Search This Blog

NILIOA JINI NA KUZAA NAE - 5

 





    Simulizi : Nilioa Jini Na Kuzaa Nae

    Sehemu Ya Tano (5)



    ILIPOISHIA

    Saa kumi na moja jioni!. Kwanini isiwe mchana? Muda ulioutaja ni wa kujiandaa kuja kuanza kazi”

    “Na ndio muda huo ninaotaka uje ili tuondoke pamoja”

    “Kama mwenyewe unataka hivyo sawa, nitakuja hiyo saa kumi na moja”

    Nikashuka kwenye gari.

    “Ushinde salama” akaniambia wakati anaondoka.

    Jioni ile nilishughulika kuandika ile barua ya kuacha kazi, nikaitia kwenye bahasha na kusubiri asubuhi niiwasilishe ofisini kwetu.

    Hatua ile ya kupata mwajiri mpya ambaye ameniahidi kuwa ataniongezea mshahara, kwa kweli kilinifariji. Niliwaza kwamba endapo nitapata mshahara wa kutosha, nitanunua fanicha za chumbani mwangu na kuondoa zile zilizokuwemo ambazo zilikuwa zimepitwa na wakati na zilikuwa zimechakaa.

    Niliendelea kujiambia baada ya kununua fanicha zingine ikiwemo tv na deki yake, nitatafuta msichana mzuri wa kumuoa ili nifungue ukurasa mpya wa maisha yangu.

    SASA ENDELEA

    Asubuhi kulipokucha nilienda kazini bila kuvaa sare yangu. Nilipofika nilitoa ile barua kwa bosi wangu. Akaifungua na kuisoma mbele yangu.

    Alipomaliza kuisoma alishangaa na kuniangalia.

    “Umeamua kuacha kazi?” akaniuliza.

    “Ndiyo” nikamjibu.

    “Kwanini umeamua kuacha kazi ghafla, kuna tatizo lolote?”

    “Hakuna tatizo lolote. Kaka yangu ameniita Dar es Salaam. Anataka nikaishi kule. Atanitafutia kazi mahali pengine” nikamdanganya..

    “Sawa, lakini kwa sheria za kikazi itabidi usamehe mshahara wako”

    “Ninajua”

    “Sawa. Tunakutakia kila la heri huko Dar es Salaam unakokwenda”

    “Asante bosi wangu”

    Nikaondoka pale ofisini na kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani niligundua tatizo moja kwamba nisingeweza kuzitumia tena zile sare za kampuni niliyoacha kazi na hivyo ingebidi yule msichana aninunulie sare zingine atakazopenda nivae..

    Ilipofika saa kumi na moja jioni nikawa nimeketi barazani mwa nyumba niliyokuwa naishi kumsubiri mwajiri wangu mpya.

    Muda wa saa kumi na moja na robo hivi, niliiona gari yake ikitokea. Punde tu ikasimama kando ya baraza ya nyumba yetu. Nikanyanyuka na kuifuata. Moja kwa moja nilifungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia.

    “Habari za tangu jana?” Msichana huyo akawahi kunisalimia huku akitabasamu kwa haiba ya kipekee kabisa.

    “Nzuri, sijui zako?” nikamjibu.

    “Mimi mzima. Vipi?”

    “Ndiyo umekuja kunichukua?” nikamuuliza.

    “Kwani umeshaacha kazi kule kwa mwanzo?”

    “Tayari nimeshaacha. Nilikuwa nakusubiri wewe tu”

    “Asante sana. Sasa tunaweza kwenda?”

    “Ndiyo, isipokuwa…”

    “Isipokuwa nini tena Alfred?”

    “Ni suala la sare za kazi. Siwezi kutumia sare ya kampuni ya zamani”

    “Oh sawa. Nitakununulia”

    Msichana alitia gea na kuiondoa gari.

    “Sikuchukua chakula cha jioni wala chupa ya chai”. Nikamwambia wakati gari ikichanganya mwendo.

    “Usijali. Nitakupatia kila kitu”.

    Baada ya hapo tukawa kimya hadi tulipofika nyumbani kwake. Aliingiza gari ndani ya geti akaisimamisha karibu na banda la mlinzi.

    “Sasa shuka uingie kwenye banda lako” akaniambia.

    Wakati nafungua mlango aliniuliza.

    “Umekula mchana?”

    “Nimekula lakini nitahitaji chakula cha usiku”

    “Hakuna tatizo”

    Nikafungua mlango na kushuka, nikaingia kwenye lile banda. Msichana aliingiza gari kwenye banda la gari. Akashuka na kufungua nyumba yake.

    Aliingia ndani na baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika jaketi, sime na tochi. Akaingia katika lile banda na kunipa vile vitu.

    “Hili jaketi utavaa usiku na hii sime pamoja na hii tochi utatumia kwa ulinzi”

    “Asante sana”

    Nilivipokea na kuviweka juu ya meza.

    “Labda kuna kitu utahitaji?”

    “Kwa sasa sihitaji kitu”

    “Kama utakuwa na tatizo lolote nipigie simu”

    Akaniandikia namba yake kwenye karatasi na kuniwekea juu ya meza kisha akatoka.

    Alipotoka nililijaribu lile jaketi na kuona lilikuwa sawa. Nikashika ile sime na kuiangalia kisha nikairudisha juu ya meza. Nikaichukua ile tochi na kujaribu kuiwasha. Ilipowaka niliizima nikaiweka juu ya meza.

    Baada ya kuridhika kuwa kila kila kitu kiko sawa nilikaa kwenye kiti. Muda si muda yule msichana aliingia tena akiwa ameshika kiredio kilichokuwa kimewashwa.

    Akakiweka juu ya meza na kuniambia.

    “Redio hii na ya kukuchangamsha wakati wa usiku”

    “Loh!. Nashukuru sana, nitasikiliza taarifa za habari na miziki”

    “Basi nipo ndani” akaniambia na kutoka.

    Nilikaa ndani ya lile banda hadi giza lilipoingia niliwasha taa kisha nikatoka kwenye ua na kuamza kurandaranda huku na huko.

    Ilipofika saa mbili usiku kuna msichana alitoka mle ndani akiwa ameshika chano cha chakula. Hakuwa yule mwajiri wangu. Akaingia kwenye lile banda na kukiweka kile chano juu ya meza kisha akatoka.

    “Nimekuwekea chakula juu ya meza” akaniambia na kuingia ndani.

    Kilichonishangaza ni kuwa mwajiri wangu aliniambia kuwa alikuwa anaishi peke yake mle ndani. Yule msichana mwingine alitokea wapi?

    Wakati nataka kuingia ndani ya lile banda nilisikia simu inaita. Nikaingia haraka na kwenda kuipokea



    “Hellow…!”

    “Ndiyo Alfred. Nimemtuma mtumishi akuletee chakula” Ilikuwa sauti ya yule msichana aliyeniajiri kazi.

    “Nimekiona. Asante sana” Na mimi nikamjibu kwenye simu.

    “Sawa. Endelea kula”

    Akakata simu. Nilikitupia macho chakula hicho. Ilikuwa pilau ya kuku na bilauli ya juisi. Pembeni mwa sahani kuliwekwa ndizi mbivu moja pamoja na chungwa.

    Yule mtumishi alirudi tena, safari hii akiwa na jagi la maji na bakuli. Aliweka bakuli juu ya meza akaniambia.

    “Nikunawishe mkono”

    Nikakinga mikono yangu kwenye lile bakuli. Mtumishi huyo akanimiminia maji. Niliosha mikono yangu nikamwambia.

    “Basi”

    Akaliweka jagi juu ya meza na kutoka.

    Mtumishi alikwa mrembo na alikuwa ananukia manukato. Nilitamani angalau angekuwa mke wangu.

    Pilau ilikuwa tamu. Wakati ninakula nilijiambia fedha ndio kila kitu. Msichana mrembo kama yule ameajiriwa utumishi wa ndani kwa sababu ya fedha tu.

    Nilipomaliza kula, msichana huyo alirudi tena kuondoa vyombo.

    Mwajiri wangu akanipigia tena simu.

    “Umeshakula?” akaniuliza.

    “Nimekula, nimemaliza. Nashukuru, asante sana”

    “Umetosheka?”

    “Nimetosheka sana”

    “Sasa kuwa macho usiku huu”

    “Usiwe na wasiwasi. Nitakuwa macho”

    Simu ikakatwa.

    Usiku ule ulikuwa wa faraja kwangu kwa sababu kwa mara ya kwanza tangu nianze kazi ya ulinzi, nilifanya kazi katika mazingira ya kuridhisha.

    Kwanza ni kule kupata chakula cha jioni bure na bila usumbufu na pia kukaa ndani ya banda mahali ambapo sitateseka kwa baridi.

    Nilipochoka kukaa ndani ya lile banda nilitoka nikazunguka katika ua wa ile nyumba kujichangamsha kabla ya kurudi tena ndani ya banda hilo.

    Ilipofika saa tisa yule msichana alitoka nje akaingia ndani ya lile banda na kuzungumza na mimi hadi saa kumi na moja alfajiri aliporudi ndani.

    Mpaka kunakucha sikuona kama nilipata shida yoyote. Nilifanya kazi pale kwa wiki nzima na taratibu nilianza kupazoea.

    Baada ya wiki kumalizika, wiki iliyoanza niliendelea kwenda kazini kama kawaida.

    Kulikuwa na siku ambayo nilikuta nyumba imepambwa kuliko kawaida. Na mle ndani kulikuwa na shamrashamra. Sikuweza kujua mlikuwa na shughuli gani. Aliyenifungulia geti alikuwa mtumishi wa mle ndani. Nikamuuliza kulikuwa na nini. Akaniambia kulikuwa na sherehe.

    “Sherehe ya nini?” nilimuuliza.

    “Atakueleza dada mwenyewe”

    “Dada mwenyewe yuko wapi?”

    “Yuko ndani”

    Mtumishi huyo akaondoka na kurudi ndani. Nikakaa ndani ya lile banda hadi saa mbili usiku nilipoletewa chakula. Nilipomaliza kula mtumishi alikuja kuondoa vyombo.

    Nikaendelea kubaki ndani ya lile banda hadi saa nane usiku, yule mtumishi alipokuja tena, akaniambia.

    “Unaitwa ndani”

    Nilishituka. Sikujua nilikuwa naitiwa nini. Na mle ndani shamra shamra zilikuwa zikiendelea hadi muda huo.

    Nikamfuata yule msichana aliyekuja kuniita, nikaingia naye ndani. Nilikuta watu mbalimbali waliovalia maridadi wameketi wakinywa vinywaji na kushereheka.

    Msichana huyo alinichukua hadi kwenye chumba kimoja ambacho alinionesha bafu na kuniambia.

    “Unatakiwa uoge, ukimaliza unakuja hapa kwenye kabati”

    Alinifungulia kabati lililokuwa mle ndani ya kile chumba na kunionesha nguo zilizokuwemo ndani.

    “Utachagua suti utakayoipenda, utavaa na shati jeupe na viatu vyeupe. Halafu utagonga mlango, mimi nitaingia ili nikupeleke kwa dada”

    Kwanza nilisita, nikataka kumuuliza kulikoni lakini nikaona nitekeleze vile nilivyoagizwa.

    Nikaoga. Nilipomaliza nilichagua suti ya kijivu niliyoipenda. Nikaivaa pamoja na shati jeupe na viatu vyeupe.

    Nilipomaliza niligonga mlango. Hapo hapo yule mtumishi akaingia.





    “Umependeza. Sasa twende” akaniambia.

    Nikaenda naye katika chumba kingine ambacho kilikuwa kimepambwa. Nilimkuta yule msichana mwajiri wangu naye amepambwa. Alikuwa amekaa kwenye kitanda huku wasichana wanne wakiwa wamesimama karibu yake kama walinzi.

    Niliogopa hata kuingia mle chumbani lakini yule msichana mwajiri wangu aliponiona aliniambia.

    “Ingia”

    Nikaingia. Akanitazama kwa makini kisha akaniambia.

    “Alfred umependeza leo!”

    “Asante, hata na wewe umependeza”

    “Sogea karibu yangu’

    Nikamsogelea. Alikuwa ananukia uturi (manukato).

    “Inama nikuambie”

    Nikainama.

    Akaniambia kwenye sikio langu “ Samahani sikuwahi kukwambia, shughuli hii ni yako wewe. Nilitaka kukushitukizia”

    “Mh!. Unasema shughuili hii ni yangu mimi?” nikamuuliza baada ya kutomuelewa.

    “Ndiyo, ni yako wewe. Leo tutafunga ndoa usiku huu na hutakuwa mlinzi wangu tena bali utakuwa bwana wa nyumba hii”

    “Umesema utafunga ndoa na mimi usiku huu?” nilimuuliza kwa mshituko uliochanganyika na kiwewe.

    “Ndiyo, ni kwa sababu nilikupenda tangu nilipokuona ukilinda pale dukani. Nikapanga uwe mume wangu”

    Wakati akiniambia hivyo alikuwa anatabasamu huku akiniangalia kwa jicho la huba.

    Nilishindwa kujizuia na mimi nikamwambia.

    “Kama ni kweli unayoniambia nitafufurahi kama utakuwa mke wangu”

    “Sasa ninamuita sheikh nimpe idhini atuozeshe”

    Msichana akamtuma yule mtumishi amuite sheikh. Sheikh alipofika msichana huyo akamwambia.

    “Nimekuita kukupa idhini uniozeshe na Alfred na tangu sasa atakuwa anaitwa Abubakar, jina ambalo nimemchagulia mimi”

    “Nataka na idhini ya mzazi wako wa kiume” Sheikh akamwambia.

    “Atakupa idhini huko huko”

    “Twende bwana!” Yule sheikh akaniambia.

    Nikatoka na yule sheikh nikiwa siamini yale yaliyokuwa yanatokea.

    Tulikwenda sebuleni ambako watu mbalimbali walikuwa wamekaa. Katikati ya sebule palitandikwa zulia dogo na palikuwa na watu wanne waliokuwa wamekaa hapo. Wote wanne walikuwa wamevaa kanzu nyeupe na vilemba kama waarabu.

    Sheikh niliyekuwa nimefuatana naye alinishika mkono na kuniambia.

    “Kaa hapa”

    Alinionesha pale walipokuwa wamekaa watu wanne. Nikakaa na yeye akakaa mbele yangu. Mtu aliyekuwa ameketi upande wake wa kulia alikuwa mzee aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe.

    Nikasikia akimwambia.

    “Wewe ndiye walii (baba) wa bi harusi. Nataka idhini yako ili nimuozeshe binti yako kwa Abubakar”

    Ninakupa idhini” Yule mzee akamwambia kwa sauti ndogo.

    Sheikh huyo akanishika mkono na kunifungisha ndoa ambayo sikuitarajia.

    Baada ya kufungishwa ndoa nilipelekwa katika chumba alichokuwemo yule msichana. Nikaambiwa nimpe mkono, nikampa mkono.

    “Karibu kwenye nyumba yako mume wangu” Msichana huyo akaniambia kwa furaha na kwa sauti ya unyenyekevu iliyotoka kwenye moyo wake. Hapo vigelegele na chereko vilisikika nyumba nzima.

    Mke wangu huyo akaniambia nikae kwenye kitanda karibu yake. Nikakaa. Baadaye kidogo tuliletewa vyakula na vinywaji. Mke wangu akanikaribisha, tukala pamoja. Hata hivyo mimi sikula sana kutokana na kihoro kilichonipata ingawa chakula kilikuwa kitamu.

    Baada ya kumaliza kula tuliachwa peke yetu. Msichana huyo akaniambia.

    “Sasa tulale mume wangu. Hapa ni kwako”

    Tukalala hadi asubuhi.

    Wakati huo wa asubuhi nyumba ilikuwa kimya. Sikuona mtu yeyote humo ndani zaidi ya mke wangu na watumishi wake wawili.

    Wakati tunakunywa chai nilimuuliza.

    “Wale watu wa jana usiku wamekwenda wapi?”

    “Walienda zao usiku ule ule. Walikuja kwa ajili ya harusi yetu”

    Tuliporudi chumbani msichana huyo akaniambia.

    “Mimi napenda sana kusimulia hadithi. Ngoja nikusimulie hadithi moja”

    Nikamwamia “Nisimulie”

    “Zamani kulikuwa na msichana mmoja mrembo ambaye alimpenda sana kijana mmoja ambaye naye alikuwa mzuri. Msichana huyo alitamani sana kijana huyo awe mume wake lakini ikawa vigumu kwa wawili hao kuoana”

    “Kwanini ilikuwa vigumu, huyo kijana hakumpenda huyo msichana?” nikamuuliza.

    “Lahasha mume wangu. Ilikuwa vigumu kuoana kwao kwa sababu yule kijana alikuwa binaadamu lakini yule msichana alitoka katika kizazi cha kijini”

    “Enhe!. Halafu ikawaje?” nikamuuliza baada ya kuona hadithi yake inafanana na kile kisa kilichonotokea mimi.

    “Yule kijana alipogundua yule msichana ni jini alianza kumkimbia lakini msichana huyo hakukata tamaa, aliendelelea kumfuatilia kijana huyo na kumrai na kumueleza jinsi alivyokuwa anampenda”

    Hadithi ile ilianza kunishangaza. Nikawa makini kuisikiliza ili nijue mwisho wake.





    “Basi kuna siku msichana yule wa kijini alimchukua kijana yule kwa hila na kwenda kumuonesha mama yake huko kwao ujinini, Mama yake alipomuona kijana huyo alimuuliza kama amekubali kuoana na binti yake. Kijana kwa sababu ya hofu yake alijibu hakukubali. Basi mama mtu alikasirika na akamkataza mwanawe aache kumfuta kijana yule kwa sababu hamtaki”

    Wakati mke wangu anaendelea kunisimulia hadithi ile nilikuwa nimemtumbulia macho kumsikliza. Akaendelea.

    “Basi yule msichana kwa vile alikuwa amempenda sana kijana yule alifanya mpango mwingine ambao ulifanikisha dhamiri yake ya kuoana na msichana yule. Na hadithi yangu imeishia hapo”

    “Kumbe baadaye walikuja kuoana?” nikamuuliza.

    “Ndiyo, walioana”

    “Huyo kijana hakuwa na uoga tena na huyo jini?”

    “Hakuwa na uoga tena”

    “Hicho kisa kinafanana na kisa kilichonitokea mimi, lakini mimi sikuoana naye”

    “Alah! Wewe pia kilikutokea kisa kama hicho?”

    “Kilinitokea”

    “Sasa kwanini hamkuoana?”

    “Nisingeweza kuishi na jini”

    “Mbona umeoana naye?”

    “Hapana , sikuoana naye. Alinipeleka kwao nikamkataa, sikumuona tena”

    Mke wangu huyo akatabasamu.

    “Mmeoana bwana na ndiye mke uliyenaye na unampenda sana”

    “Mimi sina mke mwingine zaidi yako’

    “Basi huyo jini nitakuwa mimi!”

    Aliponiambia hivyo nilishituka.

    “Mke wangu acha utani, wewe siye yule. Kwanza hamlingani kabisa”

    “Unajuaje kama nimejibadili ili usinitambue?”

    “Unataka uniambie wewe ni Banuna mwana wa Ziraili?”

    “Naam!”

    “Siamini mpaka nikuone katika sura ileile”

    “Nihakikishie kama utaendelea kunipenda iwapo nitakuwa kwenye sura yangu”

    “Nakuhakikishia kuwa nitaendelea kukupenda kwa maana tumeshaoana”

    “Asante. Sasa fumba macho yako”

    Nikafumba macho yangu. Muda ule ule akaniambia.

    “Fumbua sasa”

    Nikafumbua macho na kumtazama. Nilishituka sana nilipoona sura yake ilikuwa imebadilika na kuwa ya Banuna.!

    “Kumbe kweli wewe ni Banuna mwana wa Ziraili!” nikamwambia.

    “Umeamini sasa?” akaniuliza huku akitabasamu.

    Alipoona nimeshikwa na mshangao, alinikumbatia haraka na kunibana kwenye kifua chake. Nilisikia faraja sana.

    “Nakupenda mume wangu, niambie kama na wewe unanipenda” akaniambia.

    Nikajikuta nikimwambia.

    “Na mimi nakupenda pia”

    “Asante mume wangu. Nakuahidi kuwa nitakuenzi na nitakupa utajiri usioutarajia maishani mwako”

    “Nitafurahi”

    Naam. Miaka sita sasa imepita tangu tukio hilo la ajabu linitokee. Nataka niwambie kuwa nimekuwa tajiri kama msichana huyo wa kijini alivyoniahidi.

    Si tajiri wa pesa tu bali tajiri wa miradi. Nina miradi mbali mbali ya kiuchumi iliyonifanya niishimike mjini. Unaponiona huwezi kunidhania kuwa miaka sita iliyopita nilikuwa korokoroni niliyekuwa nikilinda maghala.

    Tena nikiwa muajiriwa wa makampuni ya ulinzi ambaye mshahara wangu haukufika hata shilingi laki moja!

    Raslimali iliyokuwamo chumbani mwangu wakati huo kilikuwa kitanda cha bei rahisi na kimeza kilichochochakaa.

    Nashukuru kwamba Banuna alikuwa ameniwezesha!

    Mke wangu huyo nilikuwa ninaendelea kuishi naye hadi ninaposimulia kisa hiki. Ananipenda na mimi nampenda.

    Kwa kweli tunapendana mapenzi ya dhati na ya kweli. Amenionesha mahaba ya kijini ambayo sijapata kuyaona maishani mwangu.

    Katika kipindi nilichoishi naye Banuna ameshapata ujauzito mara mbili lakini watoto alikwenda kuwazalia kwao. Mtoto wetu wa kwanza alikuwa mwanamke wa pili alikuwa mwanaume.

    Mara moja moja anawaleta pale nyumbani niwaone wanangu halafu anawarudisha kwao. Ameniambia watoto hao hatuwezi kuishi nao pale nyumbani wakiwa wadogo kwa sababu ni majini.

    Licha ya unyenyekevu alionao Banuna, ni mkali na ana wivu wa kupindukia.



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog