Search This Blog

MZIMU WA WAUFI - 5

 







    Simulizi : Mzimu Wa Waufi

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga shughuli za kila siku zilikua zikiendelea, pilikapilika za matabibu na wauguzi ziliendelea kama ilivyo ada, Hali ya ukimya ilitawala kidogo katika mabenchi maalum waliyokua wameketi baadhi ya wagonjwa waliokua wakisubiria huduma wakati mwili wa Marehemu Ngulinzila ukitolewa katika chumba maalum cha vipimo na kurejeshwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, Hakika maiti hazoeleki maana watu wote waliingiwa na ubaridi, bila shaka wangejua aina ya kifo cha huyo anaetolewa ndani humo wangezidi kuzizima kwa hofu na upweke wa nafsi. Wakati Zoezi hilo likiendelea nae Koplo Bangi alikua amewasili eneo husika akiwa ametinga koti jeusi la suti na suruali ya kaki vijana wa mjini wanaita Mchuzi juu, cha ajabu Koplo Bangi hakua akijishughulisha kabisa kuangalia machela maalum iliyokua umeubeba mwili wa Ngulizila bali macho yake yaliyokua yamejificha ndani ya miwani ya jua yalikua yakiangaliana kwa tahadhari ya hali ya juu na Jicho moja la kijana mmoja mtanashati aliekua amesimama huku akiiangalia machela ile kwa umakini wa hali ya juu, Jicho hilo lilikua ni la Hunudu



    Takribani dakika nzima macho mawili ya koplo Bangi yaliendelea kumtazama kijana huyu katili kutoka Waufi, tayari Koplo Bangi alianza kuhisi hali ya hatari eneo lile, alijaribu kuvuta kumbukumbu ya maelezo ya Masu kuhusu mtu mwenye ‘Chongo’ ambae ameukua akishirikiana na marehemu Ngulinzila katika kutaka kumuangamiza Masu. Wakati huo tayari kengere ya hatari ilikwishaanza kugonga ndani ya kichwa cha Hunudu baada ya kugundua kua alikua akiangaliwa sana na Afisa huyu wa jeshi la Polisi

    “Hunudu..” Koplo Bangi aliita kwa sauti ya utulivu na ya uhakika kwamba alikua habahatishi, Sauti ya Koplo Bangilana ilipenya sawia katika masikio ya Hunudu lakini akajikausha kama mtu ambae hakusikia chochote

    “Hunudu” Koplo Bangi aliita tena bila kuitikiwa na kijana huyu aliemkusudia, ndipo sasa akaamua kumsogelea na kushika Begani

    “We Kijana si ninakuita wewe?”

    “Nani? Mimi?” Hunudu alijibu kama mtu asiejua lolote kama kuna mtu alikua akimuita

    “Sasa kumbe naongea na nani hapa?”

    “Mbona Kibabe sana Mzee? Sikukusikia si unajua tena tunatembea na mawazo mengi, pengine ungeniita kwa jina langu ningesikia”

    “Nimekuita mara mbili nzima, Hunudu, Hunudu, uko kimya tu”

    “Hunudu? Mie siitwi Hunudu”

    “Acha maskhara kijana au ulitaka nikuite Hunudu wa WAUFI?...” Baada ya swali hilo la kichokonozi Jicho moja la hunudu lilianza kuzunguka kama saa mbovu, hakika Hunudu alihamanika dhahir, mdomo ukajaa maji kabla ya Koplo Bangi kuendelea …

    “..Pole kwa msiba wa mwenzenu, najua jinsi gani unavyoumia”

    “Oya mbona unanizingua mzee? Hebu endelea na Shughuli zako, me sio Hunudu wala sijafiwa na mtu yoyote hapa”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haha ha ha..” Koplo Bangi alicheka kwa dharau ya hali ya juu aliyokua akimuoneshea Hunudu kua amemjua vizuri kasha akaendelea “Hunuduuu, Shefa Mkuu kutoka katika Dini ya Waufi, haya niambie umekuja kumuuguza nani hapa hospitali kama sio kuhakikisha umauti uliomfika mwenzio? Mimi najua kupambana na wachawi mnaotumiwa na mizimu, leo nitakudhibiti” Hunudu akainuka kwa jazba na wahka wa hali ya juu sana huku akianza kuondoka eneo lile kabla kiganja kipana cha Koplo Bangi hakijatua juu ya paji la uso la Hunudu na kumuachia maumivu makali Hunudu hali iliyopelekea taharuki kubwa kwa baadhi ya wagonjwa na ndugu zao waliokua wameketi katika mabenchi,



    Masu hakukubali kudhalilika nae akarusha ngumi iliyotua katika kimpuma cha Koplo Bangi mpaka miwani ikaruka hewani na hapo sasa watu walishuhudia Sinema ya Bure kati ya miamba hii miwili, zilpigwa ngumi zenye viwango vya kimataifa, kila mmoja alionekana kupambana kwa kuzingatia kanuni sahihi za ngumi, Japo Hunudu alikua na Jicho bovu lakini alikua akizikwepa ngumi na mateke ya Koplo Bangi mithili ya Twiga anavyokwepesha shingo yake katikati ya miti mirefu awapo anakimbia, Baada ya kivumbi hicho cha dakika kama tano hivi Hunudu alikua akifuta damu iliyokua ikichuruzika kutoka katika tundu moja ya pua yake, Ngumi ya Koplo Bangi ilipenya na kutua alipokusudia..



    Mpambano wa vidume hawa ulipelekea hali ya Sintofahamu hospitalini hapo kiasi cha wagonjwa na wauguzi kuanza kuparaganyika hovyo kila mmoja akijaribu kuiokoa nafsi yake,

    “BANGIIIIIII” Sauti kali ilitokea nyuma ya ofisi ya Mganga mkuu, Koplo Bangi akageuka ndipo alipokutanisha macho na Ocd Nkeli , kabla jajafanya chochote huku nako kwa wepesi wa ajabu Hunudu alirukia upande wa pili ambako kuna Korido ndefu isiyokua na kona akakatiza ili akimbie, hapo hapo kitendo bila kuchelewa Koplo Bangi nae akaruka mpka upande wa pili cha ajabu alipofika katika Korido hiyo aliokatisha Hunudu alikuta ‘PATUPU’ Hunudu hakuonekana kabisa, alikua amepotea ghafla. Wakati Koplo Bangi akiendelea kustaajabu tukio lile kama la mazingaombwe tayari OCD Alikua ameshafika eneo lile huku Pistol yake ikiwa mkononi pia akiwa na kijana mwingine alievalia sare zake za jeshi la Polisi bila shaka ni dereva au mlinzi wa OCD

    “Kuna nini Koplo?” Alisaili Amos Nkeli

    “Afande dah, haya maajabu ya mwaka”

    “Kivipi?”

    “Amepotea ghafla tu kama maigizo”

    “Ni nani kwani Yule?”

    “Hunudu wa WAUFI”

    “HUNUDU??”

    “Ndio afande, huyo huyo niliemuelezea kwenye maelezo ya kesi ile ya kishirikina”

    “We umemjuaje?”

    “Ni story ndefu Afande”

    “Twende haraka Ofisini” OCD Amos Nkeli na Koplo Bangi wakaanza kuondoka huku kundi kubwa la watu likiwashangaa, nao hawakugeuka nyuma wakaanza kutoka kabisa katika eneo lile la hospitali, walipofika nje ya Hospital wakakuta gari ya OCD ikiwa inawasubiri na ndani yake kuna askari mwingine akiwa ameketi vizuri katika uskani , wakaingia wote na safari ya kurudi kituoni ikaanza

    *****



    Ndani ya Ofisi ya Amos Nkeli, mkuu wa kituo cha Polisi Shinyanga alikua ameketi juu ya kiti Koplo Bangi, wakati huo Afande Nkeli Akiwa amesimama huku amechegama kidogo katika nondo za dirisha, Saa ya ukutani ilikua ikionesha kua ilikua imetimu saa Kumi kamili Alasiri, Ocd Nkeli alikua amechanganyikiwa sana baada ya kusikiliza maelezo yote ya Koplo Bangi kuanzia alivyomtambua Hunudu kutokana na maelezo ya Masu, mpka alipoanza kumuhoji na kumgundua na hatimae mapambano yalipoanza, hakika Amos Nkeli alikua katika lindi la mawazo yasiyo na majibu

    “We ulienda pale Hospitalini kufanyaje?”

    “Afande ni wewe ndie ulienipigia simu kua tukutane pale, kuna taratibu za kufanya” Majibu ya Koplo Bangi yalizidi kumfanya sasa Ocd azidi kujiona kua amechanganyikiwa maana ni kwli yeye ndie aliemuagiza Koplo Bangi kua wakutane kule..

    “Ooh.. Ok Ok, nimekuelewa Koplo, sasa naungana na wewe kua Afande Ngulinzila alikua akijihusisha na mambo ya kishirikina,Maelezo ya kina Masu ni sawa kabisa hivyo sasa tunaweza kuwapa dhamana hawa watuhumiwa wote kasoro Masu tu…” Kabla hajamalizia kuongea akakohoa kidogo halafu akarudi akaketi katika kiti chake akawa anaangaliana na Koplo Bangi ndipo akaendelea “Masu kwakua bado anapaswa kutusaidia ukweli kuhusu Mzee Kishindo hivyo inabidi aendelea kua hapa, wakati huo huo pia Masu anakabiliwa na ile kesi kule Tabora mpaka mgonjwa atakapokua na hali nzuri ili tujue ukweli wa mambo”

    “Sawa afande..”

    “Wakati huo jitihada za kumtafuta Yule Mzee Kikoko nazo ni za muhimu sana maana nae anaonesha anajua mengi sana katika kesi hii,,” wakati Amos Nkeli anajaribu kumpa maelezo Mpelezi wa kesi hiyo Koplo Bangi mlango ukagongwa kasha akaingia askari mmoja wa kike, akapiga saluti kasha akatoa taarifa ya muhimu kwa Mkuu wake huyo

    “Afande kuna mzee hapo Nje amekuja amesema amepata taarifa kua anatafutwa na Jeshi la Polisi na pia watu wake wamekamatwa wako hapa, nadhani ndo Yule Mzee afande Bangi ulitupa taarifa zake”

    “Mzee gani huyo?” Koplo Bangi aliuliza kwa haraka na hamu ya kutaka kumjua

    “Amesema yeye ni Alwatan Kikoko” wakati askari huyu anamaliza tu kuweka nukta katika sentesi yake tayari Koplo Bangi alikua ameshainuka huku akienda huko kaunta kumuangalia mtu waliekua wakimuhitaji muda mrefu wakiamni amekimbia, sasa anaambiwa amejileta mwenyewe, amejisalimisha

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Koplo Bangi alipofika pale Kaunta alikutanisha macho na Mzee Kikoko, Mzee mtata, Mzee wa mjini, Mzee anaeonesha dalili zote za kujiamini ikiwa ni pamoja shari inayomtembea mwili mzima, Koplo Bangi hakua akimjua vizuri mzee huyu ila baada ya kumuona aliweza kuitambua sura ile kwa kua ni ya Mtu wa palepale Mkoani Shinyanga na pia alikua akifanana sana na mwanae ambae amekua akihojiwa na Koplo Bangilana mara kwa mara, Koplo akamuashiria Mzee Kikoko azunguke nyuma ya Kaunta hiyo nae Mzee Kikoko bila ajizi akiwa na Begi lake dogo la nguo lililoashiria kua alikua ndo amefika kutoka huko Dodoma alizunguka kule alipoitwa na kukutana na Koplo Bangi ambae alimchukua mpaka Ofisini kwa Ocd Nkeli, na baada ya kuketi katika kiti chake alianza kusailiwa mfululizo

    “Mzee Kikoko?” alianza kuongea Afande Nkeli

    “Naam ndo mimi, Alwatan Bin town”

    “Umekua wapi siku zote hizo wakati unatafutwa?”

    “Mie nilikua Dodoma, ambako nilikua nimelazwa hospitalini, ndipo nilipopata taarifa kua mnanitafuta na mmewakamata watu wangu kwa ajili yangu, haya sasa nimekuja mwenyewe na muwaachie huru”

    “Sio kwamba ulikua umekimbia?”

    “We unaona kuna sura ya kukimbia hapa?”

    “Ulipata wapi taarifa kua unatafutwa?”

    “Kutoka kwa vyanzo vyangu vya khabari, na mashushushu wangu wa kujitegemea” Kikoko alikua akijibu kama vile anaongea na wahuni tu wa mtaani, kitu ambacho kilizidi kumjaza hasira Afande Nkeli japo alijitahidi kuzificha hisia zake, baada ya afande Nkeli kutulia kwa muda muda akaendelea

    “Koplo”

    “Afande” Koplo Bangi aliitika kwa nidhamu

    “Wapigie simu wale wazee waliokuja kuwawekea dhamana hao watuhumiwa, waje wawadhamini ndugu zao, ila Masu asitoke na huyu Mzee muweke ndani mpaka atakapokua tayari ku..” kabla hajamalizioa sentesi yake akakatizwa na Mzee Kikoko

    “Hivi kosa langu ni nini hasa mbaona kama siwaelewi? Na kwanini mnapanga nani adhaminiwe na nani asidhaminiwe?”

    “Kaa kimya mzee” Bangilana alimjibu kwa mkato kabisa

    “Siwezi kukaa kimya, ni haki ya kila mtuhumiwa kujua kwanini anashikiliwa, na ni haki pia kwa mtuhumiwa kupewa dhamana, kijana haujui kazi yako inataka nini?” Kabla Koplo Bangi hajajibu lolote Afande Nkeli kadakia

    “Ulipigana na marehemu Kishindo siku moja kabla ya kifo chake hivyo una kila sababu za kujibu juu ya hilo”

    “Vipimo vya matabibu vinaonesha kua Kishindo alikufa kwa kupigwa na radi, kwahiyo unataka kuniambia kua zile ngumi zangu zilikua kama shoti ya umeme iliyojilimbikiza mwilini mwake ikaenda kugeuka radi huko porini?”

    *****



    Nje ya wodi ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya rufani ya Kitete mkoani Tabora kulikua na hali tete, baada ya wauguzi kugundua kua mmoja wa wagonwa waliokua mahututi ametoweka katika mazingira ya kutatanisha, Mgonjwa huyu Nyamizi Fundikira alikua katika uangalizi maalum kufuatia kesi liyopo kituoni inayohusisha tukio lake la kupigwa mapanga mpaka kupoteza fahamu huko Kipalapala na kufanya watuhumiwa wa tukio hilo ambao ni akina Ngaliba Kayoka na Babu yake Masu washikiliwe na Polisi kituoni hapo Tabora mpaka hali ya mgonjwa itakapoimarika kwa ajili ya kupata uhakika wa taarifa za maajabu kua aliempiga na mapanga alitoweka katika mazingira ya ajabu



    Wauguzi walikua wamechanganyikiwa vilivyo, hofu ilizidi kutamalaki hospitalini hapo, hakuna aliejua mahala alipokwenda mgonjwa Yule, kama ametekwa au Laa, kama amerudiwa na Fahamu akaamua kutoweka au Laa, ilikua ni hali ya fadhaa kubwa, tayari taarifa zilikua zimepelekwa Polisi na muda huo Sajent Malumbo alikua njiani akielekea hospitalini hapo kufuatilia ukweli wa kadhia hiyo

    *****

    Baada ya majibizano ya muda mrefu hatimae Koplo Bangi alimchukua Mzee Kikoko na kuandika maelezo yake yote na kisha ‘akamsweka’ ndani, baada ya zoezi hilo kukamilika ndipo akachukua simu na kuwapigia wazee waliokuja kuwadhamni Sheikh Jabu na Masu hapo mwanzo, wazee hao ni akina Mzee Kagomba ambao ni watu wa karibu sana na Mzee Kikoko. Na haikuchukua muda akina Kagomba wakawasili pale kituoni na walipokamilisha taratibu zote za dhamana walifanikiwa kuwatoa watu wawili tu Sheikh Jabu na Mama Almasi ambae ni mke mdogo wa Mzee Kikoko

    *****



    Kijiwe mashuhuri cha kahawa kinachomilikiwa na Mzee Kagomba swahiba wake wa karibu na Mzee Kikokoo Kilichopachikwa jina la BBC kutoka na kupatikana wa kila habari zote zinazojiri kila pembe ya mji siku hiyo kilikua kimesheheni wadau wengi zaidi kutoka na kupatikana kwa habari mpya kua Mzee Kikoko amejipeleka Kituoni na hatimae amewekwa ndani, pia katika Kijiwe hicho siku hiyo alikuwepo na Sheikh Jabu ambae baada ya kuachiwa na Polisi ilibidi aende akafike nyumbani kwa Mzee Kagomba ili kuepusha hali ya utata baina ya familia hizi mbili za Mzee Kikoko, alijua fika endapo ataenda kukaa kwa Mama Masu basi angetafsirika vibaya kwa Upande wa familia ya Mama almas ambae ni mke mdogo wa Mzee Kikoko halikadhalika kama angeenda kufikia kwa Mama Almasi, na kwakua msiba ulikua umekwisha kule nyumbani kwa marehemu Kasimba hivyo hakua na sababu ya kufikia kwa yeyote kati ya wake wa rafiki yake, akaamua kufikia nyumbani kwa Mzee Kagomba ambae ndie alieenda kumdhamini akishirikiana na mke wa Sheikh Jabu ambae yuko pale Shinyanga tangu kwa takribani siku tatu hivi akiwa na watoto wadogo wa Masu ambao walitakiwa kutolewa kafara na Mzimu wa Waufi, Judith ambae ni mke wa Masu muda wote huo alikua Arusha baada ya kuchukuliwa sasa na kaka yake mkubwa ambae anafanya kazi huko

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo mjadala mkubwa ulikua ni juu ya kadhia nzima inavyoendelea katika family ya Kikoko

    “Sasa ilikuaje bwana Kikoko akajitokeza?” aliuliza mzee Maguno

    “Yule bwana ni mwingi wa khabari, mie wakati ndo nimechukuliwa na askari siku ile ya kwanza nilipata Wasa’a wa kuteta nae kwa njia ya simu nimpa hadhari kua asijitokeze kabisa, Khaa ghafla leo namuona mwenzangu huyu hapa kituoni na sharubu zake”

    “Kweli alwatani Kikoko kidume, nasikia kamkaripia mpaka mkuu wa kituo”

    “Unajua hakuna mkate mgumu mbele ya chai, atalainika tu ile ni dola inataka heshima yake”

    “Naam, na Wahenga walisema ‘Akikalia kigoda mtii’, mwenye mamlaka ni mwenye mamlaka tu”

    “Hivi jamani mie naomba kuuliza, hivi pamoja na ukaribu wenu na Alwatan Kikoko mmeshindwa kabisa kumuweka chini wazee wenzie mkamkanya na kumpa ushauri ili sasa suala hili lifikie mwisho? Maana kwa hali nayoiona mimi ni kwamba Mzee Kikoko anazidisha tatizo kila kukicha” alidakia mazungumzo bwana mmoja mmoja hivi anaeonekana kua si kijana sana lakini pia si Mzee wa rika la kina Mzee Kagomba, swali lake liliwafanya wengi wakae kimya huku wakionesha kumuunga mkono kwa hoja yake aliyoiwasilisha kwa mtindo wa swali, ndipo Jabu sasa akaanza kutiririka

    “Binafsi leo niliongea kwa kirefu sana na Bwana Kikoko kuhusiana na kisanga hiki, hasa hasa tatizo lake la jazba na mihemko isiyokua na maana, na ameonesha kujutia kila nukta aliyoisababisha, na akaniagiza kua sasa ni wakati wa kumpeleka Masu huko Kipalapala akafanyiwe matambiko yao, na pia amekiri kua sasa ni wakati wake yeye kwenda kuwataka radhi ukweni kwake huko Tabora kwa kuyapuuza na kuyazembea matatizo haya, pia akanitaka nikishatoka ndani mule niende kwa Mama Masu nikajaribu kumsihi kua nae akawatake radhi huko Tabora ili tusafiane nia sote kwa pamoja..” Baada ya maelezo hayo Sheikh Jabu akachukua kikombe chake cha kahawa na kuanza kuinywa taratibu huku hadhira nzima ikiwa imetulia kuskiliza maelezo ya Sheikh Jabu, ndipo tena Mzee Kagomba alipoongeza neno

    “Kikoko anakuja kukunja ngumi ugomvi umekwisha”

    “Hapana, ni hatua kubwa sana hiyo kwa mtu mtata kama Kikoko kuonesha kukiri, unajua Dhambi ikikaririwa ni nusu ya marekebisho na kulijua tatizo ni nusu ya tiba” alidakia Mzee Kagomba

    “Nimesema hivyo kwa maana kua hayo maamuzi angeyakubali tangu mwanzo pengine saa hizi wala tusingekua tunajadili jambo hili hapa, lakini upuuzi wake kidogo tu umezua yote haya, ndio maana Wahenga wakasema ‘Cheche ya moto huteketeza msitu’ Sasa umesikia habari za Tabora huko?..”

    “Zipi tena?”

    “Si yule Mgonjwa aliekua akisubiriwa apone ili atoe ufumbuzi wa tukio la kupigwa kwake Panga ili walau akina Masu na babu yake wapate tumaini la kutoka..”

    “Amefariki?”

    “Bora angefariki tukajua moja, Mgonjwa ametoweka tu ghafla”

    “Afanaleik..” Wadau wote walipigwa na butwaa kusikia habari hizo mpya sasa, na mjada wa kina ukachukua nafasi, kila mtu alikua ameingiwa na hofu na kuamini kua sasa akina Masu wataozea ndani, lakini Sheikh jabu akawapa moyo kidogo

    “Unawajua Waswezi wewe? Wale ni hatari usije ukawachezea, bila shaka hilo tukio ni lao”

    “Sasa kwanini wamteke mgonjwa wao?, Itakua ni Waufi hao Baba, wababe wa vita” Kijana mmoja aliongea kwa sauti ya kebehi,

    “Sasa nimeongea na Mama Masu, ananiomba nimsaidie haraka iwezekanavyo ili kesho aende huko Kipalapala Tabora ili akaombe msamaha na pia akaombe hifadhi huko maana amesema zimebaki siku tatu ili afanyiwe kitu kibaya na hao Waufi, nimejaribu kumdodosa lakini hajaniambia siku tatu hizo ni za nini hasa! Na kitu hicho kibaya afanyiwe kivipi tena!, Basi ni utata juu ya utata”

    “Mama Masu anawajua vizuri waufi, ana makubaliano nao ambayo amaeyakiuka, na sasa watammaliza yeye pamoja na Masu kama hatokua makini” Mzee Maguno ambae ni mtaalam wa tafsiri za ndoto aljibu kwa kujiamini sana kitu ambacho kilisababisha Mzee Kagomba atie neno

    “Sasa wewe unazipata wapi hizi habari na kila siku unajifanyaga haujui chochote?”

    “Ajuaye mengi, hasemi mengi, lakini pindi mwaka ila kuna siku mtanikubalia maneno yangu”

    “Mnh haya, tuyaache hayo, sasa Sheikh Jabu utaenda na shemejiyo huko Tabora?”

    “Hapana, nimemwambia kua kesho inabidi nirudi mara moja Dar kuongea na bwana mmoja hivi mkubwa serikalini pengine atatusaidia katika kesi hii hivyo huenda yeye kesho kaondoka peke yake na kwenda Tabora, ila anaonekana kuchanganyikiwa sana hasa baada ya ile habari ya mpambano wa nguvu hopitalini kati ya afande Bangi na huyo Hunudu wa Waufi”

    “Hunudu wa Waufi?” Kagomba aliuliza kwa mshangao, bila shaka hakua na taarifa zozote za kilichojiri kule Hospitali. Ndipo sasa Sheikh Jabu akaanza kuwapa mkasa mzima ulivyo kuanzia kwa Marehemu afande Ngulinzila mpaka tukio hilo la hospitalini, kila mmoja alibaki mdomo wazi…

    *****



    USIKU WA MANANE

    Chini ya mti mkubwa kama ilivyo ada wafuasi wa Mzimu wa waufi walikua wamekusanyika kwa wingi, hoja zilikua nzito, walikua wakijibizana mpaka kutishia hali ya utengamano wao, inaonesha walikua katika malumbano makali sana

    “Mimi nataka kujua kwanza kwa nini yeye Mama Masu mwenyewe hajaja leo?” aliuliza mama mmoja wa makamo aliekua amejifunika shuka nyeusi ambapo akajibiwa na mkuu wao aliekua amekaa juu ya Kigoda cheusi

    “Mama Masu hatukumpa taarifa ya kuja hapa leo kwa sababu mjadala huu unamuhusu yeye hivyo hapaswi kuwepo hapa”

    “Sawa, sasa mimi nasema hivi hakuna muda wa kupoteza hapa, Mizimu imeshakasirika huko na tusipokua makini tutatahamaki tumeangamizwa wote hapa, cha msingi bado siku tatu tu za kupambana na Masu na bila shaka siku hizo hazitoshi tena kwetu hivyo huu ni muda muafaka wa kumtoa kafara Mama Masu mwenyewe ili tuendelee na mambo mengine” Mama yule alihitimisha hoja yake kabla ya kijana Hunudu kusimama na kuanza kutoa taarifa yakeCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “WAUFIIIIIII”

    “Mzimu wa watemi wa Bahari”

    “Jamani mimi sioni haja ya kulumbana hapa, muda umeshatutupa mkono, kwa sasa tunapambana na watu wengi sana, hata yule askari niliepambana nae kule hospitali leo ana nguvu za ziada, anasaidiwa na Waswezi bila ya kujijua mwenyewe ndomaana alikua akinizidia maarifa mara kwa mara, wakati huo mfahamu kua yule Mgonjwa sitaweza kumpata tena kirahisi maana Waswezi wameshamtorosha hivyo baada ya siku tatu hizi kukamilika inabidi sasa tummalize Mama Masu mwenyewe na kuachana na Waswezi mapema” Baada ya maelezo hayo ya Hunudu kukamilika aliketi chini, ndipo sasa mkuu wao anaefahamika kama Mtemi Kalovya aliposimama na kuanza kuongea

    “Najua inauma kumtoa mwenzetu lakini hayo ndio makubaliano yake na Waufi, hatuna jinsi, tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu lakini imeshindikana, inabidi maamuzi yapitike tu vinginevyo tutaangamizwa sote hapa, Mzimu umetuasa kwamba zikipita hizo siku zilizosalia bila ya kua tumemmaliza mmoja kati ya Masu au Mama yake basi sote hapa tutaangamizwa kila mmoja kwa namna yake, pia mkumbuke kwamba kitengo chetu cha mapambano kimepwaya baada ya Ngulinzila kuuawa hivyo amebaki Hunudu peke yake, nae akizidiwa tu basi tumekwisha, hivyo sasa mwenye mapenzi mema na Mama Masu kwa sasa anaweza kumsaidia tu kwa kumuangamiza Masu ila ikifika siku ya tatu kutokea leo endapo Masu akiwa bado salama nimetoa Ruhusa kwa Hunudu kufanya kazi yako ya kutuletea damu na kiwiliwili cha Mama Masu…, kama atatokea mwenye mawazo yoyote anifuate mapema nyumbani kwangu, kwa sasa hakuna jipya kila mmoja arudi nyumbani kwake” alihitimisha Mtemi Kalovya na kundi lote kutawanyika japo wengine wakiwa na kinyongo kwa mpango wa kummaliza Mama Masu

    *****

    Siku iliyofuata asubuhi na mapema zikiwa zimesalia siku mbili tu ili aangamizwe na Waufi kama kafara Mama Masu alikua ndani ya Basi akielekea Kipalapala mkoani Tabora akiwa na malengo makuu mawili, Mosi, ni kwenda kuwaangukia ama kuwataka radhi wazazi na familia ya mke mwenzie ambae ni Mama almasi kwa kitendo alichokifanya miaka mingi iliyopita cha kuuiba ujauzito wa mke mwenzie kishirikina, pia aliamini kua nguvu za mizimu ya Kasomangila chini ya Waswezi ni kubwa kuliko Waufi hivyo aliona kwa sasa muda wake wa kutolewa kafara umeshasogea hivyo ni bora akawaombe radhi huko ili apate hifadhi kwa nguvu ya mizimu hiyo ya Kasomangila chini ya Waswezi.



    Wakati Mama Masu akiwa ndani ya basi kuelekea mkoani Tabora kisanga kingine kinatokea katika kituo cha Polisi mkoani Tabora ambako Sajent Malumbo alikua katika ofisi yake ya upelelezi, alikua ameketi juu ya kiti chake huku akiwahoji watuhumiwa wake wa kesi ya kule Kipalapala mkoani Tabora ambao walikua wameketi chini sakafuni, japokua kesi haikua ni ya mauaji tena kama ilivyotafsiriwa mwanzoni lakini ilikua ni kesi ngumu sana baada ya mtuhumiwa aliekua mahututi hospitalini kutoweka ghafla, wakati Sajent Malumbo akiendelea kuwahoji watuhumiwa wale ili japo kupata kujua japo labda pa kuanzia kufuatia kutoweka kwa Nyamizi ndipo alisikia sauti ya askari mwenzie nje ya ofisi hiyo ikitokea usawa wa dirishani

    “Mr Malumbo”

    “Ndi afande”

    “Kuna mgeni wako hapa”

    “Ok, nina mazungumzo kidogo anaweza kunisubiri?”

    “Lakini ingekua vema kama angekuja tu humo humo ndani maana anweza kusaidia kazi yako”

    “Ok Mlete” Sajent Malumbo alishtushwa na maneno ya afande mwenzie kua mgeni huyo anaweza kusaidia kazi aliyonayo, hakujua ni nani, akahisi labda ni daktari amekuja kutoa taarifa mpya kuhusu mgonjwa alietoweka, kwakua ofisi ya Sajent Malumbo ilikua ndani kabisa na ukizingatia kuna kona nyingi sana mpaka kuifikia hivyo ilichukua kama dakika tano hivi kabla ya Afande Salma kuingia ndani ya ofisi hiyo akifuatiwa na mgeni alitajwa, Macho ya Sajent Malumbo yalipiga usoni kwa sasa huyo alieambiwa klua ni mgeni wake lakini hakumtambua kwa haraka, alijaribu kuvuta kumbukumbuku sura ikawa iamuijia lakini haikumbuki vizuri lakini sauti kali kutoka kwa Ngaliba Kayoka, mmoja kati ya wale watuhumiwa wake wawili waliokua wamekaa katika sakafu ya zege ya ofisi hiyo iliweza kumpa jibu la swali lake

    “NYAMIZI?” Ngaliba Kayoka alishtuka sana kumuona Nyamizi akiwa mzima kabisa japo amefunika kilemba kichwani hivyo hakuweza kuona jeraha lililosababishwa na upanga wa Hunudu

    “Ndio mimi Mjomba”

    “Mungu ashukuriwe” Ngaliba Kayoka akainuka kwa furaha ili akamkumbatie mpwa wake huyo aliesemekana kua amekufa na baadae ikadhihirika kua ni mzima japo mahututi, na baadae akatoweka kabisa hospitalini. lakini alakemewa na sauti kali kutoka kwa Sajent Malumbo

    “Kaa chini mzee, unataka kufanya nini? Unataka kutoroka? Au unataka kutunyang’anya silaha?”

    “Hapana afande nilitaka kumpokea binti yangu, ndie huyu uliesema ametoweka hospitalini”

    “Kaa chini Mzee” Ikabidi Ngaliba Kayoka arudi aketi tena chni kwa upole, wakati huo babu yake Masu nae alikua ameketi pale chni akiangalia kila kinachotokea kwa macho ya mshangao

    “Afande Salma umemtoa wapi huyu dada?” Malumbo aliuliza

    “Amekuja mwenyewe akajieleza sasa kwa kua nilikua naijua hii kesi ndipo nikamuelewa na kumleta huku” baada ya majibu ya afande Salme sasa Sajent Malumbo akamgeukia Nyamizi

    “haya dada hebu keti hapo kwenye kiti” tayari sasa sura ya Nyamizi ilikita katika ubongo wa Sajent Malumbo, alimkumbuka haswa kwa alikwisha muona mara kadhaa alipokua hospitalini

    “Ahsante” Nyamizi akaenda mpaka kwenye kiti alichoelekezwa na kuketi kwa nidhamu

    “Enhee Nyamizi hujambo?” alianza Sajent Malumbo kumuhoji Nyamizi sasa

    “Mie sijambo afande”

    “Pole na maumivu”

    “Ahsante ninaendelea vizuri tu kwa sasa”

    “safi, haya, hawa wazee unawafahamu?”

    “Ndio, wote ni wajomba zangu”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ilikuaje wakakukata mapanga? Uliwafanya nini?”

    “Hwakunikata hata na kiwembe, ila ni Yule Hunudu mshenzi ndie alienifanyia unyama ule”

    “Hunudu? Ndo nani?” Sajent Malumbo alijifanya kutokufahamu kilichotokea japo alikua na habari zote za tukio zima la Hunudu kuvamia kule kipalapala na kumdhuru dada huyu

    “Hunudu Yule kijana mwenye Chongo kutoka kwa wachawi wa Waufi”

    “Mnh, haya hebu tuelezee ilikuaje tukio zima” Sajent Malumbo alimpa swali la mtego dada huyu ili atakapoelezea ndipo aoanishe na maelezo ya hawa babu zake Masu, Nyamizi alianza mwanzo wa tukio mpaka mwisho bila ya kupishana na maelezo ya akina Ngaliba Kayoka.. Maelezo yalikua ni ya kutisha na kuogofya sana, japokua ilikua kama vile filamu lakini ikambidi Sajent Kuamini tu sasa kwakua anaesimulia ndie aliepigwa na amekanusha kuusika kwa wazee wale zaidi ya kumtuhumu huyo Hunudu..

    “Kwahiyo hata kama tutawaachia huru hawa wazee wako una uhakika hawakukudhuru hata kidogo?”

    “Ndio afande, hawa ndio waliokua wakipigana na Hunudu muda mfupi kabla hajanirukia mimi wakati nilipokua nakimbilia kuwaita ndugu zetu wengine kama nilivyokueleza”



    Wakati Nyamizi alipokua akitoa maelezo yake Sajent alikua akiendelea kuandika maelezo hayo kwa utulivu na umakini wa hali ya juu

    “Afande acha mie nikaendelee na majukumu ya kujenga Nchi nyie endeleeni kupambana na ushirikina” Sauti hii ilimshtua Sajent Malumbo, ilikua ni sauti ya Afande Salma, Malumbo hakujua kama kumbe afande Salma alikuwepo muda wote mule ndani maana kwa utata wa stori ile alijukuta kama hamuoni vile. Baada ya Sajent kumaliza kufanya mahojianona kuandika aliwasainisha watuhumiwa wote na kisha akamsainisha Nyamizi katika maelezo yake kisha alinyanyua simu na kumpigia Koplo Bangi wa Shinyanga na kumuelezea hali halisi ilivyo ili sasa kama ni dhamana Masu apewe, alipomaliza kufanya kazi hiyo akawatafuta kwa njia ya simu ndugu zao na kina Ngaliba kayoka waliowasili kituoni hapo mara kadhaa kwa ajili ya kuwadhamini ndugu zao ili sasa waweze kufanya hivyo Ndugu waliwasili na kukutana na Nyamizi hapo kituoni walifurahi sana, wakapokeana na kulakiana kabla ya kuanza zoezi la kuwawekea dhama wazee wao lakini kutokana na taratibu baadhi za kipolisi zoezi la udhamini halikukamilika siku hiyo, ikabidi Ndugu waondoke ili kesho yake ndipo wakawatoe akina Ngaliba Kayoka na Babu Masu

    *****

    Huko Shinyanga nako Baada ya Koplo Bangi kuongea na mkuu wake wa Kituo ambae amekua akimsaidia kwa karibu sana kupambana na kesi hii waliamua kuwapa dhamana watuhumiwa wao wawili Mzee Kikoko na Masu hivyo Mzee Kagomba , Sheikh Jabu na Mzee Maguno waliwasili kituoni hapo kuwadhamini watu wao lakini zoezi halikua rahisi japo waliambiwa dhama iko wazi, walifanikiwa kumdhamini Masu tu ila Mkuu wa kituo aligoma kumuachia Mzee Kikoko bila shaka kutokana na majibu mabaya ya Kikoko tangu awapo pale kituoni, Baada ya akina Mzee Kagomba kuhangaika sana ndipo mkuu huyo akawaambia kua waende kesho yake kumtoa hivyo ikabidi sasa kwa siku hiyo waondoke na Masu tu

    *****



    Siku ya ijumaa ikawasili ikiwa imebaki siku moja tu ya Kafara kwa Mama Masu, bila shaka sasa Waufi walikua wakisubiri muda ufike ili wammalize Mama Masu ambae muda huo alikua ameshafika Tabora mjini kwa baadhi ya ndugu zake waishio hapo ili jioni yake wamsindikize sasa Kipalapala kwa ajili ya dhamira aliyoikusudia. Jitihada za waufi za kumshambulia Masu zikawa kama zilizofifia sana kitu ambacho kilifanya sasa hali iwe mbaya sana kwa Mama Masu. Asubuhi hiyo tayari Wazee wa mji walikua katika kituo cha Polisi kwa ajili ya kumdhamini Mzee Kikoko japo zoezi lilizidi kua gumu japo Kikoko hakua na makeke tena lakini dharau na majigambo yake yalikua yakimgharimu, Mkuu wa kituo alikua ‘busy’ sana na shughuli zake na alitoa taarifa kituoni kua mtu yeyote asitoe dhamana kwa Mzee Kikoko mpaka atakapoidhinisha yeye. Baada ya kuhangaika sana kwa wazee hawa ndipo saa Nne asubuhi kwa huruma tu ya Ocd Nkeli akapata dhamana na kuachiwa, wakaondoka mpaka nyumbani kwa Mama Masu lakini hawakumkuta

    “Vipi huyu nae kisisina kaenda wapi?” Mzee Kikoko alikua akiuliza kuhusu mama masu

    “Usimuite kisisina mkeo, sio uungwana” Mzee Kagomba alimjibu

    “Huyu mwanamke ni kisisina tu, yeye ndie sababu ya yote haya”

    “Wewe ndie kisisina kwakua uliyafumbia macho matatizo uliyoyajua kabisa, na mkeo alikua akijivunia jeuri na ubabe wako”

    “Mimi sikua nikijua kuhusu haya mambo ya kishirikina kwa kua nilishapata kuyasahau kitambo kirefu sana, lakini kumbe yeye alikua akielewa kinachomsibu mwanangu halafu akazidi kuchochea tu”

    “Usimshushie zigo la lawama, wewe mzee mwenzangu ujuaji umekuzidi sana na ndio maana sasa yamekukumba yote haya”

    “Bwa Kagomba tafadhali ntakudandia sasa hivi nikutwange vichwa, ohoo usitake kunikoroga saa hizi”

    “Nini? We una ubavu wa kupigana na mimi? Hapo ulipo unawazo kila mia kichwani nikikusukuma tu unaanguka, halafu ukiniletea ujuaji wako nakurudisha polisi mimi ndie mdahamini wako” Maneno ya Mzee Kagomba yalimtisha kidogo Kikoko ikabidi tu sasa apunguze Munkari

    “Jamani hapa hakuna haja ya kulumbana, tuongee ki utu uzima sasa, iko hivi Bwana Kikoko mkeo Mama Masu amekwenda Kipala pala Tabora” alianza kuongea Sheikh jabu

    “Umeona sasa huyu mwanamke, ameenda kufanya nini wakati huko ndiko alipoyakoroga?!” alidakia Mzee Kikoko alieonekana kujawa na jazba kama kawaida yake, lakini aliwahiwa na Mzee Kagomba ambae licha ya kumdhamini lakini alionekana kukerwa sana na vitendo vya rafiki yake huyo

    “Acha akili za uwaluwalu wewe mtu mzima, tulia upewe habari sio unakurupuka tu, hebu Sheikh Jabu endelea

    “Haya, Mama Masu amekwenda Kipalapala kutafuta suluhu na kuwaomba radhi wazazi wake na Mama almasi pamoja na mama Almasi mwenyewe ambae nae ameondoka kaenda huko huko Kipalapala ameitwa na wazee wake wamemuambia kua kuna dharura huko… Mwanao Masu nae ameondoka amekwenda huko huko”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



     Sheikh Jabu akanyamaza kidogo huku akiwaangalia machoni wazee wenzie waliokua wakitupiana macho kama majogoo yanayojiandaa kuvaana, kisha akaendelea “Pia habari kutoka huko kipalapala ukweni kwako zinasema hivi leo baada ya kutachiwa na Polisi na wewe unahitajika huko inaonekana kuja jambo zito na la muhimu hivyo jiandae muda huu tunaenda kutafuta usafiri wa kwenda Tabora,” Maneno ya Sheikh Jabu yalimuingia sana Mzee Kikoko akawa kama aliyepagawa sana

    “Jamani kwa jinsi nilivyochoka hapa mpaka mkia sidhani kama nitaweza kusafiri leo” hapo hapo Mzee Kagomba akampigapiga Mzee Kikoko na kiganja chake begani huku akimjibu kwa dharau

    “Acha ujuha we mzee, tunaondoka sasa hivi, ingia bafuni uoge kisha tunapitia nyumbani kwangu kumchukua mke wa Sheikh Jabu na wale watoto wa Masu baada ya hapo msafara wa hiari ulio wa lazima utaanza, umeelewa” Kikoko alikua na jazba lakini akajikuta hana cha kufanya, alitamani kuuliza juu ya hao wajukuu zake alioambiwa kua wapo hapo Shinyanga lakini muda haukua rafiki tena ikabidi aingie bafuni kwa upole kabisa kichwa chini mikono nyuma, ambako baada ya kupata maji alipata chakula kasha safari ya kwenda kwa mzee Kagomba kuwachukua watoto wa Masu pamoja na mke wa kikoko ikaanza, Sheikh Jabu alikua na hali nzuri ya kiuchumi hivyo gharama zote zilikua juu yake ikiwa ni pamoja na kukodisha gari ndogo ya kuwapeleka Tabora, Kipalapala



    Wakati huo kule Tabora akina Ngaliba Kayoka na Babu yake Masu walikua wameshaachiwa kwa dhamana, na mpaka muda huo walikua nyumbani kwa ndugu zao hapo hapo Tabora mjini katika kata ya Chemchem, japo walikua wamechoka ila walipokea taarifa kutoka kwa mkuu wa waswezi huko Kipalapala kua ni lazima siku hiyo waende huko kuna jambo zito linatakiwa kufanywa hivyo waliamua kupumzika ili mchana waanze safari ya kuelekea huko kipalapala

    *****



    Safari ya kutoka Shinyanga ilikua ndefu sana lakini ilikua ni lazima Kikoko afikishwe kipalapala siku hiyo, Ndani ya gari alikuwepo Sheikh Jabu alieketi siti ya mbele, Mzee Kikoko, Mzee Kagomba na Mke wa Sheikh Jabu walikua wameketi katika siti tau za nyuma huku wakiwa wamewabeba Zani na Fani watoto wa Masu majira ya saa tisa lasiri tayari akina Kikoko walikua Tabora mjini, hakika dereva waliempata alikua vizuri katika usukani, hawakua na haja ya kupumzika wala kupitia popote ikabidi tu waunganishe kipalapala ili wakapumzike huko huko, saa kumi na moja kasoro walikua tayari wamewasili katika ardhi ya kipalapala, walipofika walipokelea kwa mbwembwe kubwa za kimila, walistaajabu jinsi walivyokuta uwanja umefurika watu, kundi la wakazi wa kipalapala walikua wamejaa wakiwa wote wamevalia mavazi maalum wayavaayo waswezi, walikua wamejifunga Khanga sehe ya juu kifuani na chini, huku wakiwa wamejipaka pemba katika nyuso zao, ngoma za waswezi zilikua zikipigwa huku baadhi ya vijana wakicheza kwa mbwembwe kwa ule mtindo wao wa kutingisha mabega,



    Baada ya Akina Kikoko kuwasili wote walifikishwa mpaka mbele ya Mkuu wa Waswezi aliekua amejitanda shuka jeupe huku akiwa amejifunga kilemba chekundu, wote wakainama kumsalimia mkuu huyo ambae alikua ameshika Usinge kama ule ambao Masu alikabidhiwa na Marehemu Kishindo akausahau kwenye basi, Macho ya Kikoko yalikua hayatulii alikua haamini kila anachokiona mahala pale, Aliwaona wake zake wote wawili na watoto zake wadogo waliokua wamekwenda likizo huko kipalapala karibu mwezi sasa, hakujua ni mbinu gani aliyotumia Mama Masu ambae ni adui mkubwa wa ukoo huo mpaka wamekaa nae kwa wema vile hakujua kinachoendelea, pia alimuona Masu akiwa amekaa mbele kabisa karibu na Mkuu huyo wa Waswezi, na baadhi ya watu aliokua akiwafahamu

    Ndipo sasa baada ya salamu ile kama vile waliokua wakisubiriwa ni wao tu, watu wote waliketi kwa utulivu ndipo sasa Mkuu wa Waswezi aliposimama na kuanza kuongea baada ya salama yao ya lugha ya Kinyamwezi

    “Jamani tumekutana hapa kwa kazi kubwa tatu ama nne tu…” watu wote walikua kimya wakimsikiliza mkuu “..Kwanza ni Zindiko kubwa kwetu sote hapa ili kujiweka salama dhidi ya hila za Waufi na wachawi wote, pili leo tutamtawaza Masu cheo kikubwa sana kutoka na shida na dhahma alizopambana tumeamua kumpa mamlaka na nguvu kubwa sasa, pia Bibie alieuiba ujauzito wa Masu na kujipa u-mama wa lazima nae yupo hapa akiwa amekuja kuomba msamaha na kukiri kosa lake, pia Bwana Kishindo nae yupo hapa, hivyo kwa atakaesamehewa leo itakua ni bahati kwake na kwa atakae adhibiwe itakua ni balaa kwake..” Macho ya Kikoko yalimtoka Pima kusikia habari za kuadhibiwa akajua tu bila shaka kwa upuuzi alioufanya basi hatotoka salama, wakati huo mkuu alikua akiendelea kuongea kwa sauti kali lakini ya utlivu sana “… Lakini kabla ya yote hayo kwanza tutafanya mazishi ya heshima ya kumzika mpendwa wetu Nyamizi ambae aliuawa kwa kupigwa panga la kichwa na kijana mmoja mshenzi anaetumiwa na Waufi..” Maneno hayo sasa yalimshtua sana karibu kila aliekua akijua kua Nyamizi alikua hai, Ngaliba Kayoka alimuangalia Babu yake Masu kwa jicho la mshangao lakini Babu Masu alionekana kua naijua siri hiyo, baada ya ukimya kutawala kwa dakika chache ndipo Mkuu wa waswezi akaendelea

    “..Baada ya Nyamizi kupigwa panga alifariki pale pale na mpaka wakati anafikishwa hospitali alikua ameshafariki lakini kwa Nguvu ya Waswezi tulikiinua kivuli chake kilichoendelea kuonekana kua kama yupo hai ili iwe ni sababu ya kuachiwa kwa wazee wenu waliokua wakituhumiwa kumuua, hakika huyo Hunudu alikua ametushinda vikali kama isingekua nguvu ya Waswezi, na baada ya kivuli cha Nyamizi kumaliza kazi husika pale Polisi sasa leo hatuna jinsi ni kumzika tu mpendwa na Shujaa wetu, Maiti yake iko ndani imeshaandaliwa kwa ajili ya amaziko, ila baada ya matukio yote haya kukamilika mwisho nitawatambulisha viongozi wa kilua kutoka Kgoma nao tumekua tukishirikiana nao kwa kariu sana kwenye vita hii, Baada ya maziko tutaanza mkakati wa mwisho wa kummaliza huyo Hunudu kivyovyote kabla jua halijachomoza kesho, Eeeh Mungu tusaidie, na Mizimu itusikie” Mkuu wa Waswezi akahitimisha kuongea na kuwaacha wote wakiwa midomo wazi

    *****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wakati hayo yakiendelea huko Kipala pala, Hunudu alikua njiani kwa kasi ya ajabu akielekea huko kwenda kummaliza Mama Masu na yeyote atakae kaa mbele yake, agizo hilo alipewa na wakuu wake, na akapewa Shart kua kama atashindwa basi Mzimu wao wa WAUFI Utawaangamiza wote



    MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Blog