Simulizi : Nilioa Jini Nikamsaliti
Sehemu Ya Nne (4)
Mzee Mukti alikata simu na kuangalia kwenye rada zake alijikuta mwili ukimtetemeka baada ya kuona ni jini Nargis mke wa Thabit waliyemdhibiti asiingie popote alipo Thabit na mkewe. Alijiuliza alikosea wapi mpaka kuingia alipopafunga, baada ya kuangalia zaidi aligundua ujaji wake ndiyo ulioua nguvu za kumzuia pale alipokwenda kibinadamu tofauti na mwanzo alipokwenda kijini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini alifarijika kwa vile hakuwa na madhara yoyote na kilichotokea kilikuwa kiini macho kisicho na madhara yoyote. Kwa vile aliweza kuingia popote katika umbile la kibinadamu alitafuta dawa ya kumdhibiti asiingie popote kwa umbile lolote. Baada ya kujua kilichotokea ofisini alimpigia simu Subira kumjulisha. Baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo mzee wangu.”
“Nimeliona tatizo.”
“Umeona tatizo gani?”
“Aliyekuja hapo ni mke wa mumeo jini Nargis.”
“Mungu wangu nimekwisha,” Subira alishtuka kusikia vile.
“Usiogope hawezi kukufanya chochote,” mzee Mukti alimtoa hofu.
“Si ulisema umemdhibiti imekuwaje ameweza kuingia ofisini?”
“Yule mwanamke ana akili sana najua atanisumbua lakini mimi ndiye mwisho wa viumbe wale. Baada ya kuja katika umbile la kijini kushindikana aliamua kuja katika umbile la kibinadamu lakini lisilo na madhara.
Kwa nilivyotengeneza hawezi kufanya chochote hata ningemuacha aje asingewazuru.”
“Babu sitaki kumuona kwa uzuri wake akikutana na Thabit lazima watarudiana.”
“Hawawezi, ila kuna dawa itakayomdhibiti kila kona atakayowafuata hawezi kuwafikia.”
“Tena ifanye leo hii.”
“Baada ya kuona hivyo silazi damu ila kilichotokea usimwambie mumeo, mwache kama zuzu ili tufanikishe mambo yetu.”
“Sawa babu, tena nitakupa zawadi kubwa kwa vile unanipigania.”
“Viumbe hawa mimi ndiyo kiboko yao,” alijigamba mzee Mukti.
“Nakuaminia mzee wangu.”
Mzee Mukti alitengeneza dawa nyingine ya kumdhibiti Nargis na kwenda kuiweka nyumbani na kwenye maduka yote na kumweleza Subira aliyoiweka ni kiboko, Nargis akiigusa lazima apotee kabisa.
“Mmh! Nashukuru mzee wangu, natamani kusikia amekufa kwani sina raha.”
“Dawa niliyoiweka akigusa anapotea.”
“Utazidi kunifurahisha mzee wangu, kesho nitakuletea zawadi yako nina mpango wa kukuongezea gari lingine mwezi ujao. Nina amini mafanikio yangu yanapitia mikononi mwako.”
“Nami nitahakikisha huguswi na jini wala wachawi.”
Maneno ya mzee Mukti yalishusha presha ya Subira baada ya kumpanda kutokana na vitu vilivyotokea muda mfupi. Alijikuta akimuona mzee Mukti kama Mungu wake kwa kumtegemea kwa kila kitu na kumsahau aliyemuumba.
***
Siku ya pili kama kawaida Nargis alifika ofisi kwa Thabit, akiwa katika umbile la kibinadamu alitembea taratibu kuingia eneo la ofisi. Alipofika getini alimsalimia mlinzi na kuelekea kwenye ofisi ya mumewe kwa mwendo uliomfanya mlinzi amsindikie kwa macho na kuusifia uzuri wake kimoyomoyo.
Alipofika katika ya uwanja alishtuka kusikia mwili wote ukiwaka moto, kila alipokuwa akikanyaga aliungua na kumfanya apige kelele za maumivu.
“Moto...moto...motoo... nakufa Thabit mume wangu unaniua.”
Sauti yake kali ilimtisha kila mmoja, Subira na Thabit walitoka nje na kumuona Nargis akipiga kelele huku akiungua moto. Kwa vile alikuwa amefika katikati alirudi alipotoka huku akipiga kelele za kuungua moto. Nargis alirukaruka kwa maumivu ya moto kila alipokanyaga aliungua. Alipotoka eneo la ofisi ya Thabit alitoweka ghafla na kuacha wakishangaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mlinzi ndiye aliyesikia maneno ya Nargis na kujiuliza yule mwanamke alikuwa nani, taratibu kumbukumbu zikaanza kumjia na kujiuliza alimuona wapi.
Maneno ya kumwita Thabit mume wake na kusema ana muua yalikuwa na maana gani. Alipanga kumuuliza Thabit kwa wakati wake.
Kwa Subira ilikuwa furaha na kuzidi kumuamini mzee Mukti kwa kazi yake iliyokuwa na majibu ya papo kwa papo. Thabit alichanganyikiwa na kujiuliza kile nini huku akimkumbuka yule mwanamke aliyekuwa akipiga kelele za maumivu ya kuungua moto na kutoweka ndiye aliyekuja jana yake.
“Kile nini?”
“Yule mwanamke si mtu mzuri ndiyo wale wachawi waliotaka kuturudisha nyuma na kutufilisi,” Subira alitengeneza uongo.
“Nimeamini mzee Mukti kazi anaiweza, ndiyo jana nilishangaa mtu kuja kujifanya ananipenda kumbe ana yake,” Thabit aliunga mkono bila kujua kilichokuwa kikiendelea.
***
Nargis alikwenda kujitupa baharini kupunguza mauivu ya moto ambao ulimchoma sehemu kubwa ya mwili wake. Alipogusa maji alipoteza fahamu na kuokotwa na vibwengo ambavyo vilipeleka taarifa chini ya bahari. Walitumwa vijakazi waliomfuata na kumpeleka chini ya bahari mwili wote ukiwa na majeraha makubwa ya moto.
Alipofika tu alipatiwa huduma ya haraka ya kuyatibu madonda makubwa yaliyosababishwa na moto uliomuunguza.
Watoto wake walipomuona walilia sana na kuapa kulipa kisasi kwa mtu aliyemfanya vile mama yao. Lakini bibi yao aliwakataza kwa kuamini wanaweza kupotea kwa vile hawakuwa na nguvu ya kupambana kutokana na kuchanganya damu ya kijini na ya binadamu.
Baada ya kumpatia huduma na kumuacha apumzike, malkia Zabeda alimwita mwanaye wazungumze juu ya hali ya Nargis na jinsi ya kumsaidia.
Alipofika tu alipatiwa huduma ya haraka ya kuyatibu madonda ya moto ambayo yalikuwa makubwa. Watoto wake walipomuona walilia sana na kuapa kulipa kisasi kwa mtu aliyemfanya vile mama yao. Lakini bibi yao aliwakataza kwa kuamini wanaweza kupotea kwa vile hawana nguvu kubwa ya kupambana kutokana na kuchanganya damu ya kijini na ya kibinadamu.
Baada ya kumpatia huduma na kumuacha apumzike, Malkia Zabeda alimwita mwanaye wazungumze juu ya hali ya Nargis na jinsi ya kumsaidia.
SASA “Mwanangu naomba tumsaidie mdogo wako hali inatisha.”
“Mama mimi msiniingize mwanao kazidi ubishi na akiendelea watamuua. Moto uliomuunguza si wa mchezo bila nguvu za kijini tungempoteza.”
“Najua, lakini bado yupo chini yetu, lazima tumsaidie.”
“Mama mimi sipo tayari kujiingiza kwenye matatizo, usalama wake ni kuachana na baba Zamzu bila hivyo mwanao atakufa.”
“Kwa ubishi wake siamini kama atakubali, namjua vizuri Nargis, kitendo cha kuumizwa patachimbika bila jembe.”
“Mama mwanao haambiliki, ubishi wake sasa hivi anapotea.”
“Ndiyo hivyo damu nzito kuliko maji hatuwezi kumuacha, basi akitoka mfuate nyuma akizidiwa msaidie.”
“Sawa mama,” Hailat alikubali ili kumfurahisha mama yake lakini aliamini nguvu za wapinzani wao ni kubwa hasa alipouona moto aliochomwa mdogo wake ulimtisha hata chuma kingeyeyuka.
Baada ya kumzuia jini Nargis, Subira kwa furaha alimpelekea zawadi ya gari alilomuahidi na kuzidi kumtia kichaa mzee Mukti.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa furaha aliyokuwanayo, mganga huyo alimuahidi Subira kumpa dawa nzuri zaidi ambayo huwa haitoi ovyo ambayo ilitakiwa kufanywa sehemu saba kwa ajili ya kumficha ili akitafutwa ashindwe kupatikana.
Sehemu ya kwanza aliyopanga kumficha ilikuwa baharini kwenye maji ya shingo, sehemu ya pili kwenye vichuguu, sehemu ya tatu kwenye mti mkavu na sehemu ya nne kwenye jalala.
Sehemu ya tano chooni, sehemu ya sita njia panda na sehemu ya saba kwenye mti mkubwa.
Kukamilisha maandalizi ya dawa hiyo, alipanga kwenda Msumbiji kuongeza vitu vilivyohitajika ambavyo aliamini vingekuwa vya mwisho kumtengenezea Subira.
Mzee Mukti aliamini ndiyo kete ya mwisho ambayo ilikuwa zawadi kwa Subira baada ya kuonesha kumjali kwa kuyabadili maisha yake tofauti na watu wengi aliowasaidia hawakuwa na shukurani baada ya kufanikisha mambo yao.
Alipanga baada ya wiki moja asafiri kwenda Msumbiji ambako angekwenda kuchota mzigo wa nguvu kwani alikuwa na fedha ya kununua dawa nyingi ambazo zingefanya kazi kwa muda mrefu. Subira naye alifurahia maisha ya ndoa baada ya kufanikiwa kumdhibiti jini Nargis.
Mlinzi wa getini alitafuta nafasi ya kuzungumza na Thabit juu ya tukio la mwanamke kuungua moto na kauli zake wakati akipiga kelele kwamba aliungua moto ambao hakuuona zaidi ya kurukaruka kutoka eneo la ofisi ile na alipotoka akatoweka kiajabu. Aliyarudia maneno ya Nargis akilini pale alipokuwa akilalamika huku akiteseka na moto usioonekana:
“Moto...moto...motoo...nakufa Thabit mume wangu unaniua bure bila kujua.”
Alibakia na maswali ambayo aliamini wa kuyajibu ni bosi wake tena angemuuliza akiwa peke yake. Alisubiri siku Subira aliyowahi kuondoka na gari lake na kumuacha mumewe kazini. Thabit alitoka kazini majira ya saa mbili na nusu usiku alipofika getini alimkuta mlinzi.
Alimuaga kama kawaida, lakini mlinzi alimuomba wazungumze kitu, kwa vile Thabit alikuwa hana makuu aliegesha gari pembeni na kuzungumza na mlinzi wake.
“Niambie naona leo una jambo!” Thabit alimuuliza mlinzi.
“Bosi samahani kama nitakalo lizungumza litakuudhi,” mlinzi alijihami.
“Zungumza tu jisikie huru kuzungumza chochote,” Thabit alimtoa hofu.
“Bosi unakumbuka wiki moja iliyopita kuna kitu kisicho cha kawaida kilitokea?”
“Kitu gani?’
“Kuungua moto yule mwanamke mzuri?”
“Yaani yule mwanamke sielewi kwa nini ananifuatafuata!”
“Unajua bosi maneno ya yule mwanamke yamenishtua sana.”
“Maneno gani?”
“Nilimsikia akikuita mume wake na kusema unamuua bure bila kujua.”
“Sasa John mimi nina mke mwingine zaidi ya Subira?”
“Lakini bosi shemu Nargis yupo wapi?”
“Nargis?” Thabit alishtuka.
“Ndiyo, tena yule mwanamke anafanana na Nargis.”
“Kwa nini unasema ni Nargis?”
“Hata alipokuja alinisalimia habari za siku huku akilitaja jina langu.”
“John achana na habari za Nargis, kumbuka alikuwa mke wangu sasa hivi nina mwanamke mwingine.”
“Basi bosi nilitaka kujua hilo tu.”
“Nimekusikia, achana na mawazo ya mtu asiyekuwepo, sasa hivi nina maisha mapya kabisa.”
“Nimekuelewa.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Basi tutaonana kesho, usiku mwema na kazi njema.”
“Na kwako pia.”
Thabit aliingia ndani ya gari lake na kuondoka kuelekea nyumbani huku akirudia maneno ya mlinzi na kujikuta akisema mwenyewe:
“Nargis...Nargis...Mmh!“ jina lilikuja lakini lilipotea akilini.
Lakini wazo lile lilipotea baada ya kupigiwa simu na Subira alipokea na kuzungumza:
“Haloo mpenzi.”
“Upo wapi mume wangu?”
“Njiani ndiyo narudi.”
“Wahi basi mume wangu si unajua nipo kama kinda la ndege linalohitaji joto la mzazi wake, wewe ndiyo joto langu.”
Usihofu nakuja mpenzi wangu.”
“Leo nimekupikia chakula ukipendacho cha tambi na nyama.”
“Ndiyo maana nakupenda, na ile ahadi ya nyumba ya ghorofa ujenzi unaanza wiki ijayo.”
“Jamani mume wangu nakupendaje!”
“Asante mume wangu.”
“Basi tusimalize maneno yote nikakosa ya kuongea nikiwa pembeni yako.”
“Haya mpenzi ufike salama.”
“Amina.”
Baada ya kukata simu alijikuta mawazo yake yamehamia kwa mkewe na kusahau kuhusu mkewe NargisNargis baada ya kupata nafuu alirudiwa na fahamu na kujitambua baada ya kupoteza kwa wiki nzima.
Kila alipojiangalia mwili wake ulivyoharibika kwa moto alilia na kuapa kufa na mtu. Hakukubali kushindwa kwa haki yake, suala lake hakutaka kuwashirikisha familia yake kwa vile aliamini vita ile ni kubwa hivyo aliamini kabisa kama akishindwa basi afe peke yake.
Wanaye mapacha Zumza na Zamzu baada ya mama yao kupata nafuu waliomba wamsaidie kwenye vita ile.
“Mama ukiondoka tunaondoka wote,” Zumza (Kulwa) alimwambia mama yake aliyekuwa akijiandaa kuondoka.“Hapana wanangu ninyi bado wadogo, tutaondoka siku nyingine kwanza sasa hivi usiku.”
“Hata kama ni wadogo tutakufa na wewe,” Zamzu (Doto) alimwambia mama yake.
“Mama ukifa tutabaki na nani hatukubali? Ukiondoka tunakufuata,” Zumza alimuunga mkono mdogo wake. “Sikilizeni watoto wangu wapenzi, najua mnanipenda sana mama yenu, nakuombeni kitu kimoja, kwa vile mmejitolea kunisaidia mama yenu nimepanga kwenda kwenye mapambano mpaka nipone kabisa,” Nargis aliwadanganya wanaye.
“Mama, kwa baba tunakwenda lini?” Zamzu aliuliza.
“Kuna safari nakwenda nikirudi tutakwenda kwa baba yenu, sawa wanangu?”
“Sawa mama,” walikubali kwa pamoja.
Kwa vile ulikuwa usiku wanafamilia yake wakiwa wamelala, alitoka kwenda kujaribu tena huku ajiuliza amekosea wapi kwani aliamini alichokuwa akikipigania ni haki yake hata kama akifa angekuwa amekufa kwa haki yake ya msingi.
Alijua majini na binadamu wote ni viumbe wa Mungu na ndoa yake aliyofunga na Thabit ilifuata taratibu zote hivyo alitambulika mbele ya Mungu.
Alitoka kwa kuibia kuelekea nje ya maji, kabla hajatoka alishtuka kuitwa nyuma yake.
“Mwana wa malkia.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kun’za unasemaje?” alishangaa alimuuliza Kun’za mtwana mwenye kibyongo ambaye alikuwa mkongwe kuliko wote na ndiye aliyekuwa mtiifu kuliko wote.
“Binti mfalme najua una matatizo mazito kutokana na vita yako na wanadamu.”
“Umejuaje?” Nargis alishtuka sana.
“Najua tu binti wa mfalme wa bahari ya dhahabu,” Kun’za alijibu kwa utulivu kama kawaida yake.
“Nani kakuambia?” alizidi kumuuliza.
“Hata bila kuambiwa uso wako unaonesha kila kitu na safari yako inaonesha si njema kwako.”
“Wewe umejuaje?” Nargis alizidi kumuuliza.
“Najua kwa kukutazama.”
“Wewe Kun’za mtwana umetoa wapi uwezo wa kufahamu mambo ya wakubwa?”
“Babu yangu ni mchawi aliyefukuzwa kwenye anga za majini na kwenda kukaa kwenye miamba myeusi ambayo hakuna jini wala kiumbe chochote kilichowahi kufika huko. Mimi nilifika baada kuelekezwa na marehemu mama yangu ambaye alinielekeza nimtafute babu yangu alipo na alinilazimisha lazima nifike japokuwa sehemu yenyewe ni mbali sana.
“Baada ya kuelezwa hivyo nilitoka nyumbani kuelekea kwenye miamba myeusi, huwezi kuamini nimetumia miaka mia mpaka kufika kwenye miamba hiyo. Sehemu yenyewe ina kiza cha ajabu inataka moyo kuvuka miamba mpaka kuupata mlango wa kuingia ndani ya mwamba wa kiza ambamo yumo yeye.”
“Kun’za nimekusikiliza, sijui babu yako mchawi, sijui anakaa kwenye miamba myeusi katika mwamba wa kiza, una maanisha nini?”
“Shida yangu nikupeleke kwa babu yangu akusaidie, katika viumbe wenye huruma kama wewe .”
“Kun’za toka nizaliwe kwanza leo ndiyo nasikia hiyo miamba myeusi, katika utundu wangu toka utotoni nimeishafika kila kona ya bahari lakini sijawahi kuona wala kusikia miamba hiyo. Hiyo miamba ipo bahari gani?”
“Hiihii ya dhahabu.”
“Kun’za hakuna kitu kama hicho!” Nargis alibisha.
“Binti mfalme, bahari hizi hata baba yako nina imani hazijui, mzee Dudumizi huu ni mwaka wa mia tatu yapo huko. Siri hii naijua mimi peke yangu na alinikanya nisimwambie mtu. Lakini kutokana na matatizo yako lazima nikupeleke najua utafanikiwa na utampata mumeo.”
“Kun’za unaniambia kweli au unanitania?” Nargis hakumuamini.
“Binti mfalme wa bahari sijawahi kukudanganya, najua katika watwana wako mimi ndiye mtiifu kuliko wote.”
“Najua, pamoja na kukuamini sana Kun’za lakini kwa hili mbona linanitia shaka?”
“Naomba uniamini, nakuapia utampata mumeo ila nakuomba kitu kimoja ukirudi kwa mumeo naomba niwe mlinzi wako mkuu.”
“Hilo halina shida, lakini mbona kufika huko ni miaka mingi, miaka mia ni mingi sana heri niendelee kupigana mpaka nijue hatima yangu.”
“Baada ya kufika kule alinipa dawa ya kuweza kufika kwa siku moja tena kwa saa chache.”
“Huyu babu yako ana miaka mingapi?”
“Mia saba.”
“Duh! Sasa tutakwenda lini?”
“Nataka tuondoke usiku huu, mpaka kunakucha tuwe tumerudi.”
Kwani alifanya kosa gani lililosababisha kufungwa huko?”
“Kwa kweli sijui, nilijaribu kumdodosa aliniambia niachane nayo bali nifuate kilichonipeleka.”
“Basi tuondoke.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kun’za alimshika mkono Nargis na kuzama chini ya bahari kwa kutembea kwa kasi ya ajabu ambayo ilimtisha Nargis. Ilikuwa kasi ya ajabu ambayo hakuwahi kwenda nayo katika maisha yake. Walitembea kwa saa saba na kufika kwenye miamba myeusi.
Sehemu yenyewe ilikuwa na kiza cha ajabu ambacho kilimtisha Nargis, lakini alificha hofu yake.
Pamoja na kuwa yeye ni jini kwa mara ya kwanza woga ulimtawala kutokana na kiza cha ajabu cha eneo lile. Hali ya ukimya nayo ilizidisha kuogopesha kama angekuwa peke yake angekufa kwa hofu. Lakini alimshangaa Kun’za ambaye hakuonesha wasiwasi wowote, alimshika mkono na kutembea naye kwenye miamba ya barafu yenye kugandisha damu.
Kila walivyotembea ndivyo baridi kali lilivyozidi kuongezeka baada ya muda Nargis alianza kusikia ganzi kali mwilini na kuwa na wasiwasi labda Kun’za kampeleka kule kumuua. Moyoni alijiapia watakufa wote hawezi kukubali kufa peke yake, siku zote alikuwa hakubali kushindwa.
“Kun’za mbona hatufiki? Nasikia ganzi ikisambaa mwili mzima nahisi damu kuanza kuganda.”
“Tutafika sasa hivi.”
Ghafla ubaridi ulipotea na kuanza kusikia joto ambalo kila walivyokwenda ndiyo lilivyoongezeka.
“Kun’za huku wapi tena?”
“Tunaingia mwamba wa moto.”
Baada ya mwendo kidogo walifika kwenye miamba wa moto, walipoanza kukanyaga barafu yote iliyokuwa imewaganda iliyeyuka na kuanza kuhisi joto kali. Hali ile ilizidi kumtisha na kuona ameingia dunia nyingine kabisa ambayo hakuwahi kuiota wala kuisikia.
Baada ya mwendo wa saa moja walifika kwenye mwamba wa giza ambao lilikuwa zito mpaka hewa ikawa shida kupatikana. Nargis alijuta kwenda sehemu ile kwani aliamini kabisa Kun’za alimpeleka kule kumuua. Baada ya muda alihisi baridi kali na hewa nzuri kisha mwanga mkali ulioyachoma macho yake.
Baada ya mwendo wa kutembea juu ya miamba alitokea kwenye mwamba mmoja uliokuwa na mlango.
“Tumefika,” Kun’za alimwambia waingie ndani.
Waliingia na kufika kwa kiumbe kilichokaa kama mdudu Karugu yeye kwa mwili wake wote kufunikwa na miba midogodogo na manyoya na kufanya uso wala viungo vingine visionekane. Yule ndiye aliyekuwa babu yake Kun’za babu Dumidumzi.
“Karibu Nargis mwana wa mfalme wa bahari ya dhahabu,” baba Dumidumzi alisema huku akijilaza kifudifudi kuonesha heshima kwa mwana wa mfalme.
“Asante mzee Dumidumzi.”
“Nina imani Kun’za ana mapenzi makubwa kwako mpaka kukuleta huku, poleni na misukosuko ya safari hiyo ndiyo inayonifanya nisifikiwe na kiumbe chochote. Kiumbe kinachokuja huku basi huwa kimedhamiria nami sitakiacha kiondoke mikono mitupu lazima nikipe zawadi kubwa.”
“Nitashukuru mzee wangu.”
“Mshukuru sana Kun’za kwa kukuponya kwani safari yako ilikuwa ya kifo usingerudi salama kwa vile adui yako kajipanga na anaendelea kujiimarisha. Kwa nguvu za kijini za kawaida hamumuwezi.”
“Naomba msaada wako mzee Dumidumzi.”
“Sasa unataka msaada gani mkubwa toka kwangu?”
“Kumpata mume wangu.”
“Kwa njia gani?”
“Utakayoitaka lakini nimpate mume wangu.”
“Mbona moyo wako hautaki shari sasa unataka nimtie adabu anayekusumbua, nina uwezo wa kumfanya chochote unachotaka. Nimgeuze funza wa chooni au nimuozeshe mwili mzima?”
“Mzee nataka unipe uwezo wa kumpata mume wangu bila kumwaga damu.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitakupa uwezo wa kufika popote bila kizuizi, hiyo itakuwezesha kukutana na mganga uso kwa uso na kumwambia amrudishe mumeo kwa hiyari yake akikataa rudi nitakupa kitu kimoja kitakuwa na uwezo robo ya muumba. Kwanza nitakupa uwezo wa kufanya kiini macho kitakachomkimbiza yule mwanamke mwenyewe kama hasikii mfuate mganga akileta kiburi njoo tumalize kazi. Kuna kitu anajivunia kazi ya kukichukuwa nitampa Kun’za akikichukuwa basi kila kitu kimeisha.”
“Nitashukuru mzee wangu, nitafurahi sana sijui nitakupa zawadi gani.”
“Zawadi yangu kubwa wewe ulipokuja kunitembelea.”
“Sawa babu.”
“Mnaweza kwenda ili alfajiri iwakute nyumbani kwenu, sasa hivi mtatumia muda mfupi zaidi.”
Baada ya kusema vile waliruhusiwa kuondoka, walishikana mikono na kutoweka ghafla. Nargis aliposhtuka usingizini alijikuta kitandani kwake mwili wake ukiwa hauna kovu lolote na kuwa mzuri mara dufu. Baada ya kuamka alijikuta akijiuliza kilichotokea kilikuwa ndoto au kweli kwani aliamka kitandani kwake.
Alitulia na kujifikiria jana usiku alipanga kutoroka kwenda kupambana kumrudisha mumewe mikononi mwake. Kumbukumbu zilimuonesha alikutana na jini mtwana Kun’za aliyezungumza naye na kusafiri naye kwenda kwa babu yake kwenye miamba myeusi kisha walisafiri.
Alikumbuka adha walizokutana nazo kwenye safari yao mpaka kufika kisha kukutana na babu Dumidumzi na kumpa uwezo wa kumrudisha mumewe. Akiwa katikati ya mawazo mwanaye wa kike alimshangaa mama yake kuwa na ngozi nzuri.
“Ha! Mama umepona ulikwenda wapi, sasa hivi huna makovu hata moja!”
Kauli ya mwanaye ilimfanya ajichunguze na kugundua hana kovu na ngozi yake ilikuwa nzuri sana.
Kaniitieni Kun’za,” aliwatuma wanaye kwenda kwa mtwana Kun’za.
Walitoka na kumfuata na kumkuta akiendelea na kazi na kumweleza anaitwa na mama yao. Aliacha kazi na kwenda kumsikiliza binti wa mfalme wa bahari ya dhahabu. Alipofika alikaribishwa chumbani kwake kwa mara ya kwanza.
“Naam binti mfalme.”
“Eti jana kuna sehemu tulienda pamoja?”
“Ndiyo binti mfalme, tulienda kwa babu kwenye miamba myeusi.”
“Ooh! Kwani unafanya kazi gani?”
“Ya usafi.”
“Sasa hivi utahamia kwenye bustani kuwasimamia wenzako nami nakuja kutoa amri.”
Baada ya kusema vile alitoka hadi kwenye bustani na kuwaita watwana na vijakazi wote na kuwaeleza kuanzia siku ile kiongozi wao atakuwa Kun’za kwa kuwasimamia bila kufanya kazi yoyote na walipiga magoti kukubaliana na agizo la binti mfalme.
Baada ya kupata uhakika alipanga kuanza vimbwanga vyake usiku vya kumtisha mke wa Thabit ili aikimbie nyumba na yeye kurudi kwenye nyumba yake. Moyoni alipanga kumpa zawadi kubwa Kun’za siku atakapomrudisha Thabit mikono mwake.
Kwa vile alitaka kutumia njia ya kistaarabu alipanga kwenda siku ya pili asubuhi ofisini na kuonana na Subira uso kwa macho. Siku ya pili asubuhi alikwenda ofisini kwa Thabit, akiwa katika vazi lake la heshima kama ilivyokuwa kawaida. Alivalia gauni refu jekundu lililokuwa limempendeza sana, chini alivaa viatu vyeupe vyenye mchuchumio mrefu na juu alijitanda mtandio wa hariri.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kujiamini aliingia getini kama ilivyokuwa kawaida yake alikwenda kumsalimia mlinzi ambaye alishtuka kumuona tena.
“Za asubuhi John?”
“Nzu..nzuri dada.”
“Niite Nargis.”
“Ooh! Si...si...wewe u...uli...kuwa m...m...ke wa...wa..”
“John kigugumizi cha nini, ndiye mimi shemeji yako wa ukweli!”
“Mmh! U...u...likuwa wa...wapi?”
“Utajua muda si mrefu, Thabit yupo?” Nargis alijifanya hajui kitu.
“Ha...ha...jafika.”
“Mkewe?”
“Yu...yu...po.”
“Naweza kwenda kuonana naye?”
“Ndi...ndi...yo.”
Nargis pamoja na uwezo wake wa kuweza kuingia popote bila mtu kumuona siku ile hakutaka kutumia nguvu za kijini bali busara ya kibinadamu ili waelewane. Lakini kama ingeshindikana angetumia nguvu za kijini tena zilizoongezwa nguvu na mzee Dumidumzi.
Alitembea kama kawaida yake kwa madaha kama hakuna mwanamke mwingine mzuri chini ya jua kama yeye. Mlinzi alibakia amepigwa na butwaa huku akihofia kutokea yaliyotokea siku chache zilizopita. Lakini siku ile ilikuwa tofauti, kwani Nargis alitembea taratibu mpaka alipoufikia mlango wa ofisi na kuingia ndani.
Alimkuta Subira akiwa bize macho yake kwenye kioo cha kompyuta, harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia Nargis yalimfanya anyanyue uso wake na kukutana na uso wa Nargis wenye tabasamu pana.
“He!” alishtuka kumwona mbaya wake.
“Subira unashtuka nini?” alimuuliza huku akimtazama usoni.
“Ha...ha...pana,” Subira alibabaika kumwona kiumbe aliyeambiwa hawezi tena kumsogelea. Kwake aliona kama alikuwa kwenye njozi, alifikicha macho yake ili kupata uhakika kwa kile alichokiona mbele yake.
“Subira usisumbuke kuutafuta ukweli juu ya mimi kusimama mbele yako, ni kweli nipo mbele yako pamoja na dawa ulizopewa na mganga Mukti. Siku zote haki ya kiumbe huchelewa lakini haipotei kamwe. Umejitahidi kuchukua mali yangu kwa nguvu, nina imani siku niliyounguzwa na moto mliamini kabisa mmenimaliza.
“Ni kweli mliniweza lakini bado nakueleza haki ya kiumbe haipotei bali huchelewa, sasa nakuomba kwa hiyari yako nirudishie mume wangu. Ningeweza kukufanya kitu kibaya lakini nimechoka kupata dhambi za wanadamu, nataka njia uliyotumia kumchukuwa mume wangu uitumie kunirudishia.
“Nataka usiku wa leo nilale kwangu hujui gharama ya nyumba ile wala thamani na mali zote hujui vimepatikana vipi. Kwa hiyo kwa kauli ya kistaarabu nakuomba kuanzia sasa hivi nenda kwa mganga wako mweleze mwenye mali amerudi.
“Nina imani nimeongea kwa kauli ya kistaarabu isiyo na ghadhabu hata chembe japokuwa nazungumza na adui yangu mkubwa. Naondoka, usiku narudi kwangu rasmi hivyo sitaki nikukute, nikikukuta sitataka lawama na mtu japokuwa akili yako imejaa kiburi.”
Nargis baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka na kumuacha Subira bado kapigwa butwaa bila kujua kilichotokea mbele yake ni kweli au aliota. Alifikicha macho tena bado hakuamini alijitandika makofi na kuhisi maumivu hapo ndipo aliporudi katika akili ya kawaida.
Alinyanyuka na kutoka nje ya ofisi na kwenda hadi getini kumuuliza mlinzi, alipofika alionekana amechanganyikiwa.
“John!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naam mama.”
“Eti kuna mtu kapita muda huu?”
“Wa aina gani kwa vile wamepita wengi.”
“Mwanamke mmoja mzuuuri kavaa gauni jekundu.”
“Ooh! Ndiyo.”
“Mmh! Kazi kwelikweli,” alisema huku akishusha pumzi kijasho chembamba kikitoka.
“Kwani vipi?” mlinzi alimuuliza.
“Mmh! Sijui, hebu ngoja.”
Subira alichanganyikiwa baada ya kumuona kiumbe aliyeambiwa hawezi kufika popote alipo yeye.
Lakini aliweza kufika bila kizuizi cha aina yoyote ikiwa tofauti na maelezo ya mzee Mukti. Alijiuliza mpaka ameweza kufika mbele yake na kutoa onyo kwake aliamini hali ni mbaya. Maneno aliyoambiwa yalimtisha mpaka kufikia usiku awe amemrudisha mumewe mikononi mwake na yeye anarudi rasmi kwake.
Aliona haelewi kitu jibu angelipata kwa mzee Mukti, alijikuta akiamua kuondoka muda uleule bila kupanga vitu alivyokuwa ameanza kuvifanyia kazi wala kuzima kompyuta alitoka kwenda kwa mzee Mukti kumpa kilichomkuta asubuhi ile. Aliendesha gari kwa mawenge kidogo agonge kutokana na kuchanganyikiwa.
Lakini alifika salama Kigamboni kwa mzee Mukti ambaye alishtuka kumwona asubuhi ile huku uso wake ukionesha sintofahamu.“Mjukuu mbona hivyo kuna nini?” mzee Mukti alimuuliza huku akimshangaa.
“Babu hali ni mbaya,” Subira alijibu huku akihema kama aliyetoka kupanda mlima.
“Unaumwa?”
“Heri ningeumwa babu.”
“He! Tatizo nini?”
“Yule mwanamke amekuja.”
“Mwanamke! Mwanamke gani?”
“Jini.”
“Wapi?”
“Ofisini na kunieleza kuwa leo anarudi kwake hivyo nimrudishe mumewe.”
“Umrudishe wapi?”
“Mzee Mukti ina maana hunielewi, nimekuambia leo anarudi kwake hivyo usiku wa leo anataka kulala na mumewe.”
“Kwanza sijakuelewa kaja wapi?” mzee Mukti alimsikia lakini hakumuelewa.
“Mzee Mukti ina maana yote ninayozungumza hunielewi au unafanya makusudi?” Subira alimshangaa mzee Mukti.
“Kwanza hebu tulia maana nakuona unanichanganyia maneno mara amefika ofisini mara anataka kurudi kwake mara leo anataka kulala na mumewe sasa nisikilize lipi?”
“Mzee Mukti yote niliyosema, kumbuka ulisema akigusa tena lazima afe mbona leo kaja kama kwake tena kwa kujiamini, huoni kama hiyo ni hatari angeweza kunifanya kitu chochote kibaya?”
“Unajua mpaka sasa sielewi unachokizungumza, umeota au ni kitu cha kweli?”
“Mzee wangu mbona leo nakuona kama unanigeuza kituko, nimekueleza asubuhi hii yaani nimefika hata sijaanza kazi vizuri na kunieleza niliyokueleza eti njia niliyotumia kumchukua mumewe ndiyo niitumie kumrudisha kwake.”
“Kwa hiyo kaingia ofisini?”
“Mbona leo nimekuwa kama mwalimu wa chekechea nikueleze kwa kurudia neno moja mara kumi, ina maana kila ninalolizungumza linapita halikai kichwani?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hawezi kuingia ofisini nakataa utakuwa umeota tu mjukuu wangu.”
Mzee Mukti kutokana na zindiko alilolifanya aliamini hakuna kiumbe chochote kibaya kinaweza kuingia kwenye ofisi na nyumba za Thabit na kuwadhuru. Kusikia vile aliamini alichokisema Subira kilikuwa ni ndoto.
“Sasa babu nimekuja kubishana na wewe au unisaidie maana amesema anakuja usiku nitamdhibiti vipi?”
“Hawezi.”
“Hawezi vipi ikiwa ofisini ameingia na kutoka tena amesema kaonesha ustaarabu wa hali ya juu japokuwa mimi ni adui yake. Na amesema nikikaidi atakachonifanya Mungu anajua.”
“Hebu twende ndani,” waliongozana hadi ndani ya kilinge ili mzee Mukti aangalie kuna nini.
Baada ya kuangalia kwenye setilaiti zake aliona kila kitu kipo sawa na kuamini kabisa anachokizungumza kilikuwa cha ndotoni. Lakini hakutaka kumnvunja nguvu kutokana na kumuamini sana. Alichukua maji ya manukato na kumpatia ili usiku ukiingia ajipake kufukuza nguvu za kijini.
“Hii itanisaidia?”
“Ndiyo.”
“Kwani babu tumekosea kitu gani mpaka leo kaja kama kwake?”
“Hatujakosea popote zile ni nguvu za kijini lakini hazina ubaya wowote. Kuja kwake pale ni kwa vile hakuwa na madhara kama angekuwa na madhara angekufa kabla hajakufikia. Aliyosema ni mkwara wa kukutisha ili uondoke lakini hawezi kufanya chochote.”
“Mmh! Afadhali, maana nilichanganyikiwa nilijua nimekwisha.”
“Pole mjukuu.”
“Asante.”
Baada ya kupewa moyo na mzee Mukti Buguju, Subira alirudi ofisini kuendelea na kazi lakini akiwa na wasiwasi wa usiku japokuwa maneno ya mzee Mukti yalimpa moyo.
***
Majira ya usiku baada ya chakula Subira alijipaka maji ya manukato aliyopewa mzee Mukti kisha alipanda kitandani.
Baada ya usingizi kumpitia alishtuka baada ya kumsikia mtu akimtikisa, alifumbua macho kuangalia ni nani alimtikisa. Alijikuta akishtuka baada ya kumuona Nargis akiwa katika vazi la kulalia amesimama pembeni ya kitanda. Alipoangalia pembeni Thabit alikuwa amepitiwa na usingizi.
“Nilikueleza nini?” Nargis alimuuliza kwa sauti ya upole.
Subira alibakia macho yamemtoka pima asijue ajibu nini, macho yake yake yalikataa yalichokiona na kuamini aliota ndoto. Sauti ya Nargis ilimrudisha kwenye akili yake halisi baada ya kuitwa jina lake.
“Subira, inawezekana hunijui ila kuanzia sasa utanitambua mimi ni nani,” bado Nargis alizungumza kwa sauti ya upole.
“Ni...ni...sa...”
“Subira naomba nikuulize swali jepesi, unanijua mimi?”
“Ndi...ndi...yo.”
“Kama nani?”
Subira alibakia macho yamemtoka pima asijue ajibu nini, macho yake yalikataa yalichokiona na kuamini aliota ndoto. Sauti ya Nargis ilimrudisha kwenye akili yake halisi baada ya kuitwa jina lake.
“Subira, inawezekana hunijui ila kuanzia sasa utanitambua mimi ni nani,” bado Nargis alizungumza kwa sauti ya upole.
“Ni...ni...sa...”
“Subira naomba nikuulize swali jepesi, unanijua mimi?”
“Ndi...ndi...yo.”
“Kama nani?” endelea...“
M...m...ke wa Thabit.”
“Nilikuambia nini asubuhi?”
“Ni...ni...ni..”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sikiliza kwa vile leo nimerudi kwa mume wangu naomba leo nikuoneshe sehemu ya kulala ambayo utalala siku zote.”
Baada ya kutoa kauli hiyo, alinyanyua mkono juu ghafla lilitokea jeneza pembeni ya kitanda. Aliliamuru kufunguka, likawa wazi.
“Naomba uingie ndani ya jeneza nakwenda kukuzika ukiwa hai.”
“Ni...ni...samehe...ni...ni...”
“Nilikueleza kiustaarabu lakini husikii sasa haya ni manyunyu tu ukizidisha ukaidi mvua ya mawe itakunyeshea. Ulidhamiria kuniua lakini mmeshindwa, nilikuwa na uwezo wa kukuua lakini siitaki dhambi ya kuua. ”
“Na...na...jua ni...ni...”
“Subira mimi ni jini, naweza kukufanya lolote pamoja na kujitahidi kunizuia kwa haki yangu, hivi kwa hali ya kawaida ungekuwa wewe umesafiri kwenda kwenu kujifungua halafu unarudi unakuta mumeo katekwa na mwanamke mwingine ungejisikiaje?
“Inawezekana upole wangu ndiyo unaokutia kiburi, sasa leo utanijua mimi ni nani.”
Alinyanyua tena mikono juu, ghafla sanda ilitua mikononi, alinyoosha mkono na kumpa Subira.
“Hii ndiyo shuka yako utakayojifunika huko utakapokwenda kulala.”
Alimuamuru avue nguo alizovaa wakati wa kulala, alimpa sanda na kujifunga kisha alimuamuru aingie kwenye jeneza. Subira huku akitetemeka alitembea taratibu kulifuata jeneza, alimwangalia mumewe aliyekuwa kwenye usingizi mzito bila kujua kilichokuwa kikiendelea muda ule.
Alitanguliza mguu mmoja ndani ya jeneza kisha aligeuza shigo kumwangalia Nargis ambaye wakati huo alikuwa amekaa kitandani akifikiri atamuonea huruma. Gauni alilovaa lilionesha mpaka ndani kuonesha hakuvaa nguo nyingine.
Huku machozi yakimtoka alitaka kuomba msamaha lakini jicho kali la mbaya wake lilimtisha. Nargis alimuonesha kwa ishara ya mkono aingie ndani ya jeneza huku akimweleza muda ulikwenda alitaka kulala. Subira aliingiza na mguu wa pili kisha alikaa na kujilaza chali.
Baada ya kujilaza, Nargis aliliamuru jeneza kujifunga kisha alilisafirisha hadi makaburini ambako kulikuwa na kaburi limechimbwa tayari.
Baada ya kufikishwa alitolewa ndani ya jeneza na kubebwa na viumbe wanne wa ajabu mpaka kwenye mwana ndani na kulazwa ndani yake kisha alisikia akiwekewa ubao na baada ya muda alisikia vishindo vya udongo kumjulisha alikuwa ndiyo anazikwa. Subira alijikuta akijilaumu kwa kudhulumu mume wa mtu na kukubaliana na usemi wa cha mtu sumu.
Baada ya vishindo vya muda ghafla hali ilikuwa kimya huku kiza kinene kikiwa kimetawala na kuamini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake ya duniani kwa kuzikwa akiwa hai. Kizunguzungu kikali kilimshika na kupoteza fahamu, kilichoendelea hakukijua tena.
Nargis baada ya miaka kumi na ushee alilala na mumewe kwa mara ya kwanza, lakini hakuyafurahia mapenzi kwa vile alikuwa na mumewe kama mtu aliyekuwa msukule usiyojua kitu chochote. Roho ilimuuma kwa vile uwepo wake pale Thabit hakuujua.
Alipata wazo la kurudi kwa mzee Dumidumzi kumweleza alichokikuta kwa mumewe, lakini aliona kwenda huko ni kutumia njia ndefu. Aliamini njia rahisi ni kurudi kwa mganga wa Subira mzee Mukti kuzungumza naye ili amrudishie mumewe kwa gharama yoyote kuliko kurudi katika miamba myeusi ambako hakuyapenda mateso yake mpaka kumfikia mzee Dumidumzi ilitakiwa moyo wa ziada.
Aliondoka alfajiri kwenda kwa mganga katika umbile la kibinadamu, alikuta wagonjwa waliolala pale wakipata tiba. Naye aliungana nao katika foleni ya kwenda kuonana na mganga, yeye alikuwa mtu wa nne. Baada ya wagonjwa waliotangulia kuingia Nargis naye akaingia baada ya saa nzima kupita tangu alipofika.
Aliingia kama mtu wa kawaida na kumkuta mzee Mukti amekaa kwenye kigoda chake cha kuagulia. Mpaka anaingia netiweki yake ilikuwa bado haijasoma kaingia nani, kwa kuwa Nargis alikuwa amejitanda ushungi aliuondoa na kubaki kichwa wazi na uso wake kuonekana uwazi.
Nargis alitikisa nywele na kumfanya aonekane kiumbe mrembo, ghafla nywele za Mukti zilianza kumsimama na kujikuta akishtuka alipomwangalia vizuri mteja wake aliona pembe ndogo katikati ya kichwa. Aligundua aliyekuwa mbele yake ni jini aliyekuwa akipigana naye ambaye jana yake alipata taarifa zake. Alijiuliza aliwezaje kuingia kwenye kilinge chake!
Kwa chati huku macho yake yakimwangalia usoni jini Nargis, alipeleka mkono kwenye dawa ili amzuie. Lakini kabla hajaishika Nargis alikinyooshea kidole kikopo chenye dawa ghafla kilianza kuwaka moto. Mzee Mukti alishtuka na kuona kapatikana kwa vile tangu aujue uganga hakuwahi kuchezewa kilinge chake na kiumbe chochote.
Kitendo cha jini Nargis kuingia ofisini kwake na kufanya dawa zake zishindwe kufanya kazi kilimchanganya sana na kuona amewahiwa. Aliona kilichokuwa kikitokea muda ule ni kama ndoto si kitu cha kweli. Alijifikisha macho ili apate ukweli kilichotokea kama kina ukweli na tukio lililotokea mbele yake. Baada ya tukio lile Nargis alicheka sana kisha alisema:
“Hongera umejitahidi lakini hapa ndipo mwisho wa matatizo, ila leo sikuja kwa shari nami nimekuja kama wateja wengine hivyo nataka msaada wako,” Nargis alisema kwa sauti ya upole.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment