia wewe unataka nikulipe mshahara wa kiasi gani kwa sababu ninakuhamisha kutoka mahali pengine”

    “Ni vyema uniambie wewe, utanilipa kiasi gani?”

    “Ingawa hukuniweka wazi kuhusu mshahara wako wa sasa, mimi nitakulipa mara tatu ya mshahara unaopata”

    “Sawa.”

    “Je uko tayari?”

    “Niko tayari. Unanihitaji kwa lini?”

    “Hata kwa kesho”

    “Kwa kesho haitawezekana. Subiri nimalize mwezi huu nipate mshahara wangu”

    “Samehe huo mshahara. Nitakulipa mimi. Kesho nitakupa shilingi laki moja uandike barua ya kuacha kazi. Keshokutwa uanze kwangu”

    “Kama ni hivyo sawa. Ukinipa laki moja nitaandika barua ya kuacha kazi na kesho kutwa ninaanza kwako”

    “Barua iandike leo, kesho unakwenda nayo”

    “Na hiyo laki moja…?”

    “Pia naweza kukupa leo. Lakini itabidi twende nyumbani kwangu, uione hiyo nyumba na pia nikupatie hizo pesa”

    “Sawa, twende tu”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Msichana akaligeuza gari na kuweka gea ya nyuma na kuelekea upande wa Raskazoni.

    “Unaonaje maisha?” akaniuliza baada ya kimya kifupi.

    “Tunaendeshana nayo hivyo hivyo”

    “Lakini wewe huna mke wala watoto, una nafuu si kama wengineo”

    “Hakuna nafuu yoyote, maisha ni magumu dadangu”

    “Kwa mshahara nitakaokupa, natumaini maisha utayamudu vizuri”

    “Sisi binaadamu kila upatavyo zaidi ndivyo mahitaji yanavyoongezeka zaidi”

    Nilikuwa kiti cha mbele mara akaweka gea ya tatu huku akiniangalia kwa jicho la mahaba ila moyo wangu nao ukawa na fadhaa.

    “Ni kweli Alfred, lakini unakuwa umepiga hatua ya kimaisha kuliko ulivyo sasa”

    Tulifika nyumbani kwake Raskazoni. Niliiona nyumba yake iliyokuwa kando ya bahari. Lilikuwa jumba la kifahari la horofa moja tena lilikuwa jipya.

    “Ndiyo hii nyumba yako?” nikamuuliza huku nikidhihirisha wazi mshangao.

    “Ndiyo hii, ngoja tuingie ndani”

    Geti la nyumba lilifunguka lenyewe kutokana na rimot iliyokuwa mbele ya gari. Msichana akaliingiza gari ndani. Gari hilo lilipoingia geti hilo likajifunga tena.

    Msichana huyo alisimamisha gari hilo mbele ya mlango wa nyumba.

    “Tushuke!” akaniambia huku akifungua mlango na kuitoa ile funguo ya gari na kushuka.

    Na mimi nikashuka.

    Msichana alitoa funguo na kufungua mlango wa nyumba.

    “Karibu ndani Alfred” akaniambia huku akitangulia kuingia ndani na mimi nikamfuata nyuma.

    Ni vyema nikiri kuwa katika maisha yangu tangu nizaliwe sijawahi kuingia ndani ya jumba zuri kama lile.

    Nilijikuta nimeganda pale kwenye mlango nikiangalia humo ndani jinsi mlivyokuwa mnapendeza na kujaa vyombo vya thamani. Niliona kama vile nikiingia, viatu vyangu vitachafua.

    “Mbona umesita kwenye malango?” Msichana akaniuliza alipoona nimesimama kwenye mlango.



    “Ngoja nivue viatu”

    “Hapana. Ingia tu na viatu vyako. Mbona mimi sikuvua?”

    Nikaingia lakini nilitembea kwa kunyata huku shingo yangu ikizunguka kama feni kuangalia huku na huku. Kila kitu nilichokiona nilikishangaa.

    “Karibu ukae” Msichana akniambia huku na yeye akiketi kwenye

    sofa.

    “Asante”

    Nikakaa kwenye sofa mojawapo.

    “Alfred naona umeshangaa sana” Sauti ya yule msichana ilinishitua.

    Badala yake nilitoa kicheko cha uongo kwani ni kweli nilikuwa nimeshangaa.

    Msichana naye akacheka na kuniambia.

    “Hapa ndio kwangu. Karibu sana”

    “Mbona kuko kimya. Unaishi na nani?”

    “Ninaishi peke yangu, ndio maana nilitaka mlinzi”

    Kauli ya yule msichana ilinishangaza zaidi.

    “Unaishi peke yako jumba lote hili?”

    “Ndiyo”

    “Unapokwenda sehemu, nyumba inabaki tupu?”

    “Ndiyo sababu nilihitaji mlinzi”

    “Na si kwa usiku tu, hata kwa mchana anahitajika mlinzi” nikamwambia.

    “Wewe utaweza kulinda usiku na mchana?”

    “Tunaweza kuwa walinzi wawili, mmoja wa usiku mwingine wa mchana”

    Nilipomwambia hivyo msichana huyo alitikisa kichwa.

    “Mimi ninahitaji mlinzi mmoja tu” akaniambia.

    “Kwa kweli itakuwa vigumu mlinzi mmoja kulinda usiku na mchana”

    “Basi utalinda usiku kama tulivyokubaliana. Kwa mchana sina wasiwasi sana na halafu mimi mwenyewe ninakuwepo nyumbani muda mwingi. Ngoja nikupatie zile pesa”

    Msichana huyo akanyanyuka na kuingia ndani. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa ameshika kitita cha noti nyekundu. Akanifuata pale nilipoketi. Na mimi nikanyanyuka.

    “Hizi hapa shilingi laki moja” akaniambia huku akinipa zile pesa.

    Nikazipokea na kuzitia mfukoni bila kuzihesabu.

    “Sasa twende nikakuoneshe maeneo ya hii nyumba”

    Msichana huyo akatoka, na mimi nikamfuata. Alinizungusha pande zote za ile nyumba, tukaishia kwenye banda lililokuwa kando ya geti.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hili ndilo banda la mlinzi. Utakuwa unakaa humu” Msichana huyo akaniambia.

    “Sawa”

    “Hebu tuingie ndani ulione vizuri”

    Tukaingia ndani ya lile banda. Kulikuwa na meza iliyokuwa na simu pamoja na kiti.

    “Hii simu unaweza kunipigia mimi kama utakuwa na dharura yoyote” akaniambia.

    “Sawa”

    “Ninachokusisitiza ni kuwa usilale usiku hasa kuanzia saa tisa hadi saa kumi na moja alfajiri. Wezi hupenda kuja katika muda huo kwa sababu watu wanakuwa wamekolewa na usingizi. Umenielewa?”

    “Nimekuelewa”

    “Na mara kwa mara uwe unazunguka kwenye maeneo ya nyumba niliyokuonesha, wezi wanaweza kuruka ukuta bila wewe kujua”

    “Ni kweli. Mara kwa mara nitakuwa nazunguka”

    “Ninayo tochi ya mawe sita, nitakupa pamoja na sime. Wakati mwingine taa huzimika, itakusaidia kumulika kwenye kiza”

    “Sawasawa”

    “Sasa tutoke nikurudishe nyumbani”

    Tukatoka kwenye lile banda. Msichana huyo alifunga mlango wa nyumba yake. Tukajipakia kwenye gari lake na kutoka. Hakukuwa na haja ya kushuka kufungua geti au kulifunga kwani geti hilo lilifunguka na kujifunga lenyewe kwa rimoti iliyokuwa mbele ya gari.

    Wakati tunaendelea na safari, yule msichana akaniuliza.

    “Unaishi wapi?”

    “Ninaishi Makorora”

    “Mna nyumba yenu pale?”

    “Ni chumba cha kupangisha”

    Baada ya hapo tulibaki kimya mpaka tulipoingia eneo la Makorora.

    “Unaishi mtaa gani?” akaniuliza.

    “Ninaishi nyumba ya tatu kutoka hospitali ya Makorora”

    Tulipofika hospitali ya Makorora nilimuonesha nyumba niliyokuwa ninaishi, akanipeleka hadi barazani.

    “Asante kwa msaada wako” nikamshukuru wakati nafungua mlango ili nitoke kwenye gari.

    “Asante na wewe kwa kunikubalia uwe mlinzi wangu”

    “Usiwe na wasiwasi, leo natarajia kuandika ile barua ya kuacha kazi. Kesho nitaipeleka ofisini”

    “Sasa niambie nikupitie kesho saa ngapi ili unipe uhakika kuwa unakuja kuanza kazi kwangu?”

    “Nipitie saa kumi na moja jioni”

    Saa kumi na moja jioni!. Kwanini isiwe mchana? Muda ulioutaja ni wa kujiandaa kuja kuanza kazi”

    “Na ndio muda huo ninaotaka uje ili tuondoke pamoja”

    “Kama mwenyewe unataka hivyo sawa, nitakuja hiyo saa kumi na moja”

    Nikashuka kwenye gari.

    “Ushinde salama” akaniambia wakati anaondoka.

    Jioni ile nilishughulika kuandika ile barua ya kuacha kazi, nikaitia kwenye bahasha na kusubiri asubuhi niiwasilishe ofisini kwetu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatua ile ya kupata mwajiri mpya ambaye ameniahidi kuwa ataniongezea mshahara, kwa kweli kilinifariji. Niliwaza kwamba endapo nitapata mshahara wa kutosha, nitanunua fanicha za chumbani mwangu na kuondoa zile zilizokuwemo ambazo zilikuwa zimepitwa na wakati na zilikwa zimechakaa.

    Niliendelea kujiambia baada ya kununua fanicha zingine ikiwemo tv na deki yake, nitatafuta msichana wa kumuoa ili nifungue ukurasa mpya wa maisha yangu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog