Search This Blog

NILIOLEWA NA MGANGA KWA TAMAA YA CHEO KAZINI - 3

 







    Simulizi : Niliolewa Na Mganga Kwa Tamaa Ya Cheo Kazini

    Sehemu Ya Tatu (3)





    ILIPOISHIA:

    “Rose ilianza lini na leo iwe ya pili kutoka nje usiku peke yako?”

    “Dada nilizidiwa nikaona nikikuamsha nitakusumbua nawe mgonjwa.”

    “Na yule mzee ulikuwa unatoka naye wapi?”

    “Mzee gani?”

    ”Rose, si muda mfupi umempiga busu shavuni.”

    SASA ENDELEA...



    “Mmh, sasa umbeya huo, nilikwenda kuomba dawa ya tumbo baada ya tumbo nami kuanza kunikata.”



    “Mmh, haya.”

    “Wasiwasi wako tu,” Rose alijitetea.

    “Wa nini! Kipi cha ajabu?”

    “Huenda unadhani ni mpenzi wangu!”

    “Walaaa, mimi siko huko.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Najua utafikiria vibaya, mimi kizee kile nikipeleke wapi?”

    “Rose, mbona hivyo maneno yanakutoka kama umepoteza nauli?”

    “Najua lazima utafikiria vibaya labda nina uhusiano wa kimapenzi na kizee kile, nilikuwa nakitania japo kweli kilinitongoza lakini Efrazia si kitafia kifuani kwangu.”



    “Asife kwa wake zake watatu afe kwa wewe mtu mmoja, muda umekwenda tulale mengine kesho.”

    “Lakini lazima ujue sina uhusiano na yule babu.”

    “Hata ukiwanao kipi cha ajabu, ana wanawake wadogo kuliko wewe hata akiwa mpenzi wako si makubaliano yenu. Tuachane na hayo tulale.”



    “Mmh, haya.”

    Maskini Rose aliona aibu alijua ni siri lakini nilikuwa nayajua mengi juu ya uhusiano wake na mzee Sionjwi bila ya yeye kujua akaona ni siri. Niliamini kwa muda wa kuwepo pale huenda mchezo ule wameucheza sana kwa siri. Nilivuta shuka huku nikiomba kukuche haraka ili nirudi nyumbani.

    ****

    Siku ya pili niliamka saa moja asubuhi, hali yangu ilikuwa nzuri japo tumbo liliuma kwa mbali lakini mzee Sionjwi alinihakikishia kuwa dawa atakayonipa ya kunywa itamaliza matatizo yote. Baada ya maandalizi na kupewa dawa ya mizizi ya kuchemsha kisha kuiweka katika chupa ya kunywa kila siku mara mbili asubuhi na jioni.



    Majira ya saa mbili na nusu tuliianza safari na kuingia Dar majira ya saa tano na nusu, kutokana na uchovu tulipofika kwangu wote tulioga hata bila kula tulijitupa kitandani. Mmh, tulilala mpaka saa kumi na mbili jioni. Sote tuliamka njaa ilikuwa ikiuma kama kidonda kwa vile jirani kulikuwa na muuza chipsi tulinunua chipsi kuku juisi ya boksi ilikuwa ndani tulikula na kunywa kisha jioni nilimsindikiza Rose hadi kwake.



    Rose alikuwa anakaa na wazazi wake ila alikuwa na chumba chake hata maamuzi yake alijiamulia, baada ya kumuacha nilirudi nyumbani.



    Siku iliyofuata ilikuwa Jumatatu, nilikwenda kazini kama kawaida Rose naye alikuwepo kama kawaida yake, kwa vile tulikuwa watu wa karibu muda wa chai tulikuwa pamoja hata chakula cha mchana. Kwa kweli urafiki wetu ulikuwa mkubwa sana.



    Kwa upande wa kazi kila kitu kilikwenda vizuri hata uhusiano na bwana wangu ulikuwa wa kawaida japo haikuwa kama zamani. Ukweli alinitoka moyoni nilijikuta mtu ninayependa kufanya mapenzi na wanaume wenye nguvu kama mzee Sionjwi.



    Nilijikuta nakuwa na mzee Sam kwa ajili ya pesa zake lakini mapenzi alikuwa akinitia kichefuchefu, kuna kipindi ilifika hata kutopenda aniguse kwa vile alinipaka shombo.



    Siyo siri lazima niseme ukweli nililikumbuka penzi la mwisho na mzee Sionjwi chini ya mbuyu lilikuwa tamu na zito ambalo tangu nivunje ungo sikuwahi kushikwa vile na mwanaume. Nilijikuta nikipata wazo la kijinga la kumfuata mzee Sionjwi angalau nikae naye kwangu kwa wiki ili anikate kiu ya mapenzi.



    Lakini nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi kama kawaida, usiku nilijikuta nahamu ya kuota ndoto za kufanya mapenzi na mzee Sionjwi lakini wapi mpaka kunakucha sikumuota mzee Sionjwi wala kivuli chake.

    Kitu kingine kilichonishtua ni kupotea kwa Rose ambaye walisema aliaga anakwenda kwa rafiki yake lakini hakurudi, wapo waliosema Rose mtu mzima hawezi kupotea huenda alikwenda kwa mwanaume.



    Kwa upande wangu nilimlaumu Rose kuacha kazi kwa ajili ya mwanaume kibaya hata kwao hakufahamika. Niliona heri bwana aliyemuoa kuliko kujikurupukia leo na kesho anakuacha njia panda unakosa pa kushika.

    ****

    Ilikuwa wiki mwezi Rose haonekani kwa kweli niliingiwa ukiwa kutoweka kwa shoga yangu Rose ambaye ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu kuliko wote pale kazini. Kwa ukaribu wangu nilimgeuza kama ndugu yangu wa damu, kwa kweli nilipooza sana pale kazini kwani sikuwa na mtu wa kumpa siri zangu.



    Kila kitu kina mwisho hata maumivu yana mwisho huwezi kuteseka milele, nilijikuta hali ya upweke naizoea hata kufikia hatua ya kumsahau shoga yangu Rose.



    Siku zilikatika huku kazi nayo ikienda vizuri mshahara nao uliongezeka na marupurupu juu, baada ya miezi sita tangu Rose apotee nilipata tetesi kuwa kuna nafasi ya kwenda kusoma nje na ukirudi unakuwa mhasibu mkuu wa kampuni kwa kanda zote mahesabu yote yanapitia kwangu.



    Nafasi ile ilitolewa baada ya aliyekuwa mhasibu mkuu wa kanda kukaribia kustaafu. Japo ilionekana kama mimi nina nafasi kubwa ya kwenda lakini kulikuwa na kaka mmoja aliyetoka chuoni ambaye ilionesha wazi huenda angeichukua nafasi ile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wazo la haraka lilikuwa kukimbilia kwa mzee Sionjwi sikuogopa kuniingilia kimwili kwangu hakikuwa kitu cha kunitisha sana. Cha muhimu kilikuwa kuipata nafasi ile kwa gharama yoyote.



    Siku ya Alhamisi niliaga kazini kuwa Ijumaa nitakuwa na udhuru, nilikubaliwa kwa vile nafasi ile nilimuachia yule kaka ambaye alikuwa ndo ameanza kazi, mambo mengi nilimsaidia alionekana ni mstaarabu tena mwenye heshima kitu kilichonifanya nimpende.





    Siku ya Ijumaa asubuhi nilifunga safari mpaka kijijini kwa mzee Sionjwi, nilifika mapema sana, mpaka saa mbili na nusu nilikuwa nimesimamisha gari mbele ya nyumba ya mzee Sionjwi. Kama ilivyo kawaida yangu niliwanunulia mahitaji muhimu kwa maeneo yale. Sukari, chumvi, mchele sabuni na mafuta.



    Nilipokelewa kama Malkia kila mtu alinifurahia mimi, nilipokuwa nateremka kwenye gari macho yangu yaliona kitu ambacho kwa kweli kilinishitua sana. Sikuamini macho yangu mara moja kuwa ninachokiona ndicho chenyewe. Sikuamini niliacha gari bila kufunga na kusogea karibu ili nipate uhakika ni kweli au naota au nafananisha.

    “Efrazia unashangaa nini, karibu shoga.”



    “Mmm! Siamini ni wewe Rose?”

    “Ndiyo mimi shoga nimejaa tele kama pishi la mchele.”

    Mmh, ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni, Rose alikuwa amejifunga shuka nyeupe iliyoishia juu ya matiti mgongo ulikuwa nje, chini alikuwa amevaa ndala za matairi mkono wa kushoto alikuwa amejifunga hirizi ndogo nyeusi. Yote tisa kumi alikuwa na ujauzito mkubwa tumbo lilimwelemea, nilibakia mdomo wazi.

    “Efrazia, unashangaa nini mpenzi?” aliniuliza akiwa anatafuna embe bichi.

    “Rose lini tena huku?”



    “Tangu nilipopotea kazini,” alinijibu bila wasiwasi.

    “Na ujauzito huu wa nani?”

    “Ukiona ujauzito ujue una baba yake, mbona maswali kama umesikia nimepewa na bwana wako?”

    “Rose siamini”



    “Usiamini nini au ulisikia mimi mgumba?”

    “Siyo hivyo kukukuta huku.”

    “Rose, usitake kuyajua ya watu, fuata yaliyokuleta ya kwako si uliitoa tuache tuzae.”

    “Unataka kuniambia ujauzito huu ni wa mzee Sionjwi?”

    “Kwani mwanamke yule?”

    “Sina maana hiyo najua ni mwanaume tena shababi lakini bado hujaniweka wazi ujauzito huu ni wake?”

    “Eeh.”



    “Mmh.”

    “Unaguna nini?”

    “Aah, basi.”

    “Basi karibu mi ndo mwenyeji wako.”

    Nilipewa mkeka wakati huo chai na viazi ilikuwa tayari na imetengwa kwenye mkeka wake wote wanne wa mzee Sionjwi walijumuika akiwemo shoga yangu kipenzi Rose. Sikutaka kukataa chai ile tulijumuika wote na kuinywa chai ile.



    Baada ya chai nilikaa chini ya mti wakati huo mzee Sionjwi hakuwepo alikuwa amedamka alfajiri kwenda kuchimba dawa, nilikaa na Rose hata kumuuliza maswali niliogopa kutokana na majibu yake. Nilitulia kwenye mkeka nikiwa na mawazo mengi kichwani nikijiuliza nini kilichomfanya Rose kuacha kazi na kuja kwa mzee Sionjwi na kuolewa na kuwa mke wa nne.



    Kwa kweli jibu lilikuwa gumu kupatikana na kuuliza niliogopa kuudhiana na shoga yangu, niliamua kukaa kimya mpaka nitakapoondoka na hata mjini sitamwambia mtu niliyoyaona kwa mzee Sionjwi hata wazazi na ndugu wa Rose niliapa sitawaambia kitu chochote kuhusiana na Rose niliogopa kumuudhi mzee Sionjwi na kukosa tiba ya matatizo yangu.



    Ajabu Rose hakuonesha mabadiliko yoyote zaidi ya kunenepa na kupendeza nilijiuliza ameridhika na nini, maisha kule kijijini hayakuwa mazuri sana vitu vingi hawakupata zaidi ya kula visivyokuwa na mafuta wala kiwango cha juu japo katika sayansi chakula walichokula kilikuwa bora kuliko tulivyokuwa tukila mjini vingi vilipoteza ubora.



    Mzee Sionjwi alirudi saa nane akiwa na kapu lake lililokuwa limejaa dawa, alipokuwa akija kwa mbali nilijikuta nikimuona kiumbe mpya kwangu kama mtu niliyewahi kusikia historia yake na kuwa na hamu ya kumuona. Kila nilivyomwangalia sikummaliza.



    Umri wa yule mzee kwa hesabu za haraka alikuwa anakimbilia miaka 75, ukimuangalia unaweza kusema hana nguvu lakini akikushika hasa katika mchezo wa kikubwa utamjua yule mzee ni nani hachoki pia ni mjuzi wa kukufanya ufurahie tendo lile hata usitake ateremke haraka.

    Nilimwangalia toka alipotokea mpaka alipofika karibu yangu, alipofika tulipokuwa tumekaa nilimsikia akisema.

    “Aah, kumbe tuna ugeni?”



    “Ndiyo babu shikamoo,” nilimjibu.

    “Marahaba, karibu.”

    “Asante babu.”

    “Vipi umefika zamani?”

    “Muda tangu asubuhi.”



    “Karibu, si unajua tena kazi zetu kila kukicha tunatengeneza dawa basi lazima tudamke alfajiri kuingia porini kutafuta dawa. Lakini wenyeji wako si umewakuta?”

    “Nashukuru babu wamenipokea vizuri.”

    “Rose kaniletee maji ya kunywa.”



    Rose alinyanyua na tumbo lake huku akiuma meno kufuata maji ya kunywa ya mumewe mzee Sionjwi.

    “Rose mtoto mmoja umechoka hivyo wakifika kumi je?”

    Maneno ya mzee Sionjwi yalinistaajabisha kuhusu kumzalisha watoto kumi Rose, nilijiuliza hao watoto kumi wa Rose na wengine sijui watakuwa wangapi na nini hatima ya maisha yao. Niliamini babu yule pamoja na umri mkubwa bado aliweza kufikisha watoto hata 30 lakini nini urithi wa watoto kama mzee Sionjwi atakufa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pia nilimuonea huruma Rose mtu mwenye elimu yake japo hakufikia elimu yangu lakini elimu ya kidato cha sita ingeweza kumpa mwanga wa kuchagua maisha ya kuishi na siyo kuolewa na mganga asiye na kitu chochote ambacho kingeweza kumsaidia maishani pindi mumewe atakapofariki.



    Kuna kitu ambacho niliamini Rose alisikiliza ladha ya mapenzi aliyopewa na mzee Sionjwi, kama nilivyosema ukikutana na yule mzee kimwili kama huna moyo mgumu kama umeolewa lazima utaisaliti ndoa yako. Hata sikujua babu alikuwa na nini cha ziada kuliko wanaume wengine.



    Lakini japo mzee anajua kukata kiu ya mapenzi lakini bado ulitakiwa mtu kujiuliza ukifuatacho faida na hasara ipi imezidi upande mmoja. Sikutaka kuhoji sana nililiacha kama nilivyolikuta japo nilijawa na mawazo mengi akilini mwangu.



    Kila nilivyokuwa nikimuangalia Rose jinsi Mungu alivyomuumba na uamuzi wa kuolewa na kikongwe kama mzee Sionjwi sikupata jibu. Niliamua bora niachane naye na kuendelea na kilichonipeleka pale. Baada ya muda Rose alirudi na kombe kubwa la maji nakumbuka nililileta mimi baada ya kutumwa na mzee Sionjwi nimnunulie.



    Mmh, makubwa Rose alipofika mbele ya mzee Sionjwi alipiga magoti na kumpa maji kwa heshima zote. Mzee Sionjwi alichukua maji ya kunywa huku Rose akiwa bado amepiga magoti.

    Baada ya kunywa Rose alipokea kikombe huku mzee Sionjwi sijui nimwite dume la mbwa au jogoo la mtaa kila kuku jike wake, akisema..



    “Asante mpenzi.”



    “Asante kwa kushukuru mpenzi.”



    Rose alinyanyuka na kuelekea ndani kurudisha kikombe, baada ya kunywa maji alimtuma bi mkubwa kwenda kumwekea maji ya kuoga. Aliniacha na baadhi ya wakeze na kwenda kuoga, Rose alirudi na kukaa huku akishika kiuno na kukunja uso.



    “Vipi tena shoga?” nilimuuliza.



    “Mmh, kiuno.”



    “Kimefanya nini?”



    ”Toka jana na kila nikimweleza mzee Sionjwi anasema nisubiri zamu yangu ndiyo anipe tiba.”



    “Kwani zamu yako lini?” Nilijitia umbea kuuliza yasiyonihusu.



    “Leo usiku.”



    “Sasa tiba mpaka ifike zamu yako?”



    “Utamuweza mzee yule ngono itamuua anapenda kama chakula.”



    Nilitamani kucheka kusikia hata wakeze wanajua kuwa bwana wao anapenda sana ngono.



    “Si mtamuua ninyi wote wanne tena wote mpo kamili.”



    “Kile kizee wanga tu hakina lolote.”



    “Heheheheheheheeee….Rose utanivunja mbavu miye,” nilijikuta nacheka bila kupenda.



    “Si utani Efrazia kama siyo wanga ni nini? Mtu kikongwe kama yule kuweza kugawa dozi kwetu sote tena si ya kitoto na bado yupo fiti.”



    Nilijikuta nikiangua tena kicheko  mpaka machozi yakanitoka, niliamini ule ulikuwa muda muafaka wa kumuuliza ilikuwaje akaja kule kijijini na kuacha kazi ambayo ilimwongezea kipato ambacho kilisaidia familia yake.



    “Rose mpenzi naomba nikuuliza kama nitakuudhi naomba unisamehe.”



    “Mbona unanitisha ni swali gani hilo?”



    “Ilikuwaje ukaja huku na kuacha kazi?”



    ”Efrazia hilo liache tu kama una swali lingine uliza?”



    “Sina zaidi ya hilo.”



    “Basi kama huna lingine tuendelee na mengine.”



    “Rose njoo upate dawa ya kiuno mara moja nakuona unalalamika sana,” mzee Sionjwi  alisema baada ya kutoka bafuni kuoga.



    “Shoga baadaye, ila ukiondoka usiache kuniaga.”



    “Kwani dawa gani tena hiyo ya kukulaza?”



    “Mmh, we mkubwa sasa si kila kitu uambiwe, hana dawa nyingine mzee anapenda kama chakula.”



    “Na hilo tumbo hiyo dawa atakupaje.”



    “Si ndo nakwambia yule mzee mwanga, baadaye mengine niachie mwenyewe usije ng’ang’ania bure usirudi mjini.”



    Nilimuacha Rose akapate dawa ya kiuno japo nilikisia lakini sikuwa na uhakika na dawa ya kiuno huenda sivyo nilivyodhani. Kwa kweli ilichukua muda toka saa tisa mpaka saa kumi na mbili bado walikuwa hawajatoka. Nilijua lazima nilale na huenda kazi ikafanyika usiku.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wasiwasi uliniingia huenda nami nikahamia kijijini kwa mzee Sionjwi, kama aliweza kunitembelea usingizini na kunipatia ujauzito lazima atataka kunibakiza nami kijijini. Mmh, woga uliniingia na kutamani niondoke bila kuaga. Lakini bado nisingefanya kitu kama Rose alirudi mjini na kumkuta kwa mzee Sionjwi hata mimi sikuwa na ujanja.



    Lakini kuna kitu kilinipa moyo kutokana na pesa na misaada mingi niliyokuwa nampa lazima atauona umuhimu wangu wa kuniacha niendelee na kazi. Vilevile hata kama ningekimbia bado nafasi ya kwenda nje kusoma ningeikosa na muda ulikuwa umebaki mchache sana kuteua jina la mtu wa kwenda kusoma nje, nilisikia kuna mtoto wa mkubwa ndiyo kaandaliwa.



    Nilijikuta nikipoteza woga wote na kuwa tayari kwa lolote ili mradi nafasi ile niipate.



    Nikiwa katikati ya mazungumzo na wake wa mzee Sionjwi ambao hawakuonekana kuathiriwa na maisha ya kijijini. Kila mmoja aliyafurahia maisha yake tena waliishi kwa adabu kubwa kama wanawake wote wangekuwa kama wake wa mzee Sionjwi basi nyumba nyingi zisingevunjika.



    Lakini kama wanaume wote wangekuwa na tamaa kama mzee Sionjwi watu wangezikwa kila kukicha kwa ukimwi kwa tabia yake ya tamaa ya wanawake kibaya hata kinga kwake hakutaka kuitumia.



    Muda wote nilivyowaangalia watoto wake na uwezo wa baba yao nilichanganyikiwa kabisa kwa kuamini watoto wale kupata elimu itakuwa kazi. Niliamini kabisa mzee Sionjwi hata darasa moja hakupitia, kama angekuwa na elimu hata ya darasa la nne basi angejua jinsi ya kupanga uzazi au kuwa na wanawake wengi na uwezo wake ni mdogo.



    Nikiwa katikati ya dimbwi la mawazo nilimuona Rose kwa mbali akija huku akijikongoja kama mzee na kuja nilipokuwa nimekaa huku tumbo likimtangulia mbele. Alipofika nilipokuwa nimekaa alisema huku akikishika kiuno chake huku tumbo akilitanguliza kwa mbele.



    “Vipi mwenzangu kiuno kimepona au ndio kakizidisha?” Nilimuuliza baada ya kujifikilia kukaa huku ameuma meno.



    “Dada kimepona.”



    “Sasa mbona upo hivyo?”



    “Dada weee kikongwe yule anapenda sifa hiyo dawa hajui kama nina tumbo hapa nipo hoi.”



    “Mmmh, pole.”



    “Dada usinipe pole, nipe hongera.”





    “Hongera ya nini?”



    “Tiba niliyopata si ya kitoto maumivu yote ya kiuno yamepotea.”

    “Mmh, dawa yenyewe ilikuwa ya kuchua au kuchanja maana mmechukua muda mwingi?” Nilitia umbeya.

    “Dada we mkubwa, ukiona ndevu ujue kuna mdomo.”

    “Mmh, haya nimekuelewa.”



    “Dada mzee yule kabarikiwa kanyimwa utajiri lakini nguvu za kumtoa pweza pangoni weee acha tu.”

    Tukiwa katikati ya mazungumzo niliitwa kwenda kuonana na mzee Sionjwi aliyekuwa pembeni amekaa kwenye kigoda chake na pembeni kulikuwa na mkeka mdogo, muda nao ulikuwa umekwenda kiza kilianza kuingia, nilikwenda na kukaa pembeni ya mzee Sionjwi pamoja na sekeseke na Rose hakuonekana kutetereka pamoja na kudamka asubuhi na kushinda porini na kurudi muda umekwenda. Bado ameweza kugawa dozi ya kiuno kwa Rose huku akionekana bado imara kama chuma cha pua.



    “Mmh, mjukuu karibu sana,” alisema kwa sauti ya chini.

    “Asante babu, za siku?”

    “Aah, Mungu analeta neema zake.”

    “Hata mimi naona.”



    Mzee Sionjwi hakusema kitu alitabasamu tu kisha alibadili mada kwani niliamini alikosa jibu hasa baada ya kumkuta shoga yangu kipenzi kwake tena kamjaza tumbo.

    “Mm’hu, lete habari una jipya au ni yaleyale?”

    “Kuna jipya babu.”

    “Ehe, lete habari.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilimweleza kisa na mkasa ulionifanya nifunge safari ya ghafla kwenda kumuona kule kijijini. Baada ya kunisikiliza alitulia kwa muda kama anasoma kitu kisha alisema kwa sauti ya chini.

    “Kwa hiyo nafasi hiyo unaitaka?”

    “Ndiyo maana yake babu?”

    “Mbona nafasi umepata.”

    “Kweli babu?”



    Japo nilimwamini mzee Sionjwi niliona kama jambo lenyewe alichukulia kiwepesi sana tofauti na uzito uliokuwepo kwenye nafasi ile baada ya mkubwa mmoja kumwandaa ndugu yake na kwa vile wao ndiyo wanaoteua mtu wa kwenda.



    Pamoja na sifa zilizotajwa kuwa nazo, bado upendeleo ungechukua nafasi kubwa.

    “Kwani wasiwasi wako nini?” Mzee Sionjwi aliniuliza.

    “Mazingira yamejaa utata mtupu.”



    “Ni wasiwasi wako tu, nafasi hiyo utaipata kinachotakiwa ni kunipa majina ya wote watakaokuwepo kwenye bodi ya uchaguzi niwakaange ili jina lako likae akilini mwao na ndilo litapita mbona kazi ya kitoto hiyo.”

    “Babu unasema kweli?”

    “Lipi nililokudanganya?”

    “Hakuna babu.”



    “Basi amini nafasi hiyo utaipata.”

    “Babu nikiipata kabla ya kuondoka nitakuletea zawadi kubwa ambayo hutaamini.”

    “Kama zawadi ipo bora unipe kabisa Ulaya umekwenda mjukuu wangu.”

    ”Siamini,” nilijikuta nikikumbatiana na mzee Sionjwi kwa furaha.



    Tulikumbatiana kwa muda huku nikihisi kitu fulani mapigo ya mzee Sionjwi yalikuwa juu kitu kilichonishtua. Baada ya kuachiana nilimsikia akihema kama mtu aliyeutua mzigo mzito.

    “Vipi babu?” Nilimuuliza.



    “Aah, kawaida nafasi umepata usihofu mjukuu wangu,” alisema kwa sauti ya chini.

    “Kwa hiyo naweza kuondoka leo?”

    “Ruksa ila hakikisha unawahi kuleta majina hayo.”

    “Babu kesho jioni utaniona, nikitoka kazini breki ya kwanza hapa.”

    “Basi nisikucheleweshe nikuache uwahi.”



    Niliagana na babu nikiwa na furaha ya ajabu, kutokana na furaha niliyokuwa nayo nilimpa babu Sionjwi laki tatu. Nilimuaga Rose ambaye aliniuliza narudi lini, nilimjulisha alinituma baadhi ya vitu alivyokuwa akivitaka. Muda ulikuwa umekwenda ilikuwa inakaribia saa mbili usiku niliingia kwenye gari langu na kurudi mjini nikiwa na furaha ya ajabu kama nafasi tayari nimeipata





    Njiani nilikuwa nikiwaza mengi bila kupata jibu la Rose kwenda kijijini kwa mzee Sionjwi na kuacha kazi, sikuona cha maana alichokifuata kule zaidi ya tabu ya maisha kuzaa watoto wasio na malezi bora bila kuwa na uhakika wa maisha ya mbeleni.



    Kila nilipoangalia maisha ya mzee Sionjwi na wakeze ya kubahatisha na shoga yangu Rose naye kwenda kulekule. Sikuamini kabisa kama kwenda kwa mzee Sionjwi haikuwa akili yake bali ya kiganga.



    Nilivyojiangalia mimi na Rose nilikuwa namzidi kwa kiasi kikubwa kwa uzuri, nilijikuta nikiwa na wasiwasi kama ameweza kumshika akili shoga yangu niliamini kwa tamaa yake angeweza kunishika akili na mimi na kuingia kijijini na kuongeza idadi ya wanawake zake.



    Lakini niliyapuuza na kuamini huenda ni tamaa ya Rose kwani nilishuhudia vitendo vya ngono muda mwingi. Nilikumbuka siku ya kwanza niliwafuma wakifanya mapenzi kwenye majani, kwa hilo liliniondoa hofu kwa kuamini huenda walikubaliana wenyewe.



    Hilo lilinifanya niondoe hofu moyoni mwangu, kwa kuamini mzee Sionjwi na Rose walikuwa wakijuana huenda penzi tamu la mzee Sionjwi ndilo lililomchanganya akili na kulifuata porini.

    Nilifika Dar majira ya saa saba usiku, ajabu nilikuwa mtu mwenye furaha kutokana na kuhakikishiwa kuipata nafasi ile. Sikuwa na wasiwasi nilijua majina ya bodi ya kuchagua mtu atakayetakiwa kusafiri kwenda kusoma nje nitayapata kupitia shoga yangu Safia katibu muhtasi wa mkurugenzi ambaye alikuwa akinieleza kila kilichokuwa kikiendelea kuhusu mchakato ule.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipofika nyumbani nilijilaza ili kuisubiri siku ya pili kwa hamu kubwa, asubuhi ilipofika nilijiandaa kama kawaida na kuelekea ofisini. Nilifika ofisini kwa kuwahi kidogo na kuingia ofisini kwangu. Japo niliwahi ofisini lakini akili yangu ilikuwa katika kuyajua majina ya bodi ya uteuzi wa jina la mtu atakayekwenda nje kusoma.



    Katika majina yote yaliyopendekezwa mimi nilikuwa nina sifa zote lakini kutokana na tabia za ndugunaizesheni niliingiwa wasiwasi wa mkuu mmoja kumteua ndugu yake. Kutokana na kuifahamu vizuri kazi ya mzee Sionjwi niliamini kabisa kazi ile haikuwa ngumu kwake hasa baada ya kumuondoa kigogo wa uchawi Mbwana.



    Nilijikuta nikipingana na wazo la kumpigia simu shoga yangu Safia katibu muhtasi wa mkurugenzi ili aniambie kina nani wapo kwenye bodi ile japokuwa kulikuwa na watu niliwajua lakini ilikuwa lazima wajumbe wachache watoke kwenye matawi yetu hasa baada ya malalamiko kuonesha makao makuu hujiamulia wenyewe na viongozi wa matawi kukosa fursa ya wao nao kumpendekeza wanayemuona anafaa kwenda.



    Pamoja na upinzani wa kijana aliyeonekana anatishia kazi yangu kutokana na kuwa na kivuli cha mkubwa bado niliamini uwezo wa mzee Sionjwi ulikuwa mkubwa sana mimi kuipata nafasi ile. Wakati nikiamini mbaya wangu ni yule kijana lakini nilipata taarifa nyingine kuwa kuna msichana mmoja anatoka katika moja ya tawi letu ana elimu kama yangu japokuwa mimi nilimzidi kidogo lakini alikuwa mpenzi wa meneja wa matawi ambaye ni swahiba wa mkurugenzi hivyo ushawishi wake kwenye bodi ulikuwa mkubwa ili mtu wake apite.



    Wazo la kumpigia simu Safia niliona kama ni kuvujisha kile ninachokihitaji, niliamini kumuona uso kwa macho kuna nafasi kubwa ya kumshawishi mtu kwa vile uso umeumbwa na aibu. Nilinyanyua simu kumpigia Safia kumjulia hali pia kujua ratiba zake.



    Baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili:

    “Halo Efrazia niambie shoga, leo umeniota nini?”

    “Kwa nini?”



    “Naona asubuhiasubuhi.”

    “Walaa, nilitaka kukujulia hali tu shoga yangu.”

    “Asante sijambo sijui wewe?”

    “Mi sijambo, kazi zinasemaje?”

    “Ziko poa.”



    “Eti kikao cha kupitisha majina kitakuwa lini?”

    “Ijumaa, tena kuna ubuyu (umbea) nataka kukuambia.”

    “Ubuyu! Unahusu nini?”

    “Tukutane lunch nikumwagie ubuyu.”

    “Poa.”



    Nilijikuta nikiwa na shauku ya kujua shoga yangu Safia ana ubuyu gani ambao ameupata toka bodi ya uteuzi wa jina la mtu atakayekwenda kusoma nje ili aje ashike madaraka makubwa baada ya aliyekuwa akishika wadhifa huo kuwa katika hatua za mwisho za kustaafu.



    Ilionesha kuna mizengwe mikubwa katika uteuzi tofauti na siku za nyuma.

    Hata hamu ya kazi iliniisha zaidi ya kutaka kuumung’unya niijue ladha yake kama ni chungu au tamu lakini kwa kauli ya Safia ilionesha kuna kitu hivyo ubuyu niliuona si mzuri kabisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini kwa upande mwingine haukunitia shaka sana kwa vile niliishajua kuna ushindani na ndiyo sababu iliyonifanya niende kwa mzee Sionjwi. Pia ile ilikuwa nafasi yangu nzuri ya kujua watu watakaokuwepo kwenye bodi ya uteuzi, hivyo ilikuwa rahisi kuyajua majina ya watu hao ili niwahi kuyapeleka kwa mhusika. Baada ya kuwaza yale nilijikuta nikipata nguvu za kufanya kazi. Muda wa chakula cha mchana ulipofika niliongozana na Safia kwa kutumia gari langu hadi kwenye hoteli iliyokuwa pembezoni kidogo na mji palipokuwa patulivu ili shoga animwagie ubuyu kwa uhuru mkubwa.



    Baada ya kufika kwenye hoteli iliyokuwa na hadhi ya nyota tatu tulitafuta meza ya pembezoni na kukaa kisha tuliagiza chakula. Baada ya chakula kuletwa tulianza kula huku nikiwa na shauku ya kuujua huo ubuyu. Lakini Safia alinieleza nipunguze pupa tule kwanza baada ya chakula tulikuwa na muda wa kutosha wa mazungumzo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog