Search This Blog

NILIOA JINI NIKAMSALITI - 5

 







    Simulizi : Nilioa Jini Nikamsaliti

    Sehemu Ya Tano (5)





    Alijifikisha macho ili apate ukweli kama tukio lililotokea mbele yake lilikuwa la kweli. Baada ya tukio lile Nargis alicheka kisha kwa upole alisema:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hongera umejitahidi lakini hapa ndipo mwisho wa matatizo, ila leo  sikuja kwa shari nami nimekuja kama wateja wengine hivyo nataka msaada wako.”



    Mzee Mukti akiwa bado mapigo ya moyo yapo juu na kijasho kiliendelea kumtoka, alijiuliza Nargis anataka msaada gani ikiwa tayari ameonesha ana uwezo mkubwa kuliko yeye. Huku akijitahidi kuficha hofu yake alimuuliza.



    “U...u...una...taka m...m...saada gani ewe jini mwana wa mfalme wa bahari ya dhahabu?”

    “Naomba kwanza suala la ujini liweke pembeni nami nakuja kama Subira alivyokuja, naitwa Nargis mke halali wa Thabit. Kwa hiyo nisaidie kama mwanadamu mwenye matatizo na si jini ndiyo maana nipo mbele yako kama mwanadamu.”

    “U...unataka msaada gani?”



    “Nataka unirudishie mume wangu mikononi mwangu.”

    “Nimrudishe vipi?”



    “Kama ulivyomtoa, najua umepewa fedha nyingi baada ya kuninyang’anya mume wangu. Nataka kukuambia ulichopewa na Subira, mimi nitakupa mara mia ili tu  unirudishie mume wangu. Mimi kweli ni jini lakini nina haki ya kuishi maisha nitakayo bila kumdhuru kiumbe yeyote.



    “Ni kweli mwanzo kabla ya kuwa mzazi nilikuwa sikubali kushindwa, nilipata dhambi nyingi kwa ajili ya kutoa roho za watu na majini kwa ajili ya kumlinda mume wangu. Lakini nimeona si lazima kutumia nguvu au kutoa uhai wa kiumbe kumlinda mume wangu.



    “Kipindi hiki cha kumtafuta mume wangu nimekutana na vikwazo vingi toka kwako nina imani uwezo wako ndiyo uliomfanya Subira akupe zawadi nyingi za nyumba na magari. Nilikuwa na uwezo wa kuviteketeza vyote ulivyopewa lakini sikutaka kufanya hivyo kwa vile kwangu mali si muhimu kama mume wangu.



    “Mali aliyokupa Subira ni yangu kwa vile hajui imepatikana vipi, mimi ndiye mmiliki wa mali yote aliyonayo Thabit. Kumbuka mali zote ziliteketezwa pamoja na uganga wako hukuweza kuzirudisha lakini nilizirudisha. Hata mume wangu alipopata matatizo usingeweza kumtibu, nilimtibu mwenyewe.

    “Huoni jinsi gani ninavyomjali mume wangu pia ni mzazi mwenzangu, kwa hiyo ninacho kuomba kikubwa nirudishie mume wangu. Sema unataka nikupe kitu gani ili unirudishie mume wangu.



    Hata wewe kama unasafiri kwenda nyumbani ukirudi ukute mkeo kipenzi kaolewa na mtu mwingine utajisikiaje tena kwa hila za huyo mwanaume? “Nina imani unajua maumivu yake kingine nimeteswa kwa haki yangu hivi hapa jini na mwanadamu nani mbaya?” Nargis aliuliza huku machozi ya uchungu yakimtoka na kuongeza uzuri wake mara kumi.



    “Mzee Mukti kwa nini unamlisha chakula asichokipenda mume wangu? Kwa nini unamlisha haramu? Subira yupo na mume wangu kwa nguvu za dawa yupo kama ndondocha. Sitaki nirudi nilipotoka kwani uvumilivu una kikomo, waganga wengi walikufa kwa ubishi hivyo sitegemei na wewe kuwa hivyo.

    “Lakini leo nimekuja kistaraabu, hivi mtu aliyedhamiria kukuua unaweza kuzungumza naye hivi?” Nargis alimuuliza mzee Mukti aliyekuwa amepigwa na butwaa macho yamemtoka pima.



    “Nakuuliza mzee wangu, mara ngapi mmepanga mipango ya kuniua lakini mmeshindwa. Lakini leo nakuja kwako kistaraabu hivi, kweli?”

    “Najua nazungumza maneno mengi bila vitendo,” Nargis alisema huku akinyanyuka kitendo kilichoongeza wasiwasi kwa mganga na kujua kumekucha.



    Lakini ilikuwa tofauti kwa Nargis ambaye alishika mkono kichwani kwa muda kisha alipiga kofi. Ghafla walitokea  viumbe wawili wamebeba mabegi mawili makubwa na kuyaweza mbele ya mganga. Baada ya kuweka Nargis alipiga kofi jingine lililowafanya viumbe wale kuyeyuka. Baada ya kutoweka Nargis alisema:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Mzee wangu, huu ni utajiri ambao utautumia mpaka kufa kwako hata kizazi chako kitakufa na kuuacha. Nina imani njaa ndiyo inayowafanya waganga wengi wawadhuru wasio na hatia. Nina imani nimeona jinsi gani ninavyompenda mume wangu.”



    Nargis alisema huku akifungua yale mabegi, moja lilikuwa limejaa fedha za mataifa mbalimbali na lingine lilikuwa na mchanganyiko wa madini yote ya thamani.

    “Sasa mama unataka msaada gani?” Mzee Mukti alichanganyikiwa na mali iliyokuwa mbele yake.

    “Kunirudishia mume wangu.”



    “Unataka nimfanye nini Subira?”

    “Sitaki umfanye kitu chochote kibaya, ninachotaka liondoe tandaburi ulilomvilingishia mume wangu ili arudi kwenye akili yake ya kawaida anitambue kama mimi ni mkewe wa halali. Najua kwa sasa umeifunga akili yake asinikumbuke na kufanya aamini kabisa mkewe ni Subira.”

    “Nitafanya hivyo, nakuahidi kazi hiyo nitaifanya mwenyewe.”



    “Sitaki uifanye wewe, nataka aifanye Subira mwenyewe kama alivyofanya mwanzo.”

    “Sawa nimekuelewa.”

    “Nina imani tutakwenda vizuri kama utafanya ninavyotaka.”

    “Nakuahidi kufanya kila ulichonieleza.”



    “Nitashukuru, naomba nikuache uendelee na wateja wengine.”

    “Hapana leo nitakuwa na kazi yako tu.”

    “Kuja kwangu kusiwe chanzo cha wengine kukosa huduma, najua lazima Subira atakuja hivyo utaanza hapo ila sasa hivi wahudumie wagonjwa wengine.”

    “Nashukuru kwa huruma yako.”



    Kama alivyoingia ndivyo alivyotoka katika umbile la kibinadamu na kuwaaga wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni. Baada ya kutoka Mukti alishusha pumzi ndefu asiamini kilichotokea.



    Alivuta begi kubwa na kuliangalia vizuri na kukuta limejaa fedha mchanganyiko za mataifa makubwa na za Tanzania.

    Alifungua begi la pili lililokuwa limejaa madini mchanganyiko na kumfanya mzee Mukti kupiga kelele za kupagawa na kuanza kujimwagia kitu kilichowashtua wasaidizi wake walioingia ndani na kukuta fedha na madini yametawanyika.



    “Nini mzee?” wasaidizi walimshangaa.

    “Sasa hivi mimi ni tajiri wa maisha.”

    “Hizi fedha na madini umetoa wapi?”

    “Ni Mungu tu.”



    Ghafla alitokea Nargis mbele yake na kumweleza afanye kazi kwanza, aliwaomba watoke na kuyaweka pembeni yale mabegi yenye fedha kisha aliendelea na kazi yake kama kawaida ya kuwahudumia wateja. Alijikuta akili yake ikimuwaza Subira na kutaka afike mapema.



    Alijikuta akimshangaa jini Nargis kuonesha huruma ya ajabu, lakini ingekuwa hiyari yake na utajiri kama ule angemfanya kitu kibaya kama si kumpa sumu ili kuwaacha Nargis na mumewe wafurahie ndoa yao. Lakini hakutaka kumfanyia baya lolote zaidi ya kurudi katika ndoa yake.

                                                          ***

    Kibaridi kikali cha alfajiri kilimwamsha Subira ambaye alipojigeuza alishangaa kujiona amebanwa na kitu. Alipofumbua macho alikutana na mwanga mkubwa ukitoka juu kuonesha yumo shimoni.  Alipojitahidi kunyanyuka  alishindwa kutokana na sehemu aliyowekwa ilikuwa ndogo na kumfanya asiweze kujitikisa.



    Ili apate msaada ilibidi apige kelele kuomba msaada kwa wapita njia, baada ya muda watu walikusanyika juu ya kaburi. Walishangaa kumwona mtu amelala kaburini akiwa amelazwa kwenye mwana ndani akiwa amefungwa sanda lakini pembeni ya kaburi hakukuwa na udogo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliingia ndani ya kaburi na kumtoa nje, watu wote walimshangaa na kutaka kujua kipi kilimsibu. Subira alishindwa kusema alikuwa akilia tu, kurudi nyumbani aliogopa aliomba msaada wa nguo. Baada ya kupatiwa pande mbili za kanga, aliomba msaada wa gari mpaka kwa rafiki yake ambaye alimshangaa kumwona yupo vile.



    Alimuomba kwanza ampe nguo zake kisha amuazime fedha ili aende Kigamboni kwa mzee Mukti kwani aliamini bwawa liliishaingia ruba lilikuwa haliogeki tena. Shoga yake alimpatia nguo baada ya kuoga. Kutokana na kuchanganyikiwa hata kula hakutaka.



    Alikodi gari hadi Kigamboni kwa mzee Mukti, kama kawaida alikuwa hakai foleni alikuwa akipitiliza na kwenda kukaa kwenye chumba maalumu alichotengewa na mganga kisha aliwatuma vijana wa mzee Mukti wakamwite kwani alionekana amechanganyikiwa.



    Mzee Mukti alikwenda kwenye chumba maalumu alichotenga kwa ajili ya kukutana na Subira kutokana umuhimu wake katika kuyabadili maisha yake. Lakini siku ile alimuona kama adui, bila Nargis angemfanya kitu kibaya baada ya akili yake kufikiria utajiri aliopewa.

    “Karibu,” mzee Mukti alificha chuki yake.

    “Asante.”



    “Mbona upo hivyo?”mzee Mukti alimshangaa jinsi alivyovaa na mwonekano wake kuonesha ana matatizo makubwa hakuwa Subira aliyemzoea kujiremba lakini siku ile alikuwa vululuvululu.

    “Babu mambo ni mabaya kuliko ulivyofikiria.”

    “Tatizo nini?”



    “Huwezi kuamini kilichonitokea, mimi wa kulala kaburini nimevishwa sanda?” Subira alisema huku akilia.

    “Sijakuelewa una maanisha nini?”



    Subira alimweleza kilichotokea usiku wakati akiwa kitandani alipotokewa na jini Nargis ambaye alimvisha sanda kama maiti na kupelekwa kulala ndani ya kaburi tena kwenye mwana ndani na jinsi alivyookolewa na watu na kutolewa ndani ya kaburi.



    “Duh!” mzee Mukti alishtuka baada kusikia uwezo mkubwa wa Jini Nargis kwa kuvunja nguvu zake zote alizoweka na kufanya anavyotaka.Kwa mara ya kwanza aliamini uchawi unazidiana na kushangaa kama Nargis alikuwa na uwezo wa kuingia kila kona na kufanya aliyoyafanya kulikuwa na umuhimu gani wa kumpa utajiri ili amrudishie mumewe mkononi mwake. Wasiwasi wake alijua lazima alikuwa akimtega kama akikaidi basi naye amtie adabu.



    “Mzee wangu naumbuka kwani tumekosea wapi mpaka imekuwa hivi?”

    “Mmh! Hebu subiri.”Mzee Mukti alitoka na kumwacha Subira akiwa ameshika tama asijue hatima yake, mzee Mukti aliamini ile ndiyo ilikuwa nafasi yake ya kulirudisha penzi la Nargis kwa mumewe. Alitumia nafasi ile kufungua vifungo vyote alivyomfunga Thabit, baada ya kuandaa dawa ya kuvunja kila alichokifanya ili Thabit ampende Subira.



    Baada ya kuandaa dawa alirudi chumbani na kumpa Subira, alipofika alimpa dawa za kuoga, kuweka katika chakula, kinywaji na kuweka katika maji ya kunyunyizia  kuzunguka nyumba nzima.

    “Hebu kafanye hivi.”



    “Mzee wangu mbona kama dawa ulizokuwa ukinipa zamani, zitaweza kweli?”

    “Mama, mimi ndiye mganga, hebu kafanye niliyokuelekeza.”

    “Mmh! Sawa, naweza kurudi nyumbani kwangu?” Subira aliisha ingia woga.

    “Nenda tu wala usiogope.”



    “Yaani nakwenda lakini nimeingiwa woga kweli.”

    “Ukiingia vitani usiogope kupigwa lazima upambane na si kuogopa.”

    “Kwa nini tusiende wote, yaani naogopa.”“Hakuna kitu we nenda tu.”

    “Mmh! Sawa,” Subira alisema na kunyanyuka kuelekea nje ili aelekee kwake ambako alipaona panawaka moto.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Subira alirudi nyumbani akiwa hajiamini kwani wasiwasi wake wote ulikuwa kwa Jini Nargis mwanamke halali wa Thabit aliyempindua. Alikodi gari hadi nyumbani kwake, bahati nzuri alimkuta mumewe Thabit bado yupo nyumbani.



    Alimshangaa mkewe mavazi aliyovaa na asubuhi ile alikuwa akitoka wapi.

    “Mke wangu unatoka wapi asubuhi yote hii na ulikuwa wapi?”

    “Mume wangu nitakueleza naomba uniache nipumzike kwanza mengine tutazungumza baadaye.”

    “Sawa, vipi kazini huendi?”

    “Naenda.”



    “Basi fanya haraka tuondoke mengine tutazungumza jioni tukirudi.”

    “Sawa mume wangu, naomba nikaoge ili nikuandalie kifungua kinywa.”

    “Sawa mke wangu fanya haraka.”



    Subira alishangaa Thabit kuendelea kumwita mkewe pamoja na kulala na mkewe jini, alikwenda kuoga maji aliyochanganya dawa aliyopewa na mzee Mukti. Baada kuoga alimwita na Thabit kuoga maji ya dawa. Mumewe aliingia bafuni na kuoga bila kujua maji aliyokuwa akioga yalikuwa na dawa.



    Baada ya kuoga alimwandalia kifungua kinywa kama kawaida na kuweka dawa kwenye chakula. Baada ya kuweka dawa alimpelekea chakula ambacho walikula pamoja. Kila alivyokuwa akila na kunywa alihisi kuona kama maluweluwe machoni mwake.



    “Subira,” alimwita baada ya kushindwa kujielewa.

    “Nini mume wangu?”“Au basi,” alijibu baada ya hali kutulia.

    “Niambie mume wangu kuna nini?”

    “Walaa, tuwahi kazini.”

    “Sawa.”



    Kabla ya kuondoka  Subira alimuacha ndani Thabit na kuzunguka nyumba kunyunyuzia dawa aliyopewa na mganga. Alifanya kwa haraka kisha alirudi ndani na kumweleza mumewe.

     “Mume wangu twende zetu,” Subira alisema huku akimshika mkono wawahi kazini.



    Walitoka pamoja na kuingia ndani ya gari kuwahi kazini, walipofika waliendelea na kazi kama kawaida huku Thabit akiwa hajielewi baada ya kuingiwa na kumbukumbu ya ghafla ya Nargis.

    “Mmh! Nargis...Nargis...ni...ni...nani? Hapana si...si mke wangu..Mungu wangu na...na Subira ni nani yangu? Hebu,” alinyanyua simu na kubofya namba kisha alizungumza.

    “Subira.”

    “Abee.”



    “Njoo mara moja.”

    “Nakuja.”

    Baada ya muda Subira aliingia ofisini kwa Thabit na kusimama mbele kusikiliza wito.

    “Subira.”

    “Abee.”



    “Eti wewe hapa ofisini ni nani?”

    “Mume wangu, swali gani hilo?”

    “Umeniitaje?”

    “Mume wangu.”



    “Mimi mumeo! Tokea lini?”

    “Thabit mume wangu upo sawa?”

    “Nipo sawa.”

    “Kwa nini unaniuliza swali hilo?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna kitu kinanichanganya!”

    “Kitu gani hicho?”

    “Kwanza kuna pete niliyokuwa navaa ipo wapi?”

    “Si...si...jui!”



    “Halafu wewe ni msaidizi wangu, mke na mume imeanza lini?” Thabit alishangaa.

    “Thabit mume wangu wewe ndiye uliyeniomba niwe mkeo na kufuata taratibu zote nashangaa leo kuniuliza hivyo?”

    “Mimi nilikuoa wewe?”

    “Ndiyo.”



    “Mimi kweli! Thabit nilikuoa wewe na kuwa mke na mume?” Thabit alizidi kushangaa.

    “Ndiyo na sasa hivi tuna miaka zaidi ya mitano.”

    “Mmh! Siamini...siamini, mimi nina mke.”

    “Ndiye mimi.”



    “Hapana mke wangu anaitwa Nargis.”

    “Mume wangu leo umekuwaje?” Subira alisema huku akitoka ofisini na kurudi na picha iliyokuwa kwenye flemu ya siku yao ya harusi wakiwa wamepozi na kuipeleka mbele ya Thabit.



    “Mume wangu hii nini?” Subira alimuonesha Thabit picha yao ya harusi.

    “Mmh! Hii harusi ulifunga na mimi?” Thabit alizidi kushangaa huku akitazama picha ya harusi yao kama ndiyo siku ya kwanza kuiona.



    “Thabit mume wangu umekuwaje leo, asubuhi tumetoka pamoja na siku zote tupo pamoja kipi cha ajabu kwa leo?” Subira alizidi kushangaa mabadiliko ya ghafla ya mume wake.

    “Bado naona mauzauza.”

    “Mauzauza gani jamani?’



    “Naomba uniache kwa muda nitakupigia baadaye.”

    Subira alitoka ofisini kwa Thabit akiwa amechanganyikwa asijue nini kimetokea kwani kila dakika mambo yalizidi kumchanganya. Kwa haraka alichukuwa simu kumpigia mzee Mukti ili amweleze kilichotokea kwani ni muda mfupi toka atoke kwake na kupewa dawa ambayo badala ya kupunguza imeongeza matatizo.



    Baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili:

    “Haloo.”

    “Haloo babu mbona mambo huku yanazidi kuwa magumu?”

    “Kivipi?” Mzee Mukti alijifanya hajui kitu.



    Subira alimweleza kilichotokea muda mfupi, mumewe kumshangaa na kumwona si mkewe. Mzee Mukti aliamini kazi aliyotumwa na Nargis ilikuwa imekwisha, alishusha pumzi na kusema:

    “Mmh! Mambo mazito, inaonekana uwezo wangu umefikia mwisho.”

    “Mungu wangu sasa itakuwaje?”



    “Kwani anasemaje?”

    “Kama nilivyokueleza anashangaa hata picha za harusi yetu na kuuliza ile picha kama ni yake huoni kama naumbuka mwenzio?”

    “Mmh! Kweli kazi ipo.”

    “Mzee wangu fanya uwezavyo ili mambo yawe sawa nakuahidi kukupa chochote ukitakacho.”

    “Nina ushauri mmoja.”

    “Ushauri gani?”



    “Nakuomba umuachie mume wake?”

    “Eti nini?” Subira alishtushwa na kauli ya  mzee Mukti.

    “Njia rahisi ya kumaliza suala hili ni kuachana na mumewe lakini zaidi hapo nauona mwisho wake ni mbaya.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sikubali nimeishapoteza fedha nyingi kwa ajili ya kulinda ndoa yangu, lazima niipiganie,” Subira hakukubali kirahisi.

    “Lakini si unajua Thabit ni mume wa Nargis?”

    “Hata kama, mimi ni mwanadamu na yule ni jini hivyo mwenye nafasi kubwa ni mimi kwa vile ndoa ya halali ni mwanadamu kwa mwanadamu.”



    “Unajua mwenye haki ni huyo jini na sasa hivi ana nguvu mara mbili ukishindana naye utakufa unajiona.”

    “Bora nife lakini sikubali lazima nipambane.”

    “Nakuhakikishia kama kwangu umeshindwa hakuna sehemu yoyote utakapopata msaada.”

    “Siamini, wewe si mganga wa mwisho nitahakikisha namrudisha mikononi mwangu,” Subira alisema kwa hasira.



    “Sawa, lakini kwa ushauri wangu achana na mume wa Nargis yatakukuta makubwa.”

    “Leo ndiyo umeyaona hayo?”

    “Subira acha ubishi hata huo utajiri ni wa huyo mwanamke.”

    “Hakuna ni wa Thabit si wa jini wako.”

    “He! Ameisha kuwa jini wangu! Subira ninayokueleza haya ni kwa ajili ya kukupenda, lakini kama huyo jini angekuwa na roho mbaya angeweza kutuua wote.”

    “Umejuaje?”



    “Kuna siri nzito nilikuficha juu ya yule jini, ndiye aliyerudisha mali zilizopotea na ndiye aliyemponya Thabit kwa vile ni mume wake. Amekosa kuniua zaidi ya mara nne na kunieleza kama ninataka usalama wangu na wako basi tumrudishe mumewe mikononi mwake la sivyo atatupoteza wote.”

    “Mzee Mukti, wewe si ulinieleza kuwa wewe ni kiboko ya majini?”

    “Ni kweli lakini imeonekana Nargis ana nguvu za ziada tofauti na mwanzo tulivyomfanya.”

    “Ndiyo maana nikasema wewe si mganga wa mwisho kama uwezo wako umeishia hapo wapo wenye kukuzidi.”



    ”Sawa, lakini nakuomba kwa usalama wako achana na Thabit kwa vile mwenye mali amerudi kama alikulaza kwenye kaburi anaweza kukufanya chochote anachotaka.”

    “Sikubali nipo radhi kufa lakini nimrudishe mume wangu.”

    “Kila la heri.”



    Subira akiwa amechanganyikiwa alibeba mkoba wake bila kumuaga mumewe na kutoka nje. Alikumbuka kuna mganga mmoja anasifika sana maeneo ya Bunju, aliingia kwenye gari na kuondoka. Alipofika Bunju hakujua yupo wapi, ilibidi ampigie shoga yake ambaye alikuwa akiwafahamu waganga kila kona.



    “Nenda mpaka Bunju mwisho kisha ulizia Moboja, ni maarufu sana.”

    Baada ya kuelekezwa vile alisogea pembeni ya barabara kulikokuwa na vijana wenye bodaboda. Aliteremsha kikoo na kumwita mmoja aliyekuwa amesimama pembeni.

    “Samahani kaka naomba nikuulize.”



    Yule kijana alisogea hadi kwenye gari la Subira na kuuliza:

    “Unasemaje Sister?”

    “Eti unamjua mganga anayeitwa Moboja?”

    “Si yule anakaa mpakani?”



    “Hata najua, kuna mtu kanielekeza anakaa Bunju.”

    “Mimi namjua yule wa mpakani?”

    “Labda ndiye yeye si mwanamke?”

    “Ndiyo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Basi atakuwa yeye.”

    “Basi nenda mpaka ukikaribia daraja linalotenganisha Bunju na Bagamoyo, kata kulia kuna njia ndogo lakini gari linafika fuata barabara hiyo mpaka mbele utaona nyumba ina kitambaa chekundu juu ya mti kama bendera ndipo hapo.”

    “Asante kaka yangu,” Subira alisema huku akimpatia elfu mbili kisha aliwasha gari na kuondoka kuelekea kwa mganga.



    Alifuata barabara mpaka alipokaribia kwenye daraja alikata kulia na kuifuata njia alipofika mbele aliona nyumba yenye bendera nyekundu. Aliamini ni pale alipoelekezwa alisimamisha gari. Aliteremka na kuelekea kwenye nyumba kwa kuingia mlango wa uani ambako alikuta kuna wagonjwa waliokuwa wakipata matibabu na wengine wakiwa kwenye foleni ya kumuona mganga.

    Baada ya kuwasalimia alikaa pembeni kusubiri zamu yake, baada ya dakika arobaini aliitwa ndani kwenda kuonana na mganga. Baada ya kukaa na kusalimiana alitulia kumsikiliza.

    “Karibu.”



    “Asante.”

    “Una tatizo gani?”

    “Ndoa yangu imeingia katika matatizo baada ya jini mmoja kutaka kumchukuwa mume wangu. Naomba msaada wako ili kuhakikisha mume wangu hachukuliwi kwa gharama yoyote. Tena ukifanikisha kumbakisha mume wangu nitakupa zawadi kubwa ambayo hutaisahau maishani mwako.”



    Baada ya kumweleza mganga alitulia kwa muda na kuchukuwa mtandio mwekundu na kujifunika usoni ili ampigie ramli. Aliwasha udi na kuufusha kisha aliuweka chini ya kitambaa na kuvuta moshi wake baada ya muda alisikika akiguna peke yake na kusema kwa sauti nyembamba.

    “Ewe mwanadamu una shida gani?”



    “Nataka kuchukuliwa mume wangu.”

    “Mbona unasema uongo?”

    “Kweli huu ni mwaka wa tano nipo ndani ya ndoa yangu.”





    “Mbona kuna aliyeanza kuwa katika ndoa kabla yako?”

    “Ni kweli, lakini naomba msaada wako.”

    “Sasa nimsaidie nani mwenye mali au wewe?” Mganga aliuliza.

    “Kivipi?” Subira hakumwelewa mganga.



    “Mwenye mume ametoka hapa kuomba nisiiguse ndoa yake la sivyo atanifanya kitu kibaya.”

    “Lakini wewe si mganga, hawezi kukutisha.”

    “Ni kweli lakini si wakuharibu mambo ya watu.”

    “Kwa hiyo huwezi kunisaidia.”



    “Sina msaada zaidi ya wewe kumwachia mume wake, zaidi ya hapo utatafuta matatizo.”

    “Kwa hiyo umeshindwa?” Subira aliuliza.

    “Sijashindwa bali huo ndiyo ukweli, hebu angalia pembeni yako,” mganga alisema akiwa bado amejifunika kichwani.

    “Nini?” Subira aliuliza huku  akigeuka kuangalia pembeni yake lakini hakuona kitu.

    “Mbona hakuna kitu, kuna nini?”

    “Umeangalia vizuri?”

    “Ndiyo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona mimi naona.”

    Kauli ya mganga ilimfanya Subira ageuke tena kuangalia pembeni japokuwa mwanzo hakuona kitu chochote. Alipoangalia pembeni kwa mara ya pili hakuona kitu aligeuka ili amuulize mganga aliyemuona alimchezea akili baada ya kazi kumshinda. Macho yake yalishtuka baada ya kumuona mtu tofauti na mganga aliyekuwa amekaa mbele yake.

    “He!” Alishtuka na kushika mkono kifuani kwa mshtuko.

    “Unashtuka nini?” aliyekuwa mbele yake alimuuliza.

    “Ha...ha...pana, ni...ni...sa...mehe.”

    “Nikusamehe nini?”



    “Ni...ni...me...me...ku...wa si...si...sikii,” Subira alipata kigugumizi cha ghafla.

    “Sikiliza Subira nina imani kote ulipopita umeelezwa vizuri mimi ni nani na nina nguvu gani. Najua una tamaa ya mali, sikiliza sasa hivi sitaki shari na wanadamu ndiyo maana sitaki kukufanyia lolote baya. Sasa nieleze unataka nini ili uachane na mume wangu?” Subira aliulizwa kwa sauti ya upole tofauti na alivyotegemea.



    “Si...si...taki chochote,” alijibu huku akitetemeka.

    “Sema ukweli ulio ndani ya moyo  unataka nikupe nini uachane na mume wangu, kwa ulichonifanyia nilikuwa ninawezo wa kuua au kukugeuza kiumbe cha ajabu. Lakini namshukuru Mungu amenipa subira na akili ya kuushinda mtihani huu. Mpaka unahangaika kwa waganga ulijua kabisa Thabit ni mume wangu na utajiri aliona ni mimi nimempa lakini ulijitoa akili .



    “Ni kweli mimi ni jini na mwanaume niliyemchagua katika viumbe wanadamu ni Thabit baba wa watoto wangu Zumza na Zamzu. Hivi kweli hata akili ya kawaida tu, mfano wewe usafiri kwenda kwenu kujifungua nyuma aje mwanamke amchukue mumeo kwa nguvu za kichawi utajisikiaje?”

    “Nitajisikia vibaya.”

    “Utakubali kumwachia mumeo mpenzi?”

    “Hapana.”

    “Utafanyaje?”



    “Nitapambana ili kumrudisha.”

    “Nina imani jibu unalo, nafahamu ungekuwa wewe mtu huyo ungemuua hata kwa risasi, hali hii Thabit mume wangu wa halali umetaka kuniua vipi angekuwa mumeo mimi ni mwizi?”

    “Ni...ni...sa...samehe dada yangu,” Subira alipiga magoti.



    “Nataka kukueleza jambo moja dogo, ili ninalokupa ni onyo la mwisho. Naomba uachane kabisa na mume wangu. Nakuahidi ukiachana na mume wangu nitakupa zawadi nzuuuri.”

    “Nimekuelewa dada yangu, sasa nikitoka hapa niende wapi?”



    “Ooh! Swali zuri, kuna nyumba nimekutafutia utakaa hapo maisha yako yote masharti yake usiiuze tu.  Kwa sasa utakwenda kumueleza ukweli Thabit kuwa wewe si mkewe kisha utaondoka, ukiondoka usirudi tena kazini, nimetafuta wafanyakazi wengine.”

    “Sawa, hapo uliponitafutia nitapajuaje?”

    “Ukitoka ofisini kwa Thabit  kabla ya kuvuka mlango fumba macho ukitoka nje tu utajikuta kwako.”

    “Sawa.”



    Ghafla Subira alishangaa kujikuta mbele ya mganga ambaye muda huo alikuwa akinyanyua kitambaa alichojifunika kupiga ramli na kunyoosha mkono kuchukua maji. Alijinyoosha kuonyesha alichoka sana kisha alisema:



    “Dada ondoka, kazi yako nzito, nilikuwa nakufa najiona angeendelea dakika tano ningekufa.”

    “Angeendelea nani?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Binti hebu ondoka ukizidi kukaa hapa utanitafutia matatizo,” mganga alizungumza kwa wasiwasi huku akimeza funda la maji na kujishika shingoni kama mtu aliyekabwa.

    “Kwani umepatwa na nini?” Subira alijikuta akimshangaa mganga.

    “We’ mwana umetumwa? Hebu ondoka, kumbe ulipotoka ulimshindwa umekuja kunitafutia matatizo bure nikifa familia yangu utaitunza wewe?”

    “Mmh! Makubwa.”



    Subira alijikuta akichanganyikiwa asijue nini kimetokea, kwani muda mfupi alikuwa akizungumza na Nargis na ghafla tena akawa anazungumza na mganga, alijiuliza kile ni nini. Kwani baada ya kuzungumza na mganga ghafla akaja Nargis mara tena akarudi mganga.



    Japokuwa alijiona kama yupo ndotoni lakini maneno ya Nargis yalikuwa na ukweli hivyo alitakiwa kuyafuata kwa usalama wa maisha yake. Hakutaka kuendelea kuwa pale kwani kila dakika mganga alipandisha hasira. Alinyanyuka na kutoka nje na kwenda kwenye gari lake na kurudi moja kwa moja ofisini kufanya aliyoelezwa na Nargis.



    Aliendesha gari mpaka ofisini na kwenda moja kwa moja ofisini kwa Thabit na kuingia. Thabit alipomuona alishtuka na kumuuliza:

    “Subira ulikuwa wapi?”

    “Thabit naomba unisamehe.”

    “Nimekusamehe, kaendelee na kazi.”

    “Hapana kuna kitu nataka kuzungumza na wewe.”



    “Kitu gani?”

    Kuhusu mimi na wewe.”

    “Kitu gani hicho?”

    “Eti mimi na wewe tupo vipi?”

    “Subira swali gani hilo?” Thabit alishangaa.



    “Thabit naomba kuanzia leo uendelee na mkeo Nargis, mimi si mkeo.”

    “Kwani wewe ndiye unayeongoza maisha yangu kwanza nani kakupa jeuri ya kusema hivyo?”

    “Na kazi ndiyo mwisho.”



    “Mbona sikuelewi, kama umeamua mwenyewe sawa.”

    Subira alishangaa na kuamini kila chenye mwanzo kina mwisho, kwa hali ile ilionesha Thabiti alirudi katika hali yake ya kawaida. Hakuongeza neno alinyanyuka na kutoka nje ya ofisi. Kabla ya kuvuka mlango wa kutoka nje alifumba macho na kutoka, ghafla alijikuta kwenye nyumba nzuri. Hakuamini alibakia amesimama kama mgeni, mara alisikia hodi.



    Hakujibu haraka, aliusogelea mlango na kuufungua, alishtuka kumuona Nargis akiwa amesimama.

    “Ka...ka...ribu,” aliingia wasiwasi.

    “Asante,” Nargis alisema huku akiingia ndani.



    “Ka...karibu,” Subira alimkaribisha huku akitetemeka.

    “Acha woga, hukuogopa ulipotaka kuniua uniogope nikiwa hivi.”

    “Sa...sa...mahani dada Na...na...”

    “Nargis,” Nargis alimalizia jina lake.

    “Karibu dada.”



    “Asante,” Nargis alijibu huku akikaa.

    “Dada mimi ndo’ nafika hata sijui nyumba ikoje,” Subira alizungumza kwa unyenyekevu.

    “Utajua kwa vile ni kwako, mi si mkaaji nimekuja kukumbusha tena achana kabisa na mume wangu ukijitia kiburi cha nazi kushindana na jiwe sitakuua nitakugeuza nzi wa chooni  maisha yako yote yatakuwa kwenye kinyesi.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dada nakuapia kuanzia leo sitamfuata mumeo, nashukuru kwa kunisamehe kwa ubaya wote niliokufanyia.”“Hilo si la muhimu kwangu zaidi ya kukukanya kwa mara ya mwisho.”

    “Nakuahidi sitamsogelea tena, hivi nimetoka kumweleza pia kuacha kazi.”

    “Nashukuru kama umenielewa.”



    Baada ya kuachana na Subira, Nargis alirudi moja kwa moja ofisini kwa Thabit ili kuhakikisha kama kweli dawa za Subira alizopewa na mganga zimefanya kazi. Baada ya kufika eneo la ofisi za Thabit alitembea taratibu. Alijishangaa alivyokuwa mwepesi kila alivyotembea tofauti na siku za nyuma.



    Alimsalimia mlinzi ambaye alimpokea na kujikuta akimuuliza.

    “Shemeji ni wewe?”

    “Ni mimi John.”

    “Karibu.”



    “Asante, mheshimiwa yupo?”

    “Ndiyo.”

    Wakati huo Nargis alikuwa ameishamweka jini sehemu ya mapokezi mwenye sura ya Subira ili asiwachanganye watu. Alipomuona alimkaribisha.

    “Karibu binti wa mfalme.”



    “Asante,” Nargis alijibu huku akiingia ofisini  kwa Thabit.

    Wakati huo Thabit alikuwa ameinama akiishangaa picha yake na Subira ambayo ilimshangaza sana kila alivyojiuliza alikosa jibu. Alijiangalia mkononi na kutandaza vidole kuangalia pete aliyoachiwa na mpenzi wake haikuwepo. Alijuliza kipi kimepita kwani alishindwa kuelewa nini kinaendelea.



    Moyo wake ulijaa wasiwasi na kujiuliza kama mkewe Nargis angetokea siku ile na kukuta hali ile lazima angeonekana msaliti.  Alipata wazo la kuziondoa picha zote alizokuwa amepiga na Subira wakionekana wapenzi kitu ambacho yeye kwa akili zake alikuwa hakumbuki kabisa kama aliwahi kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote zaidi ya Subira.



    Akiwa bado katika dimbwi la mawazo aliisikia sauti ya Nargis siku alipokuwa akiondoka kwenda kwao ujinini kujifungua: “Thabit naondoka nikiwa nimekuachia utajiri mkubwa ambao hutaumaliza mpaka unakufa, unajua kiasi gani nilivyopigana na majini wenzangu na wanadamu kukulinda.



    Nina dhambi ya kuua majini na wanadamu kwa ajili yako. Nimewatia wanadamu na majini vilema ambavyo watakufa navyo kwa ajili yako. Thabit naondoka nakuacha peke yako, kwa utajiri ulionao una mtihani mzito kwa wanadamu kila mwanamke atakutaka wapo watakaokuendea kwa waganga ili wakupate. Kipindi changu cha kujifungua sitaweza kutoka mpaka miaka kumi hivyo sitakuwa karibu na wewe tena.



    “Mpenzi naomba usinisaliti nimechoka kubeba dhambi za wanadamu na majini kwa ajili yako. Nakuomba baada ya kuondoka kaa mbali na wanadamu, mafuta niliyokuachia siku ukinikumbuka sana jipake usiku wakati wa kulala utaniota usingizini lakini hatutaonana mpaka miaka kumi ipite,” Nargis alisema kwa hisia kali.



    “Nakuahidi kuwa muaminifu kwako, sitakusaliti nakupenda sana Nargis, nilitamani niwapokee wanangu wakati wa kuzaliwa lakini sina jinsi. Nenda mpenzi wangu ukijua nakupenda kuliko kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu. Nakuahidi kukusubiri hata kwa miaka mia moja,” Thabit alimuahidi Nargis.

    “Kweli Thabit?” Nargis alimuuliza Thabit huku akimkazia macho yake makubwa lakini yenye urembo wa ajabu.



    “Kweli kabisa.”

    “Hutanisaliti?” alimuuliza tena.

    “Siwezi.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuyakumbuka maneno ya zaidi ya miaka kumi iliyopita alijikuta mapigo ya moyo yakimwenda mbio na kujiuliza Nargis akitokea na kuona zile picha alizopiga na Subira atamuona mnafiki na muongo. Wazo lilikuwa kuzitoa picha zote na kuzichoma moto.



    Akiwa katika mawazo mazito alisikia mtu akibisha hodi, alitulia bila kujibu huku macho yake yakitua kwenye picha kubwa ya Subira akiwa katika tabasamu pana iliyokuwa mbele yake ambayo siku ile lilikuwa tabasamu baya kama amemuona mtoa roho mbele yake.



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog