Search This Blog

PETE YA MVUVI - 2

 







    Simulizi : Pete Ya Mvuvi

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila nilipojaribu kugonga mlango wa Mzee Magori sikupata majibu kwani ndani kwake kulikua na giza lililoashiria mlango ule umefungwa nay eye pamoja na familia yake walikua wameshalala, Hivyo nilizunguka uwani kwake ndipo kwa bahati nzuri baiskeli yake aliisahau nje. Niliichukua na kuanza safari ya kuelekea ziwani kumuangalia babu yangu, Mvua kubwa iliendelea kunyesha lakini sikukata tamaa niliendelea kuendesha baiskeli ile kwa haraka mno. Nikiwa njiani kwa bahati mbaya tairi ya mbele ya ile baiskeli ilipasuka, Hivyo ilinilazimu nishuke na kuikokota baiskeli huku nikitembea kwa haraka na moyo wangu ulijawa na wasi wasi mno kwani nilianza kuhisi mikosi hii inawezekana ikawa babu yangu amepatwa na matatizo. Mvua iliendelea kuongezeka kila baada ya dakika huku radi kali zikipiga na kufanya miti kuanguka, Nilizidi kuogopa sana kwani nilikua katikati ya pori ambalo ni lazima upite pindi uendapo ziwani na pori lile lilijulikana kwa kuwa na wanyama na viumbe wa ajabu ajabu pindi tu ifikapo usiku. Nikiwa natembea huku nikikokota baiskeli ghafla nilimkanyaga nyoka aliyekua na rangi nyekundu huku kichwa chake kikiwa na pembe mbili kama za mbuzi, Nyoka yule alinirukia kiunoni na alipojaribu kuningata tumboni nilimshika kichwa chake na kumtupa chini kisha niliitupa ile baiskeli na kuanza kukimbia, Nilipokua nikikimbia nilijiuliza sana ujasiri ule wa kumshika mnyama hatari kama yule niliutolea wapi!? Ila niliamini ni Mungu tu! aliniepusha na balaa lile. Pori lile lilikua ni kubwa sanaaa!! Hivyo juhudi zangu za kukimbia zilifika ukingoni kwani pumzi iliniishia huku pia miguu iliishiwa nguvu kwani nilikua nikikimbia kwenye matope na madimbwi makubwa ya maji huku nikitobolewa na miiba, Nilisimama kwa dakika chache nikiwa nafuta pumzi na kutafuta nguvu za kuendelea na safari ya ziwani, Nilisikia sauti za fisi na vishindo vyao na kwa mbali niliwaona fisi wawili wakiwa wananifata kimya kimya na waliponiona tu! walianza kunikimbiza. Nilianza kukimbia na uchovu ule huku nikiwa nikimuomba Mungu na kwa sauti nilisema, “Mungu weeeeee!!! Mungu!!!! Niokoe mimiiii!!!” nilitamka maneno yale huku nikiendelea kukimbia mara ghafla sikusikia sauti wala vishindo vya fisi wale hivyo nilisimama na nilipojaribu kukohoa nilikohoa damu nzito huku pua zangu nazo zilianza kutokwa na damu, Maskini!!! Hali yangu ilikua mbayaaa mnoo…Nilikumbuka msemo wa babu uliosema, “Mwanaume ni shujaa na kila apatapo majaribu basi hana budi kupambana kuyashinda” Hivyo msemo ule ulinipa nguvu ya kuendelea kutembea na baada ya muda wa dakika 10 nilifanikiwa kufika ziwani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilitazama huku na kule nikitafuta mtumbwi wa babu ila sikufanikiwa kuuona japo kwa mbali, Machozi yalianza kunitoka taratibu taratibu na kadri nilipokua nikiangalia ziwa lile bila kuona dalili yoyote ya babu yangu kurudi nilianza kulia kwa nguvu kwani nilihisi kuna kitu kibaya kimemtokea babu. Ghafla kuna kitu kiliugusa moyo wangu na nilinyamaza, nilikumbuka nimeacha mlango wa nyumba yetu wazi na huku ndani nilimuacha mdogo wangu Neema, Nilishtuka sana na kusema, “Mungu wangu kumbe nimeacha mlango wazi?” Niliogopa sana kwani kawaida ya kijijini kwetu pindi mvua kubwa inyeshapo huwa kuna wanyama na wadudu kama nyoka na nge huwa na tabia ya kuingia ndani ya nyumba za watu kutafuta joto. Nilizidi kuogopa kwani ni lazima nipite tena kati kati ya lile pori lakini kutokana na upendo wa dhati niliokua nao kwa mdogo wangu (Neema) nilijikaza kiume na nilifanikiwa kupita bila kufukuzwa na mnyama yeyote. Nilipofika karibu na nyumba yetu nilimuona nyoka mkubwaaa!!! Akiwa anatoka ndani ya nyumba yetu huku tumbo lake likiwa limejaa. Daaaah!!!! Niliishiwa nguvu kabisaaa!! Kwani nyoka yule alikua mkubwa sana na alitoka huku akionekana amekula kitu na nilihisi atakua amemmeza Neema, Nilimsubiri nyoka yule apotee kabisa na ndipo kwa haraka sana nilikimbilia ndani na moja kwa moja nilielekea chumbani nilipokua nimemuacha Neema. Kwa bahati nzuri nilimkuta neema akiwa ameamka huku akicheza cheza na shuka, Nilihema kwa nguvu na kusema, “Ooooooh!! Asante Mungu”. Nyoka yule alimeza kiroba kilichokua na mabaki ya samaki na nyama ya mbuzi. Nilirudishia mlango wa nyumba yetu na kisha nilipanda kitandani kulala, Nikiwa ndotoni niliota ndoto mbaya sana kwani niliota nipo msituni nikizungukwa na watu waliokua na sura za wafu huku shangazi yangu aishio mjini akiwa na kisu kikali kilichotapakaa damu ya babu. Sikuweza kuendelea na ndoto ile kwani Neema alishtuka na kuanza kulia……



    na kwa uwelewa nilijua ana kiu cha maji, Hivyo nilitoka kitandani kumfatia maji na kumnywesha baada ya muda kidogo alilala. Baada ya kuota ile ndoto sikupata usingizi kabisa kwani nilianza kuitafakari ile ndoto huku nikitokwa jasho na mikono yangu kutetemeka, Nilizidi kuogopa na nilikua nikitamani asubuhi ifike mapema. Asubuhi ilifika na mlango wa nyumba yetu uligongwa kwa nguvu, Mimi nilikua bado usingizini ila kwa mbali sana nilisikia sauti za watu zikisema, "Joshuaaaa!!! Weweee!!! Amkaaaa!! Babu yako ana hali mbaya sanaaa!! Fungua mlango" Mhhhh!!! Niliposikia jina la babu yangu limetajwa nilishtuka mara moja na nilitoka nje kuona ni nini kiliendelea. Maskiniiii!!!! Nilimuona babu yangu akiwa amelazwa chini huku anatokwa na damu za pajani na kifuani huku sura yake ikijawa na uchungu kwa kuvumilia majeraha yale, Babu aliniambia,"Joshua baba naomba uniletee maji kwenye kikombe changu cha kahawa" Nilinyanyuka haraka na nilimletea maji, Babu alikunywa yale maji na yalipofika nusu kikombe aliniangalia kwa huruma na kisha alisema,"Mjukuu wangu kikombe hiki na maji haya nakukabidhi yawe baraka zangu kwako na mdogo wako, Pia nakuomba uzisimamie mali zangu vizuri ukiwemo mtumbwi wa kuvulia samaki na hili shamba lililopo hapa nyumbani, Babu yako sidaiwi chochote na mtu yeyote yule hivyo asije mtu akakudanganya, Joshua Mungu akusimamie, Kwaheri mjukuu wangu" Kabla hata sijaanza kumuuliza kwanini ananiambia maneno yote yale, Babu yangu alifumba macho huku pumzi yake ikikata, Maskini babu alifariki akiwa mikononi mwangu....Kifo cha babu yangu kilisababishwa na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya kungatwa na fisi alipokua akirejea nyumbani usiku ule ambao masaa machache kabla ya tukio lile nilienda kumtafuta eneo zima la pale ziwani lakini sikumuona. Kuchelewa kwa babu yangu kurudi nyumbani kulisababishwa na upepo mkali uliokua ziwani huku zile mvua zilizopiga kwa nguvu mno zilimfanya babu pamoja na rafiki zake kusubiri mpaka upepo na mvua ile kubwa ipungue, Na usiku huo walirudi wakiwa na furaha mno kwani walivua samaki wakubwa na wengi sana hivyo kwa furaha ile babu pamoja na rafiki zake walielekea moja kwa moja kilabuni japo kujipongeza na chupa kadhaa za pombe aina ya BALIMI, Babu yangu hakutaka kunywa pombe hivyo aliwaacha rafiki zake yeye alianza safari ya kurudi nyumbani, Kumbe alipokua kati kati ya lile pori alikua amebeba mfuko mkubwa uliojaa samaki huku alikua akiimba nyimbo zake kwa kupiga miruzi. Harufu ya samaki wale na mlio ule wa mruzi uliwakurupusha fisi na hivyo walitafuta harufu hiyo ipo wapi na walipomuona babu akiwa na mfuko mkubwa wa samaki,

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa nguvu walimshambulia babu na kumjeruhi sehemu kubwa sana mwilini mwake. Maagizo yake yote aliyoniachia marehemu babu nilianza kuyatimiza pale tu! tulipomaliza kumzika,lakini kwa kuwa nilikua mdogo kujua nini hatma zile mali zake niliona ni vizuri nimshirikishe Shangazi yangu kwani yeye ndiye aliyekua mtoto wa pekee aliyebaki kwa babu yangu. Nilimueleza Shangazi kila kitu nilichoambiwa na babu huku nilimpa zile karatasi ambazo sikujua maana yake ni nini?, Shangazi alishtuka sana kwani aliona jina langu kwenye kila karatasi zile ambazo ni hati za mali za marehemu babu yangu. Shangazi yangu kwa hasira alisema, “Niniiiiiii!!!!? Eboooo!!? Joshua? Yani wewe ndio mrithi wa mali za baba yangu? Thubutuuu!!! Labda mimi sio binti wa marehemu” Niliogopa sanaaa!! Kwani aliongea kwa hasira huku macho yake yalianza kubadilika na kuwa myekundu, Kwa uwoga ule niliondoka eneo lile na kukimbilia ndani kumuangalia mdogo wangu (Neema) asiyejua lolote lilokua linaendelea. Enzi za uhai wa babu yangu alipenda sana kunisihi nisije nikamuamini Shangazi yangu hata chembe lakini nilikua sina wa kumuomba msaada kwa mzigo ule mzito wa kusiamamia mali niliokua nimekabidhiwa na marehemu baba kwani umri wangu ulikua ni mdogo kuweza kuhimiri jukumu lile peke yangu……



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog